Tuesday, April 19, 2011

Mawaidha ya Mwakilishi Keith Ellison

Leo hapa Chuoni St. Olaf tulitembelewa na mgeni maarufu, Keith Ellison, ambaye ni mwakilishi kutoka Minnesota katika Congress, ambalo ni bunge la Marekani. Keith Ellison ni mu-Islam wa kwanza kuwa mjumbe katika Congress.

Aliongelea changamoto zinazoikabili Marekani na dunia katika mkabala wa kuwepo kwa tofauti za dini.

Kwa kutumia mifano ya Marekani, alisisitiza kuwa watu wa dini mbali mbali tuna uchaguzi wa kufanya. Tunaweza kuchagua kuheshimiana, kuelewana na kujenga dunia ya amani, upendo na mshikamano, au tunaweza kuchagua kuwa na uhasama, ubaguzi, chuki, mfarakano, na migogoro.

Alisema kuwa wahubiri wa dini wana wadhifa mzito. Wanapopanda kwenye mimbari au sehemu nyingine ya kuhubiria, wana ushawishi mkubwa mioyoni mwa waumini. Wana wajibu wa kujua hilo, kwani wanao uwezo wa kujenga umoja na maelewano katika jamii au wanaweza kujenga uhasama na chuki katika jamii.

Alisisitiza wajibu wetu wa kuwaheshimu watu wa dini mbali mbali, na watu wasio na dini. Wote wanastahili heshima, na wala hakuna mwenye haki ya kumshinikiza mwenzake kwenye masuala ya imani za dini.

Hotuba yake iliwagusa sana watu. Kitu kimoja kilichonivutia zaidi ni hoja yake kuwa mtu ukifanya juhudi ya kuifahamu dini kwa kusoma na kutafakari, utagundua kuwa inakupeleka kwenye mtazamo wa maelewano, upendo, kuwaheshimu wanadamu wengine, wawe wana dini au hawana dini.

Aliyoongelea yanatugusa sote. Nilitamani angekuja Tanzania kutoa mawaidha hayo. Hotuba yake HII HAPA.

6 comments:

Anonymous said...

Profesa,tatizo kubwa la kuhusiana na chuki za kidini linakuja kupitia MEDIA.Tukiangalia zaidi ktk nchi za west na hasa hapo USA uisilamu umekuwa ktk target ili kuwajengea chuki wananchi wao na waisilamu ili wapate sapoti kubwa ktk kila vita wanazozianzisha.Ukiangalia kwa makini hizi vita zote zimeelekea ktk nchi za ki-isilamu kwa kudai wanapigana na Terorist kitu ambacho hakiingii akilini.Na pia vita hizi hazijaanza leo ni tokea karne nyingi zilizopita au angalia historia ya ukweli kuhusu "Roman empare"walivoingia Palestine.Na kuna baadhi ya viongozi wa kidini wanatumiliwa kueneza chuki kama kuchoma Quran na kutangaza uongo kuhusu uisilamu.Lakini kitu ninacho wapendea hawa watu wa west kwa wale waliosoma wanajitahidi kutowaunga mkono serikali zao na sera za vita kutokana na kuujua ukweli upo wapi.Na kila siku watu wanajifunza mengi kutokana na makosa wanayo yafanya ktk hizi sera zao za uongo na hawato shinda.

Anonymous said...

Profesa..hizi serikali za west zinendeshwa na kundi la matajiri ambao wanafaidika ktk uuzaji wa silaha na hawana dini kwa ufupi Mtu anae amini mungu kupitia dini yeyote ile basi hawezi kutafuta njia ya kuua mamilioni ya watu.Hawa watu kumbukeni wameuwa mamilioni na kuchukua nchi za watu kama USA sio ya kwao waliwateketeza wananchi wa hapo ambao walikuwa ni red indians na wanaangalika kama wa mexico kidogo.Ni pamoja na Canada vilele kama ilivyo Australia na Palestina.South africa iliponea chupuchupu kutokana kwamba miaka ilikua imepita na waafrica wengi walikuwa wameshaelimika na kusaidiana.Hivyo watu ni muhimu kusoma historia za ukweli na kujua hasa adui wako ni nani.Lakini profesa hawa watu wanatumia udini ambao wanajua kama ni inanguvu zaidi kuliko kitu kingine.Na kila nchi inapoanzisha mfarakano wa dini basi wao hufurahia kwa kuingia kiurahisi na kujifanya wao ni wazuri kuja kusaidia watu.Profesa wewe unaiona hali iliyoko hapo ulipo ilivyokuwa ngumu na USA watu wengi hawana kazi na wanahitaji kusaidia,na idadi ya homeless imeongezeka kwa kiasi kikubwa na wanashindwa kuwasaidia.Lakini hushangai ikiwa majanga yakitokea wao wakwanza kupeleka misaada yenye thamani kubwa wakati uchumi kwao umeanguka na je inaleta maana gani.Ni wao ndio wenye kuchafua dunia na kujenga chuki kwa watu wenye kupenda kukaa kwa amani.Wamechafua hali ya hewa na njaa umasikini uliokithiri.Je ukristo kweli ndio unavyotaka maana hutumia kwa kujiita wakristo,sasa waumini wanayakubali haya?

Mbele said...

Shukrani kwa maoni na mawaidha hayo hapa juu. Ni muhimu. Kauli ya kwamba watu wakiwa na juhudi ya kujisomea, wanajikinga na propaganda hizo ni kauli murua.

