Tuesday, January 20, 2015

Mihadhara Nisiyolipwa

Nimewahi kuongelea suala la kulipwa ninapotoa mihadhara. Nilisema kuwa wa-Marekani wanapokualika kutoa mhadhara huuliza malipo yako ni kiasi gani. Nilitamka kuwa huwa sitaji kiasi ninachotaka kulipwa, bali nawaachia wanaonialika waamue kufuatana na uwezo wao. Hata kama hawana uwezo, niko tayari kuwatimizia ombi lao.

Napenda kufafanua kidogo kuhusu utoaji wa mihadhara bila kulipwa. Labda wako watu ambao watashangaa kwa nini ninaridhika kutoa mihadhara ya aina hiyo. Labda wako watakaosema ninapoteza muda wangu. Huenda wengine wataniona nimechanganyikiwa. Ni jambo la kawaida kwetu wanadamu kuwa na fikra na mitazamo inayotofautiana.

Nina sababu zangu kwa kuwa na huu msimamo wangu. Kwanza ninatanguliza ubinadamu na utu, sio hela. Kuwasaidia wengine ni jambo jema sana, ambalo lina maana kuliko hela. Unaweza kuwa na hela nyingi ukazifuja, zisikuletee faida yoyote maishani, lakini, kama walivyosema wahenga, wema hauozi.

Kuna usemi mwingine, "Tenda wema nenda zako; usingoje shukrani." Ni usemi unaoniongoza na kunipa faraja maishani. Nazingatia kuwa kuna Mungu, ambae ndiye anayenipa uzima siku hadi siku, na akili timamu ya kuweza kuelewa mambo na kuwafundisha wengine. Siwezi kujivunia au kuringia vipaji alivyonipa Mungu, kwani ni dhamana kwa manufaa ya walimwengu. Falsafa hii inanitosha kikamilifu.

Ninapotoa mhadhara popote, kwa watu wenye kunilipa, wasio na uwezo wa kunilipa, au wenye uwezo kidogo sana, ninajua kuwa ni fursa ya mimi kujiongezea uzoefu na elimu, hasa wakati ninapojiandaa na wakati wa masuali na majibu. Uzoefu na elimu ni bora kuliko hela. Ni mtaji  unaoweza kutumiwa kuzalisha hela nyingi. Huenda ni mtaji imara kuliko yote.

Nilipwe nisilipwe, ninapotoa mhadhara ninalichukulia jukumu langu kwa dhati na umakini wa hali ya juu. Ninajua kuwa ni fursa ya kujinadi, bila mimi kulipia, kama tunavyolipia matangazo. Kwa ufafanuzi zaidi, napenda niseme kuwa mihadhara ninayoongelea hapa aghalabu huhusu masuala ya elimu na tofauti za tamaduni na athari zake katika dunia ya utandawazi wa leo. Wanaonialika hufanya hivyo kutokana na kusoma maandishi yangu, kama vile kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kwenye mhadhara, nakala zinakuwepo na zinauzwa.

Kutoa mihadhara bila kulipwa si kupoteza muda wala si hasara. Ni aina ya uwekezaji. Huwezi kujua hao wanaokusikiliza ni watu wa aina gani. Huenda wako ambao wana uwezo wa kukuunganisha na jumuia, taasisi au kampuni zitakazopenda kukualika na zenye uwezo wa kukulipa. Mungu husawazisha yote, tena kwa namna tusiyotegemea. Narudi kwenye usemi kuwa wema hauozi. Kukataa kuwahudumia watu kwa vile tu hawana uwezo wa kukulipa ni kukosa upeo wa kuona mbali.

Nimeona niseme hayo machache, kujiwekea kumbukumbu za mtazamo wangu kwa wakati huu. Akili yangu haijasimama, bado natafakari masuala ya aina hii, na hakuna ubaya iwapo nitarejea tena siku za usoni na kufafanua zaidi mtazamo wangu, kuongeza na kuboresha, au kurekebisha baadhi ya vipengele vyake. Ni matumaini yangu kuwa wako ambao watajifunza kitu kutokana na mawazo yangu.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...