Saturday, March 2, 2013

Kimahama Literature Centre, Arusha

Kati ya maduka ya vitabu yaliyoko Tanzania, kuna moja mjini Arusha liitwalo Kimahama Literature Centre. Sikumbuki ni lini nilianza kusikia jina la duka hili, ila nakumbuka kuwa miaka zaidi ya kumi iliyopita, uongozi wa duka hili ulinunua kutoka kwangu nakala za kitabu changu cha Matengo Folktales. Kama nakumbuka vizuri, walinunua nakala 20. Baadaye nilipata taarifa kuwa zote zimeuzwa.









Siku nyingine, miaka michache iliyopita, nilijikuta tena ndani ya Kimahama Literature Centre kama ilivyo kawaida yangu, kutembelea maduka ya vitabu. Meneja alikuwa mpya. Katika maongezi, nilipomwambia kuwa nimechapisha kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, alinunua nakala kadhaa kutoka kwangu.

Mwaka huu, niliona kitabu hiki kinauzwa hapo, nikapiga picha hiyo hapa kushoto. Kuwepo kwa kitabu hiki katika duka hili kuliwahi kuelezwa na mwanablogu Bwaya katika blogu yake.

Hizi ndizo baadhi ya kumbukumbu zangu za duka hili. Kitu kimojawapo kilichonigusa ni kuona wahusika wa duka la vitabu wakiwa ni wapenda vitabu. Ni muhimu sana kwa wauza vitabu kuwa wapenda vitabu. Vinginevyo ni kujidanganya. Nimegusia suala hili katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, kurasa 30-32.

Duka la Kimahama Literature Centre liko katika jengo hili linaloonekana pichani, ambalo linatazamana na hoteli ya Golden Rose. Ni usawa wa chini kabisa wa hilo jengo, hapa yalipopaki magari.

2 comments:

Goodman Manyanya Phiri said...

Kimahama oyeeee! Na asiyewahi kusikia utamu wa kusoma kitabu labda hastahili kuishi duniani ya leo. Ni lazima tujifunze kupenda vitabu. (Na asante kwa stori ya Kimahama, Prof!)

Joseph said...

Asante Mkuu. Najaribu kueneza taarifa kama hii ili kujaribu kuwahamasisha watu wawe na tabia ya kuingia katika maduka ya vitabu.

Sio lazima kila unapoingia humo ununue vitabu. Nilipokuwa sekondari, seminari kule kwetu Ruvuma, mapadri waliokuwa wanatufundisha walitueleza umuhimu wa kuchunguliachungulia maktaba au duka la vitabu, kwa mtindo wa "browsing."

Sio lazima ukisome kitabu chote, bali unaweza kupitia pitia tu. Na si lazima ununue, kama huna uwezo. Lakini elimu fulani utaipata kwa "browsing."

Maisha yangu yote, kuanzia nilipokuwa sekondari, nimekuwa hodari sana wa "browsing." Ninafahamu mambo mengi sana kutokana na tabia hiyo. Mimi mwenyewe nina vitabu vingi sana, zaidi ya elfu tatu, lakini vingi sijavisoma na katika maisha yangu, sitaweza kuvisoma.

Lakini ukiniuliza kuhusu suala fulani, naweza kukueleza ukasome vitabu vipi, kwani "browsing" imenipa ufahamu huo vizuri kabisa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...