Tarehe 9 mwezi huu, nilienda Chuo Kikuu cha Minnesota kutoa mhadhara. Mada niliyoombwa kuongelea ni "Embracing African and African American Culture." Hiyo ilikuwa ni fursa nyingine kwangu kuelezea mtazamo wangu juu ya mahusiano baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika. Nilikuwa na mambo manne ya kuelezea: umuhimu wa mada ya mahusiano baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika, umuhimu wa kutambua utata na matatizo ya uhusiano huo, umuhimu wa kuelewa tulifikaje hapa tulipo, na umuhimu wa kutafakari namna ya kusonga mbele.
Kuhusu umuhimu wa mada, nilisisitiza kwamba watu weusi ulimwenguni wanakabiliana na matatizo ya pekee, tofauti na watu wengine. Nilisema kwamba waasisi wa "Pan-Africanism" walitambua jambo hilo vizuri. Kuhusu kipengele cha pili, nilitoa mifano na kufafanua migogoro na kutoelewana baina ya wa-Marekani Weusi na Wa-Afrika. Kuhusu tulivyofika hapa tulipo, niliongelea historia ya Afrika, tangu mwanzo, ambako tulikuwa jumuia moja, hadi pale watu wa Ulaya, kwa msukumo wa ubepari, walipofika na kuwachukua wa-Afrika kwa mamilioni kuwapeleka utumwani mbali na Afrika na papo hapo, kwa msukumo huo huo wa ubepari, wakavamia bara la Afrika na kulifanya makoloni.
Hapo ndipo wa-Afrika waliopelekwa Marekani wakaanza kuwa na historia tofauti na ile ya wa-Afrika waliobaki Afrika, kwani Marekani kulikuwa na mfumo wa utumwa na ubaguzi wa rangi na ukandamizwaji wa aina ya pekee. Hapo ndipo tofauti kubwa lilijengeka katika pande hizo mbili katika tamaduni, mitazamo, hisia, na mambo mengi mengine. Chimbuko la misuguano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi ni hilo, kwani walipitia njia tofauti. Jukumu lililopo ni kujielimisha. Wa-Afrika wajielimishe kuhusu historia ya wa-Marekani Weusi. Wajielimishe kwa dhati. Wa-Marekani Weusi wajielimishe kuhusu historia ya wa-Afrika. Wajielimishe kwa dhati. Mimi kama mwanafasihi ninafahamu kuwa fasihi ina mchango mkubwa katika elimu hiyo.
Kwa kiasi kikubwa, mhadhara huo ulifuata mwelekeo wa mhadhara niliotoa mwezi Januari katika mkusanyiko wa Nu Skool. Imekuwa ni bahati kupata fursa mbili kuelezea mawazo yangu na kusikiliza na kujadili masuali na maoni mbali mbali.
Showing posts with label wa-Afrika. Show all posts
Showing posts with label wa-Afrika. Show all posts
Thursday, April 12, 2018
Sunday, February 26, 2017
Mpiga Debe Wangu Kutoka Liberia
Nina jadi ya kuwatambulisha wasomaji na wapiga debe maarufu wa vitabu vyangu katika blogu hii. Ninafanya hivyo ili kuwashukuru, nikizingatia kuwa wanachangia mafanikio yangu kwa jinsi wanavyoupokea mchango wangu.Leo ninapenda kumtambulisha Charles Chanda Dennis, raia wa Liberia ambaye anaishi hapa Marekani, jimbo la Minnesota. Huyu ni mtu maarufu, hasa katika jamii ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi. Ni mtangazaji na mwendeshaji wa kipindi kiitwacho African Roots Connection katika KMOJ Radio.
Sikumbuki ni lini nilifahamiana na Charles, lakini nadhani ni miaka karibu kumi iliyopita. Aliwahi kunialika kama mgeni katika kipindi chake tukahojiana juu ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Wiki chache zilizopita, alinialika tena, tukafanya mahojiano marefu na ya kina ambayo unaweza kuyasikiliza hapa:
https://www.dropbox.com/home?preview=Story+Telling.mp3
Miaka yapata mitano iliyopita, Charles alialikwa na wanafunzi hapa chuoni St. Olaf kutoa mhadhara juu ya historia ya mahusiano na harakati za watu wa asili ya Afrika. Nilihudhuria mhadhara ule. Charles alithibitisha kuwa ni msomi wa uhakika, mwenye uwezo mkubwa wa kuchambua mambo. Anafahamu vizuri njia waliyopitia watu weusi barani Afrika na nje ya Afrika, hasa Marekani.
Alivyonialika kwenye mahojiano safari hii, hatukuongelea angenihoji kuhusu nini hasa, bali nilihisi kuwa alitaka kufuatilia masuala ambayo ninashughulika nayo katika jamii, kama mwalimu na mtoa ushauri kuhusu tamaduni. Niliguswa na masuali yake, kama inavyosikika katika ukanda wa mahojiano niliyoweka hapa juu.
Niliguswa kwa namna ya pekee jinsi Charles alivyonitambulisha kwa wasikilizaji, akinipigia debe kwa bidii na kuwahamasisha watu wasome Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Ninamshukuru kwa hilo, nikizingatia umaarufu wa kipindi chake cha African Roots Connection na KMOJ Radio kwa ujumla.
Saturday, February 18, 2017
Mahojiano Radio KMOJ: Charles Dennis na Joseph L. Mbele
Tarehe 4 Februari, 2017, nilikuwa mgeni katika programu ya African Roots Connection ya Radio KMOJ, Minnesota. Mwendesha kipindi Charles Dennis alifanya mahojiano nami juu ya masuala mbali mbali yanayohusu historia na utamaduni wa watu wenye asili ya Afrika. Unaweza kuyasikiliza mahojiano hayo hapa:https://www.dropbox.com/home?preview=Story+Telling.mp3
(mpiga picha Zawadi Mbele)
Sunday, January 8, 2017
Msomaji Wangu Mpya
Jirani yangu mama Merri, mdau na mpiga debe mkubwa wa maandishi na shughuli zangu za uelimishaji, amenitambulisha kwa mwalimu Paul White anayeishi California. Alianza kuniambia habari za mwalimu huyu miezi kadhaa iliyopita, wakati aliponiambia kuwa anataka kumpelekea kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Alinunua, nikasaini, akampelekea.Baada ya hapo, nami nilianza kutafuta taarifa za mwalimu huyu mtandaoni. Niliguswa sana na juhudi na mafanikio yake katika kuwafundisha na kuwapa mwelekeo vijana walioshindikana, waliokata tamaa, wahalifu, na ambao jamii iliwaona hawafundishiki wala hawawezi kuokolewa.
Katika maisha yangu yote, sijawahi kusoma kuhusu mwalimu mwenye mtazamo na moyo kama alio nao mwalimu White. Mfano moja wa taarifa zake zilizonigusa ni mahojiano haya hapa. Nilivyosoma taarifa zake, nilifikiwa na wazo la kuanzisha mpango kama wa kwake nchini mwangu, kuwaokoa vijana waliotemwa na mfumo wa elimu, waliokata tamaa, wahalifu, ambao jamii inaamini wameshindikana.
Hatimaye, kwa kuhimizwa na mama Merri, jana nilimpigia simu mwalimu White. Mke wake aliitika akaniambia kuwa mwalimu alikuwa ameondoka kodogo, nikaacha namba ya simu. Baada ya nusu saa hivi, mwalimu alinipigia simu, tukaongea kwa msisimko wa furaha. Aliniambia kuwa anakifurahia kitabu changu, akanukuu sehemu mbili tatu kusisitiza tofauti baina ya wa-Afrika na Wamarekani.
Ameongea kirefu, akanihimiza niandae mhadhara wa TED, na pia nifikirie kwenda California kutoa mihadhara kuhusu masuala yanayoikabili jamii ya wa-Marekani, kama vile tofauti za tamaduni. Tumefurahi kuwasiliana na tunafurahi zaidi kuwa tutaendelea na mawasiliano. Nimeona nijiwekee hizi kumbukumbu zangu, kwani ni lengo langu moja muhimu katika kublogu.
Sunday, October 23, 2016
Siku ya Mashujaa wa Kenya, Rochester, Minnesota
Nilipata taarifa ya sikukuu hii kutoka kwa Olivia Njogu, m-Kenya aishiye Rochester, na mwanabodi wa Rochester International Association. Anaonekana pichani hapa kushoto, wa pili kutoka kulia. Chama hiki huandaa tamasha la kimataifa kila mwaka, na Olivia tulifahamiana niliposhiriki tamasha hilo mwaka huu, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Baada ya tamasha, Olivia alisoma kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na kisha akaniandikia kunielezea alivyokipenda. Taarifa hiyo niliiandika katika blogu hii.
.Hii haikuwa mara yangu ya kwanza kuhudhuria sherehe za wa-Kenya hapa Marekani. Daima nimependezwa kujumuika nao, kama nilivyowahi kuandika katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Hali ilikuwa hivyo hivyo jana. Nilivyokuwa ninapaki gari kwenye eneo la sherehe, walikuja wa-Kenya kadhaa kunipokea, ingawa hatukuwa tunafahamiana. Tulitambulishana na hima tukazama katika maongezi ya dhati na michapo.
Hii ilikuwa ni sherehe iliyojumuisha watoto vijana na watu wazima. Pamoja na maongezi yasiyo kikomo, vicheko na chereko, kulikuwa na vyakula tele na muziki. Nilivutiwa kwa namna ya pekee na muziki wa Kenya, nikakumbuka safari zangu za Kenya kuanzia mwaka 1989, za utafiti juu ya tungo za zamani na utamaduni wa wa-Swahili.
Picha hapa kushoto ni ushahidi wa hali ya furaha iliyotawala.
Wengi waliohudhurua sherehe ya jana sikuwa nimefahamiana nao kabla, ingawa wachache walinikumbuka kwa kuwa waliniona katika tamasha la kimataifa la Rochester la mwaka huu.
Sherehe hii haikuwa ya wa-Kenya pekee. Ingawa sikuweza kuongea na kila mtu, nilipata fursa ya kuongea na watu wawili wa mataifa mengine: mmoja kutoka Nigeria na mwingine kutoka Uganda.
Katika kuishi kwangu hapa Minnesota, nimeweza kufahamiana na wa-Afrika wengi waishio Minneapolis, St. Paul, na maeneo ya jirani. Sasa ninafurahi kuweza kujenga mtandao wa aina hiyo maeneo ya Rochester.
Wanadiaspora wa Afrika tuna wajibu wa kujenga mshikamano miongoni mwetu, kama msingi wa ushirikiano katika bara letu. Waliotutangulia huku ughaibuni, kama akina Peter Abrahams, Jomo Kenyatta, na Kwame Nkrumah walifanya hivyo. Kwangu kama mwandishi na mwalimu, hizi zote ni fursa za kielimu. Darasa ni popote, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.
Saturday, July 19, 2014
Tunajiandaa kwa Tamasha la Afrifest, Agosti 2
Kila mwaka, tangu mwaka 2007, nahudhuria tamasha la Afrifest, ambalo hufanyika hapa Minnesota, Marekani.
Imewahi kutokea kwamba nilikuwa Tanzania wakati wa tamasha hilo. Binti zangu wananiwakilisha.Wanafahamu vizuri shughuli zangu, na wanawaeleza watu wanaoulizia kuhusu shughuli zangu na vitabu vyangu.
Hizo "ti-sheti" tulizovaa zina nembo ya kikampuni changu kiitwacho Africonexion: Cultural Consultants, ambacho najaribu kukijenga.

