Saturday, February 17, 2018

Ripoti ya Mhadhara wa Red Wing

Nashukuru nimeweza kwenda leo Red Wing na kutoa mhadhara juu ya "African Storytelling," kama ilivyotangazwa. Barabara zilikuwa na theluji, kwa hivyo ilibidi niendeshe gari kwa uangalifu. Lakini nilifika salama, saa tatu na dakika hamsini. Mhadhara ulipangiwa kuanza saa nne, na ndivyo ilivyokuwa.

Nilipokelewa vizuri na wahudumu wa maktaba ya Red Wing, hasa Lindsey Rindo ambaye ndiye aliyefanya mawasiliano nami tangu mwanzo, mwaka jana, kuniulizia kama ningeweza kwenda kutoa mhadhara, akafuatilia na kufanya mipango yote hadi kufanikisha shughuli ya leo.

Walikuwepo watu wa kila rika, kuanzia watoto wadogo hadi wazee. Nilianza kwa kuelezea umuhimu wa Afrika kama chimbuko la binadamu, tekinolojia, lugha, na usimuliaji wa hadithi. Nilielezea jinsi falsafa na maadili yalivyohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi katika aina za fasihi simulizi kama vile methali. Nilitoa mifano ya methali.

Kisha nilisimulia hadithi ya "Spider and the Calabash of Knowledge," na "The Lion's Advice," kutoka katika kitabu cha West African Folktales cha Jack Berry, na hadithi ya "The Chief's Daughter," kutoka katika kitabu cha West African Folktales cha Steven H. Gale. Hizo hadithi mbili za mwanzo sikuzifahamu hadi jana. Ndipo nilizisoma, nikaamua kwenda kuzisimulia leo. Hiyo ya tatu niliifahamu, na niliwahi kuisimulia.

Dakika kumi za mwisho zilikuwa za masuali na majibu. Kwa tathmini yangu, mhadhara wa leo umekuwa moja wa mihadhara bora ambayo nimewahi kutoa. Nilivutiwa kuona wazazi wamekuja na watoto wao. Inapendeza kuona jinsi watoto wadogo wa Marekani wanavyozoeshwa kutumia muda maktabani.

Lindsey alikuwa ameniambia kuwa nilete vitabu vyangu, nikitaka, kwa ajili ya kuuza, nami nilifanya hivyo. Nilichukua nakala za kutosha za Matengo Folktales na Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Wakati wa kunua na kusainiwa vitabu, niliguswa kumwona mama moja alivyokuwa na ari ya kununua kitabu cha "Africans and Americans." aliniambia kuwa ni mfanya usafi katika maktaba hiyo. Kwa hapa Marekni, ni jambo la kawaida watu wa aina zote kupenda vitabu.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...