Tuesday, March 26, 2013

Ufundishaji Wangu wa Maandishi ya Achebe

Nimefundisha maandishi ya Chinua Achebe kuanzia miaka ya sabini na kitu. Kabla sijahitimu na shahada ya kwanza Chuo Kikuu Dar es Salaam, mwaka 1976, huenda nilifundisha Things Fall Apart katika shule za sekondari nilikopelekwa kufanya mazoezi ya kufundisha, yaani sekondari ya wasichana Iringa, 1974, na sekondari ya Kinondoni, 1975. Sina hakika.

Lakini baada ya kuhitimu shahada ya kwanza, mwaka 1976, nilipata fursa za kufundisha Things Fall Apart, nikianzia na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo nilikuwa mhadhiri. Mwaka 1980, chini ya mkataba wa ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi, nilifundisha kwa wiki kadhaa katika Chuo Kikuu cha Burundi. Kitabu kimojawapo kilikuwa Things Fall Apart

Uzoefu huu ulinifanya niandike mwongozo wa Things Fall Apart, ili kuelezea mambo ambayo waandishi wengine hawajayaweka wazi.  Ilikuwa ni fursa kwangu kuwaelezea wanafunzi na walimwengu namna ninavyoichukulia riwaya hii ya Things Fall Apart. Kwa maelezo zaidi ya historia hii, soma hapa. Sihitaji kuficha ukweli kwamba mwongozo huu ni maarufu na wengi wanautumia.

Baada ya kuja kufundisha chuo cha St. Olaf, mwaka 1991, nimefundisha Things Fall Apart na maandishi mengine ya Achebe. Kuna muhula fulani nilitunga kozi nzima juu ya maandishi ya Achebe tu. Tulisoma riwaya zake kadhaa, na pia insha baadhi ya insha zake, zikiwemo "The Novelist at Teacher," "Colonialist Criticism," na "An Image of Africa." Tulisikiliza pia baadhi ya mahojiano yake. Ingekuwa muda unaruhusu, tungesoma pia mashairi yake.

Ni wazi kwamba Things Fall Apart ni moja ya riwaya ambazo nimezifundisha sana. Kila ninapoifundisha, nazua masuala mapya na tafakari mpya. Hiyo ni tabia ya fasihi. Hata misahafu ina tabia hiyo, ingawa wako watu wanaodai kuwa misahafu haibadiliki. Binafsi, kutokana na uzoefu wangu wa kusoma na kutafakari fasihi na maandishi mengine, siamini kwamba kuna andiko lolote, hata msahafu, ambalo haliguswi na mabadiliko, kuanzia na mabadiliko ya lugha na maana zake, ambayo hayakwepeki. Nimegusia suala hilo katika mwongozo wangu.

2 comments:

emu-three said...

Profesa tunashukuru kwa `mwongozo huo'. Huyu mkongwe,kwangu nasema amekufa tu kiwiliwili..lkn tupo naye wakati wote, ukitaka kuongea naye, nenda kasome vitabu vyake.
Wanasema `mwandishi wa vitabu hafi, akifa,...hufa kiwiwili tu'...au nimekosea profesa?

Mbele said...

Ndugu emu-three

Shukrani kwa ujumbe wako, na samahani kuwa nilighilibika nikawa sijapata fursa ya kuujibu hadi leo, baada ya miaka zaidi ya mitatu.

Ni kweli, kwamba waandishi maarufu huwa hawatoweki hata kama wamefariki. Akina William Shakespeare, Leo Tolstoy, Charles Dickens, Muyaka bin Haji, na kadhalika, watakuwepo daima.

Kuhusu huu mwongozo wangu, jana niliandika katika blogu hii ujumbe kutoka kwa mhadhiri wa chuo kikuu fulani cha Algeria, katika somo la fasihi ya Afrika, ambaye anafurahia mwongozo huo.