Thursday, April 21, 2011

Ziara Yangu Shanghai

Mwaka 2003 nilipata bahati ya kutembelea China. Hii ni kati ya ziara ambazo nazikumbuka sana. Nilialikwa kwenda kutoa mihadhara East China Normal University, mjini Shanghai.



Mihadhara ilikuwa kama ifuatavyo:

25 Novemba, "My Folklore Research Experience,"
25 Novemba "American Folklore Studies Today,"
26 Novemba, "My Folklore Research Experience"
1 Desemba, "African Folklore Research."

Picha zinazoonekana hapa ni za wanafunzi wa shahada ya juu. Mwalimu wao, ambaye amevaa jaketi jekundu, alinialika niongee na hao wanafunzi darasani kwao kuhusu "My Folklore Research Experience" na vile vile "Women in African Folklore" hiyo tarehe 26Novemba.

Nilifurahi kupata fursa hii ya kubadilishana mawazo na watafiti wa China. Walikuwa na masuali mengi. Huyu bwana aliyesimama pembeni alikuwa katika ngazi ya juu kuliko hao wanafunzi wengine. Wao walikuwa wanasomea shahada ya uzamili, wakati yeye alikuwa katika shahada ya udaktari. Alivyokuwa na masuali mengi magumu na niliongea naye muda mrefu.

Tarehe 27 Novemba, wenyeji wangu, wakiongozwa na huyu mwalimu mwenye jaketi jekundu, walinitembeza hadi kwenye mji wa Suzhou, ambao ni maarufu kwa historia na utalii. Tulifikia Sheraton Suzhou. Kuna vivutio vingi vya utalii Suzhou, kama vile bustani za kale.

Tarehe I Desemba alifika hapo Chuoni mwandishi wa gazeti la "Oriental Morning Post," akiwa na mpiga picha Zhang Dong, akanifanyia mahojiano ya saa nzima kuhusu utafiti wa Folklore, fasihi, na uhusiano baina ya taaluma hizo. Baada ya mahojiano hayo, walihudhuria mhadhara wangu kuhusu "African Folklore Research." Kisha tukafanya tena mahojiano ya saa nzima na nusu. Mwandishi huyu alikuwa makini kwa masuali na nakumbuka aliniulizia hata kuhusu mwandishi J.M. Coetzee wa Afrika Kusini, ambaye alikuwa amepata tuzo ya Nobel wiki chache tu zilizotangulia, mwanzoni mwa mwezi Oktoba. J.M. Coetzee amehamia Australia.

Fursa ya kutembelea China ilikuwa ni jambo la pekee sana kwangu, kutokana na historia ya urafiki baina ya Tanzania na China. Nami nilianza mihadhara yangu yote kwa kukumbushia urafiki huo, ambao ulianza miaka ya mwanzo baada ya Uhuru wa Tanganyika.

Wakati naandaa safari ya China, nilipewa jina la Mchina ambaye anaifahamu Tanzania na Zambia. Aliyenipa jina hili ni profesa katika Chuo cha St. Olaf ambapo nafundisha. Ni profesa wa lugha na fasihi ya China, ambaye ana uzoefu sana na China. Alinielezea habari za huyu Mchina, kuwa alikuwepo Tanzania miaka ile ya ujenzi wa reli baina ya Tanzania na Zambia.

Nilipelekwa nyumbani kwake mjini Shanghai na tuliongea sana. Alikuwa na vinyago vya ki-Makonde nyumbani mwake, na vitu vingine vya aina hiyo. Ni mtu ambaye anaisifu Tanzania na Zambia kwa mambo mengi. Kwa kifupi, ziara yangu ilikuwa nzuri sana, na nitakumbuka daima ukarimu wa wenyeji wangu.

12 comments:

Simon Kitururu said...

Prof. Jay baada ya kukusoma ngojea niseme tu : ULIPENDEZA kweli yani ! Hiyo kitu ya kijani uliyovaa kama ungekuwa jirani yangu na umeianika kwenye kamba na uko ndani unajisomea bila kuchungulia nje ningeiiba Prof.

Nje kidogo ya posti hii:

Kuna imejensi/ DHARURA fulani huku :

http://malkiory-matiya.blogspot.com/2011/04/nani-ni-mkali-wa-kimombo-kati-ya.html#comment-form

Mie binafsi ningependa kusikia usemacho kuhusu hili!:-(

Simon Kitururu said...

Prof. mbele: Nimegombezwa kwa staili yangu ya kukuandikia hapa na msomaji wako ambaye simtaji jina kwa kudai sina heshima kwa kukuita Prof. Jay hapo kwenye komenti yang ya kwanza!

Samahani kama naonekana sina heshima lakini Prof. wewe ni miongoni mwa niwaheshimuo sana tu na hata ujaji wangu hapa kikubwa ni kwaajili ya kuja kuchota hekima!:-(

Yukiachana na hilo:
Hivi nyumba yako madirisha yana nondo kama Bongo?:-)


Tukirudi CHINA:


Bado nafikiria ulivyovaa ulimbwende huko sehemu sehemu za mbali wakati unawamwagia hekima HATA ambao wengine WAO labda walikuwa fulu matamanio kwako kama MWANAUME katika kukuchekeachekea KWAO ULIKOKUWA UNAKUSTUKI ila weye kihekima hukustukia!:-)

Simon Kitururu said...

DUh! Commenti yako mbona haipo tena?:-)

Mbele said...

Umenivunja mbavu aisee, kwenye ujumbe wako wa hapo mwanzo kabisa. Nitakuwa naianika chumbani :-)

Ila uwongo mbaya, kama unavyoona, hapo niliwakomesha wa-China na hiyo pamba yangu :-)

Mbele said...

