Friday, April 15, 2011

Hatimaye, Bia Zitazinduliwa Ikulu

Ni juzi tu hapo niliandika makala kuhusu jinsi wa-Tanzania wanavyowajibika katika unywaji wa ulabu. Makala hiyo ni "Kazi ya Kunywa". Katika kuhitimisha, nilitamka kuwa, kwa mwendo tunaokwenda, huko mbele ya safari ulabu utakuwepo hadi shuleni na Bungeni.

Ni kama vile niliota. Wiki hii wabunge wa Tanzania wameweka historia kwa kuzindua vinywaji vikali huko Dodoma. Soma hapa.

Nchi yetu ni ya pekee. Tunauenzi ulabu kiasi hiki, ingawa unasababisha au kuchangia matatizo mengi, kuanzia ajali barabarani zinazosababisha vifo vingi na watu wengi kuumia, uharibifu wa mali, magomvi katika jamii, kuharibika akili na matatizo ya kisaikolojia.

Tunakwenda kwa kasi na ari kiasi kwamba siku si nyingi kuanzia sasa, bia zitakuwa zinazinduliwa Ikulu. Na siku ya kuzindua bia itakuwa ni ya kukumbukwa ki-Taifa.

Enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere, wabunge wangekuwa wanazindua maktaba, si ulabu. Hakuna mtu aliyethubutu kufanya mambo yanayofanyika leo. Lakini mambo ndio hayo: akiondoka paka, panya hutawala.

6 comments:

Subi said...

Imenisikitisha sana habari ile, tangu jana, siyo siri. Nimewaza na kuachwa na mafikara mengi sana. Afadhali umelikemea hili. Nakuunga mkono Prof. Mbele!

Katu said...

Prof. Mbele....
You have touched very critical issue Tanzania modern society social aspects towards economic and political development.. All those MP's are looking as role modal of majority Tanzanian young stars and Kids today...Sadly what is coming out as lesson to learn from them in our today and future generation!!

This is absolutely terrible and big shame upon mosly so called major driver tool of legislative institutions.

Water hell!

Mbele said...

Jamii yetu imepoteza mwelekeo. Hili suala la ulabu limeshakuwa ni kipaumbele kikubwa sana katika jamii yetu.

Hata mimi ambaye ni mwalimu, wa-Tanzania wananitathmini kwa kigezo cha ulabu, sio elimu niliyo nayo. Wanataka kujua naweza kuagiza bia kiasi gani.

Kama siwezi, wanadharau kabisa na kusema profesa gani huyu hata kununua bia anashindwa. Kwamba nimeandika makala za kitaaluma, si kigezo kinachothaminiwa. Watu wanataka kuona kreti ya bia :-)

SIMON KITURURU said...

MMMmmmmmh!

Anonymous said...

Kama unavojua Profesa kwamba pombe ndio inayotwala ktk nchi yetu.Pombe ndio inayo waongoza viongozi na huwaelezi kitu kwasababu watakwambia viwanda vya pombe ndio vinaingiza pato kubwa ktk serikali.Kutokana na wanywaji ni wengi na kuwapa ajira kupitia biashara ya pombe.Pombe hiyohiyo inayosababisha maradhi ktk mwili wa binaadamu,husababisha kuzorotesha nchi na maafa mengi ikiwepo umasikini.Husababisha ajali nyingi barabarani na pia husababisha kero kubwa kwa jamii kwa ujumla.Mtu anaweza kuamka asubuhi na kuondoka ktk nyumba bila ya kuacha matumizi kwa familia yake akadai hana pesa lakini akirudi nyumbani anakua amelewa tayari.Na kero jingine kubwa ni kuwepo vilabu ktk maeneo ya kuishi watu na utakuta mziki unapigwa kwa kelele usiku kucha mpaka kunakucha sasa hapo kuna kulala kweli na je hivi ndio tutajenga nchi kweli.Kwanini hatuwafuati wenzetu jinsi wanavojitahidi kuwaelimisha jamii zao kwa kuwakumbusha madhara ya pombe na sigara.Kwanza huwezi kukuta club ipo ktk eneo la kuishi watu na kama kuna PUB basi husikii makelele ya mziki au kama kuna mtu anafanya fujo basi analetwa polisi ili aondoshwe haraka ili asiwakere wananchi waliojikalia ktk majumba yao.Sasa viongozi wetu badala ya kuongeza nguvu ya kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya pombe wao ndio wanasheherekea ufunguzi wa pombe,sasa tunawaeleza nini watoto wa taifa la kesho au tunawafundisha nini kupitia ktk maisha ya kila siku yasiyo badilika.

NN Mhango said...

Mie sioni ajabu ya pombe kuzinduliwa ikulu. Kama ufisadi unabarikiwa ikulu ni nini kitawazuia walevi wa pombe na madaraka kuzindulia pombe ikulu? Kwenye safu yangu ya Jicho la Kijiweni nimekuwa, kwa makusudi mazima nikitumia neno walevi badala ya wananchi kutokana na hali hii.
Hivi kuna ulevi kama huu wa kila mwanafamilia ya mtawala kuwa naye mtawala? Hebu waangalie walevi wanavyoshangilia au kunyamazia ulevi huu kwa vile nao wamelewa na maisha.