Umuhimu wa Warsha Zangu

Sijui kama kuna jambo ninaloongelea mara nyingi zaidi katika blogu hii kuliko suala la tofauti za tamaduni duniani, athari zake, na umuhimu wa kuzielewa. Ni suala muhimu sana, hasa katika dunia hii ya utandawazi.

Nimekuwa nikiendesha warsha kuhusu masuala haya huku Marekani, na miaka ya karibuni nimeanza kufanya hivyo Tanzania. Masuala haya yanaendelea kufahamika vizuri katika makampuni, mashirika,taasisi, vyuo na jumuia mbali mbali huku Marekani na sehemu zingine za ughaibuni.

Lakini haya si mambo ya ughaibuni tu, na wala pasiwe na mtu akadhani ni mambo ya ughaibuni tu. Ndio maana naendesha warsha Tanzania. Kama kuna asiyeamini hayo, napenda kuleta tangazo la ajira lilitolewa na World Food Program la Umoja wa Mataifa hapa Tanzania, kama lilivyoripotiwa katika blogu ya Michuzi. Bofya hapa.

Kigezo cha ufahamu wa tamaduni tofauti, ufahamu wa namna ya kushughulika na watu wa tamaduni mbali mbali, kimesisitizwa kama sifa mojawapo ambayo mwomba ajira anatakiwa awe nayo. Watu waliohudhuria warsha zangu wanafahamu kuwa hapo ndipo kwenye msisitizo wa warsha zangu. Warsha zangu hazina mbwembwe wala madoido. Ni darasa, kama inavyoonekana hapa, hapa, na hapa.

Nimefurahi kuona tangazo hili la World Food Program, hasa kwa kuwa zimebaki siku chache tu kabla sijasafiri kuelekea Tanzania, ambako nitaendesha tena warsha. Kitu kimoja kinachotajirisha warsha hizi na kuzipa umuhimu wa pekee ni kuwa washiriki wanachangia uzoefu wao katika kuhusiana na watu wa tamaduni mbali mbali, sehemu zao za kazi au katika shughuli zingine. Hapo najifunza mengi, na natambua umuhimu wake. Warsha yangu ya kwanza ni tarehe 12 Juni, mjini Tanga, kama nilivyoeleza hapa.

Kwa taarifa zaidi, wasiliana nami: info@africonexion.com

Comments

Fadhy Mtanga said…
Ndugu Mbele, hakika kubadilishana uzoefu juu ya tamaduni ni nyenzo nzuri sana ya kukuza maelewano baina ya watu hao wa tamaduni tofauti.

Niliwahi kwenda masomoni nchini Zambia. Kule nilikutana na jambo la kushangaza. Wakati Tanzania kujadili Ukimwi imekuwa ni jambo la kawaida, wao bado kwa sehemu kubwa ilikuwa ni taboo. Hivyo usingetegemea kukuta mtu anakwenda dukani kweupe kuulizia mipira ya kiume.

Kutokana na kutofahamu utamaduni wa jamii ya wenzetu ambako ukristo umetawala, rafiki yangu alivaa kanzu. Alipata wakati mgumu sana kwani alitafsirika kama gaidi. Hiyo sehemu tuliyokuwepo utamaduni wao wa kuabudu ulikuwa ungali wa kikiristu na dini zao za jadi.
Mbele said…
Ndugu Mtanga, shukrani kwa mchango wako. Mifano uliyotoa imenigusa sana. Lakini hii uliyoelezea ndio halisi na itazidi kwa jinsi tunavyoendelea kukutana na watu tamaduni mbali mbali, iwe ni katika nchi yetu au nchi za nje.

Naamini wasomaji wa ukurasa huu wataelewa kuwa lengo letu ni kuwapa watu nyenzo ya mafanikio. Nina uhakika na ninayosema, na ndio maana sisiti kusema kuwa ni muhimu.
Fadhy Mtanga said…
Ndugu Mbele kuna mfano mwingine nimeukumbuka wakati nikipitia maoni yako.
Wakati nikiwa darasa la nne, nilikwenda kijijini kwetu Ilembule wilayani Njombe. Kuna ndugu yangu aishiye Denmark alikuwa amerejea likizo akiambatana na mumewe.
Ilikuwa ni nyakati za mchana. Yule shemeji mzungu alikuwa kajipumzisha baada ya shughuli za kuvuna mahindi shambani.
Sisi tulikuwa uwani tukipiga gumzo. Tulikuwa watu kama kumi, wengi ni kina mama watu wazima akiwemo mama wa dadaangu yule na dada mwenyewe. Tunapewa mastori ya Ulaya. Nadhani unaelewa shauku yetu kujua hayo.
Bwana shemeji alipoamka akaja moja kwa moja kuungana nasi. Alipofika pale akamfuata mkewe na kumbusu shavuni. Mtu wa kwanza kuona aibu alikuwa dada mwenyewe, mama yake akainua haraka na kwenda ndani. Wakina mama wengine wale wote walitazama pembeni kwa kujawa soni.
Bwan'shemeji alipoona vile akamwuliza mkewe. Akamwambia huku kwetu si utamaduni kufanya vile. Shem akajisikia aibu na kumwambia "u should have told me!"
Naikumbuka sana sentensi hiyo maana tangia hapo shuleni walinikoma, 'u should have told me ikawa ndo msemo wangu.' Ha ha haaa!

Nilichotaka kusema hapa kwa mfano huu, ni umuhimu wa kufundishana tamaduni zetu katika mahusiano.
Hata humu humu kwetu Tanzania, tamaduni hazifanani. Kwa mfano sisi Wabena, ukioa, bado huwezi kujisikia amani kulala nyumbani kwa wakwezo. Utasalimia na kwenda kulala pahala pengine, aidha nyumba ya wageni ama kwa ndugu mwingine.
Pia ni mwiko kwa mwanamke kumjibu vibaya mumewe mbele za watu. Ugomvi wake ni mkubwa.
Ni tamaduni hizi.
Nalifurahia sana somo lako na ntazidi kuwa mwanafunzi wako.
Ahsante sana.
Mbele said…
Mambo ndio hayo. Sasa tafakari hali itakavyokuwa katika masuala ya uwekezaji, ajira, biashara za kimataifa, diplomasia, mahusiano sehemu za kazi, na kadhalika, katika dunia hii ya utandawazi.

Kwa jadi iliyozagaa Tanzania ya kutothamini elimu wala vitabu, na badala yake kutafuta njia za mkato, ushirikina, na kughushi vyeti, tutaishia wapi?

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini