Saturday, October 1, 2011

Kazi Niliyofanya Tanzania Mwaka Huu

Kuanzia tarehe 7 Agosti hadi Septemba 5, nilikuwa na shughuli ya kuwatembeza wanafunzi wa ki-Marekani nchini Tanzania, katika programu ya LCCT. Ingawa tulipita katika maeneo mbali mbali, yakiwemo yale ya utalii, ziara yetu haikuwa ya utalii kwa namna dhana hiyo inavyoeleweka. Kila tulipopita palikuwa ni fursa ya kujifunza mambo ya historia, uchumi, siasa, utamaduni, na kadhalika. Hapa kushoto naonekana nikijiandaa kuongoza mjadala mojawapo, Dar es Salaam.

Kabla ya kuja Tanzania, wanafunzi wanatakiwa kusoma vitabu ambavyo ni mapendekezo ya LCCT. Kwa mwaka huu vitabu hivyo ni hivi hapa:

1) The Rough Guide to Tanzania, 3rd edition, mtunzi Jens Finke (Rough Guides, 2010)

2) The Legacies of Julius Nyerere: Influences on Development Discourse and Practice in Africa, wahariri David A. McDonald and Eunice Njeri Sahle (Africa World Press, 2002)

3) The Worlds of a Maasai Warrior: An Autobiography, mtunzi Tepilit Ole Saitoti (University of California Press, 1986)

4) Parched Earth, mtunzi Elieshi Lema (E&D Publishers, Limited, 2001)

5) Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, mtunzi Joseph Mbele (Africonexion, 2005)

Hivyo ndivyo vilikuwa vitabu muhimu, na LCCT ilivinunua na kuwapelekea wanafunzi mapema kabisa. Lakini kulikuwa pia na orodha ya vitabu vya ziada, vinavyohusu siasa, elimu, masuala ya jinsia. Pia kulikuwa na riwaya mbili tatu.

Nashukuru kwamba wanafunzi hao wamepata fursa ya kuyafahamu maeneo mbali mbali ya nchi yetu na kujifunza mengi. Sasa wanangojea tu chuo kikuu cha Dar es Salaam kifunguliwe ili waanze masomo pale, kwa muhula mmoja.

Kazi yangu haijaisha, ingawa nimesharejea tena Marekani. Ninatakiwa kufuatilia maendeleo ya wanafunzi hao na kupokea na kutathmini taarifa na makala ambazo wanapaswa kuandika, hadi watakapomaliza muhula wa Chuo Kikuu Dar katikati ya mwezi Desemba.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...