Tatizo ni sisi Tanzania, kwani watu hawana utamaduni wa kusoma vitabu. Hilo ninalilalamikia mara kwa mara katika blogu hii na blogu za wengine. Nimeandika hata kitabu ambamo pamoja na masuala mengine, nimeongelea pia suala hili. Kitabu kinaitwa CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Kwa kifupi ni kuwa, kwa kumwendekeza adui ujinga, jamii yetu tunaipeleka katika maangamizi, kwa makusudi.

Anonymous said...

Hapa kwetu TZ ni rahisi sana kuweka amani kwasababu hii nchi haina historia mbaya hata kidogo.Ni serikali ndiyo inatakiwa kutatua matatizo na kuyaweka sawa ili kusiwe na ulalamishi.Hii nchi imejitangaza kama haina udini lakini ukiangalia vizuri inayo makosa ambayo inabidi waweke sawa.Kwa mfano wakristo wamepew fursa ya kujiunga na Vatican lakini waisilamu wameomba kwa muda mrefu wapewe fursa ya kujiunga na OIC lakini inapingwa na bila ya sababu yeyote na hasa ukizingatia Zanzibar kabla ya muungano ilikuwepo lakini Nyerere aliutoa sasa Profesa huoni hapa watasababisha matatizo.Maisha kila tunavokwenda mbele yanabadilika na kila mtu anahisi anaonewa na ndiyo kitu kitakachokuja kuchafua maelewano na ni sababu ya viongozi kuweka mambo sawa.Angalia suala la KATIBA linavokwenda tunaona kwamba sivo inavotakiwa.Na vilevile viongozi wa dini wakishirikiana badala ya kujiwekea tofauti zao then warekebishe mambo bila ya upendeleo basi TZ itakuwa shwari na itabakia shughuli ya kuwatoa mafisadi tu.

Mbele said...

Shukrani kwa maoni yako mdau unayegusia wajibu wa serikali na masuala kama Vatican na OIC.

Nakubaliana nawe kabisa kuwa serikali yetu inapaswa ifanye kazi zaidi ya kufuatilia mapungufu yaliyomo katika mfumo wetu.

Mimi ninafanya juhudi sana ya kusoma yale yanayosemwa kuhusu mapungufu hayo. Na ninataka wote tufanye juhudi hiyo. Kwa mfano, Hamza Njozi alipochapisha kitabu chake, kikapigwa marufuku, nilikitetea sana. Na Hamza Njozi mwenyewe, katika kitabu chake kilichofuata, alinishukuru kwa hilo.

Ninajitahidi kujielimisha. Ninaafiki hoja kuwa kuna mambo kadhaa ambayo wa-Islam wana haki ya kuyahoji na kuyalalamikia. Ninafuatilia hoja zao.

Kwa mfano, nimeona kwenye andiko moja la mu-Islam msomi akielezea jinsi miaka iliyopita serikali ilivyokataa kuwaruhusu wa-Islam kuanzisha seminari zao, wakati wa-Kristu hatukukataliwa kuendesha seminari. Mimi mwenyewe ni m-Katoliki na nilisomea seminari.

Mimi ni muumini wa dini yangu, ambayo inatutaka tuwe wakweli na watu wa haki, tunaowatendea wengine kama tunavyopenda kutendewa, hainiingii akilini kwa nini miaka ile serikali ilikataa kuwaruhusu wa-Islam kuwa na seminari zao. Sijui kama serikali imebadili msimamo wake au la.

Hata hivi, kuna madai na malalamiko mengine ambayo bado siyaafiki au bado sijayaelewa. Mimi sio mtu wa kuziba masikio au akili. Huenda iko siku nitayaelewa na kuyaafiki.

Kwa mfano, hilo la OIC na Vatican sina ufahamu wa kutosha wa kulijadili.

Ni suala ambalo nadhani linahusu sheria na taratibu za kimataifa za kidiplomasia. Masomo hayo mimi sina ufahamu nayo. Kwa hivi, nawajibika kuwangojea waliosomea wanieleweshe.

Kinachonitia wasi wasi ni kuwa kuna wa-Tanzania ambao hawaogopi kuyarukia masuala ambayo hawana ufahamu nayo na kutoa mihadhara.

Mimi ingawa ni profesa, kuna mengi ambayo sikusomea na huwa sitoi mihadhara kwa mambo nisiyoyajua vizuri. Uprofesa wangu ni kwenye masomo ya fasihi na ki-Ingereza, sio hayo ya sheria na diplomasia za kimataifa, ambako ndiko kuna haya mambo ya Vatican na OIC.

Kinachonitisha ni kuwa kuhusu masuala ya Vatican na OIC, wa-Tanzania wengi wanasikiliza hotuba za masheikh au wachungaji ambao hawajasomea sheria zinazohusika. Wanasikiliza malumbano ya jazba yasiyo na msingi wa elimu husika. Hili ni tatizo kubwa.

Anonymous said...

mbele nimekuvulia kofia.

Profesa, yalipotokea machafuko kenya baada ya uchaguzi, tuliwacheka kwa ukabila wao.

Nao walitusifu kwa hatua kubwa ya kupinga ukabila lakini wakatucheka kwa kupinga udini mdomoni huku uhalisia udini upo ukiota mizizi na kulindwa kwa kutokuwa na sheria ya ubaguzi na kukemea malalamiko.

hilo unasemaje?