Lo, naona unajibu kasi sana. Niliiondoa kidogo ili nenda kuangalia kule kwa Matiya.

Simon Kitururu said...

Prof: Unakumbuka nyumba zetu TANZANIA zilivyo na nondo kuogopa wezi ?

Na samahani niko hapa kijiweni kwako nakusoma posti fulani uliandika mwaka jana na nastukia haraka kweli ukikohoa!:-(

Samahani kuna maarifa fulani uliandika mwaka jana nayapitia tena kwa hiyo niko hapa sasa hivi !:-(

Mbele said...

Hiyo ya Prof Jay mbona naona ni mchapo mzuri tu. Kuna usemi kuwa wa-Arabu wa Pemba hujuana kwa vilemba.

Mhakikishie huyu ndugu yetu aliyekucharura kuwa asiwe na wasi wasi. Wanablogu wengi tunafahamiana vizuri kama hao wa-Arabu wa Pemba :-)

Simon Kitururu said...

Asante kwa Jibu Prof. Nafikiri aliyenikaripia akipitia tena atastukia ulichosema:

Tukiachana na hilo ngojea nimwage hili ambalo napambana nalo hapa sasa hivi likuhusulo Prof:

Katika pitapita zangu kijiweni kwa Prof Mbele :

Kwa bahati mbaya kuna washikaji wakaja kuangalia nini nasoma .

Hii kitu imebakia akilini mwa wengi na kuanzisha mjadala uendeleao:``

Mara kwa mara nakumbuka elimu niliyopata kijijini, kabla ya kuanza shule. Wengi wetu tulipitia njia hiyo. Ni elimu gani hiyo? Tangu utotoni, tulipata maelekezo kutoka kwa wazazi kuhusu mambo mbali mbali, kufuatana na umri, kuanzia namna ya kuvaa hadi namna ya kula kwa adabu na kuwasalimia watu.´´

Profesa Joseph L. Mbele

Friday, November 27, 2009

Mbele said...

Umenikumbusha mbali. Hii makala yangu ya elimu ya kijijini imependwa na na wasomaji, kwa mujibu wa taarifa nilizo nazo. Shabiki mmoja mkubwa wa makala hii ni mwanablogu gwiji Freddy Macha, ambaye ameifagilia kwenye blogu moja mbili hivi.

Ni makala mojawapo iliyomo katika kitabu changu cha CHANGAMOTO.

Kuna dada mmoja m-Kenya hapa Marekani ambaye alikisoma kitabu hiki na kisha akanieleza kuwa hii makala ilimvutia sana.

Kitu kimoja kikubwa katika maisha yangu ni kuwa natambua kuwa elimu haipatikani shuleni tu au vitabuni tu. Wazee vijijini wananielimisha sana. Wavuta mikokoteni wananielimisha sana. Machinga na wavuvi, mama ntilie, baa medi, wote hao napenda kusikiliza mawaidha na mitazamo yao kuhusu masuala ambayo wana uzoefu nayo.

Halafu mimi huwa natembelea dala dala, basi, au bajaji. Humo ni kama uko chuoni. Elimu kwa kwenda mbele.

Nilikulia kijijini nikichunga mbuzi na ng'ombe, kama nilivyoandika kwenye hiyo makala unayoingelea. Hiyo ilikuwa ni elimu mathubuti, ambayo nasikitika kuwa nimeipoteza kwa kung'ang'ana na shule.

Bahati mbaya umri wangu sasa ni mkubwa mno, na miguu haiwezi tena kufukuzana na wale mbuzi wakorofi :-)

Simon Kitururu said...

Prof. Jay: Unajua nilikuwa leo nahangaika na mwaka jana katika maandishi yako . Sasa nikaikumbuka hii atiko na kuichimbua huko mwaka juzi ! Bahati mbaya siko peke yangu hapa na wakati naipitia imaedaka watu na tunaangaika nayo bado ingawa mie mkimya hapa nasikilizia tu watu wanavyotokanayo Baruti!:-(
Labda nitakusimulia baadaye au sikunyingine ni nini katika kucheza na hoja zako nukta ilikuwa kulia au kushoto ! Ila kwa ufupi inahangaishana na watu halafu sasa hivi nimetoa mvinyo kwa hiyo nahisi baada ya muda kuna Profesa atatokea katika hikihiki ulichoandika 2009.

Pamoja sana Prof. Mbele -na nahisi ungekuwa unapata moja MOTO moja BARIDI ningekupa mkopo baa sasa hivi pale Magomeni!:-)

Ila wewe unatukemea kweli sie wapenda kilaji mpaka najitahidi kuacha!

Pasaka njema Mkuu na najua kuwa Mkatoliki kwa hiyo sikukaribishi mishikaki!:-)

Fadhy Mtanga said...

ha ha ha haaaaaa nimeanza kwa kucheka baada ya kuzisoma komenti zenu.

Lakini nakiri kuwa Prof Mbele na Simon Kitururu ni mmoja wa wanablog ambao kila siku hupita vijiweni mwao na kusoma mambo mengi. Huwa nachota maarifa mengi sana.

Unknown said...

Ni kweli kabisa Fadhy, hata mimi ni miongoni mwa wafuasi wa Profesa japo huwa napita sana kimya kimya bila kuacha unyayo.

Na yumkini nami nikawa Profesa kutokana na Mbele mwenyewe ninavyomfuatilia, japo machapisho ya Simon Nayo DAH.

Kwa ajili hiyo, ninawajulisha wavuti hii hapa mkibpata muda itembelee:http://www.swahilitruth.com/

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...