Hapa kushoto anaonekana Deta, binti yangu wa kwanza. Siku hiyo sikuwepo.

Hapa kushoto anaonekana Zawadi, binti yangu wa mwisho, akiwa anangojea watu. Hapo ni wakati alipokuwa mdogo. Alianza kuipenda shughuli hii tangu alipokuwa mdogo sana. Alikuwa akifuatana nami kwenye matamasha ya utamaduni, akinisikiliza ninapoongea na watu. Tangu akiwa na umri ule mdogo, aliweza kuwaeleza watu kuhusu shughuli zangu na kuhusu vitabu vyangu. Kwa mfano, katika mji wa Faribault kulikuwa na tamasha la tamaduni, nami nikiwa Tanzania. Zawadi alihudhuria mwenyewe. Alihojiwa na gazeti la Faribault Daily News, akatoa maelezo vizuri kabisa.

Shughuli kama Afrifest ni fursa ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia na tamaduni mbali mbali kukutana. Naamini kuwa kwa watu wazima, vijana, na watoto, hii ni elimu bora kabisa.Hapa kushoto Zawadi anaonekana akiwa na watu wawili kutoka visiwa vya Caribbean.

Hapa kushoto wanaonekana Deta na Zawadi wakihojiwa. Kila mwaka, habari za Afrifest zimekuwa zikitangazwa katika vyombo vya habari vya hapa Minnesota. Mahojiano na waandaaji na washiriki huwa sehemu ya taarifa hizo.
Kwa mtoto au kijana, kuhojiwa namna hii ni kujijengea tabia ya kujiamini na pia uwezo wa kujieleza.
Hapa naonekana nikiwa na mama mmoja aliyekuja kwenye meza yangu. Nilimweleza yale aliyoulizia. Hata hivi, kwa kumwangalia usoni, hakuonekana anavutiwa na yale niliyokuwa nasema. Niligundua hatimaye kuwa dhana yangu haikuwa sahihi, kwani, bila mimi kutegemea, alitoa pochi yake, akalipia vitabu viwili: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales.Baada ya kuchukua hivyo vitabu, akajiondokea zake, kimya kimya. Nilizidi kuamini kuwa huyu mama sio mzungumzaji sana.
Mwaka huu, Afrifest itafanyika North View High School katika mji wa Brooklyn Park, Minnesota, tarehe 2 Agosti. Lakini shughuli za mwanzo zitafanyika siku moja kabla, yaani Agosti 1, kama unavyoona katika tangazo hapa chini. Kwa taarifa zaidi, tembelea www.afrifest.org

Subscribe to:
Posts (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Ukizunguka mitaani Dar es Salaam, utakuta matangazo mengi ya waganga wa kienyeji. Waganga hao wanatoka sehemu mbali mbali, kama vile Sumbaw...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
