Wednesday, November 22, 2017

Tamasha la Waandishi Minneapolis Lilifana

Tarehe 18 Novemba, tamasha la waandishi, Minnesota Black Authors Expo, lilifanyika mjini Minneapolis, jimboni Minnesota. Walishiriki waandishi 40 wa vitabu, nami nikiwemo. Waandaaji wa tamasha, De'Vonne Pittman na Jasmine Boudah walifanya kazi kubwa kwa miezi minne hadi kufanikisha tamasha hili la aina yake.

Picha hiyo hapa kushoto ni ya jalada la kijitabu walichoandaa chenye taarifa za tamasha, zikiwemo taarifa za waandishi na vitabu vyao. Nimehudhuria matamasha mengi ya vitabu, lakini hii ilikuwa ni mara ya kwanza kuona kimeandaliwa kijitabu cha aina hiyo. Ni jambo zuri sana, kwani mtu unakuwa na fursa ya kufuatilia taarifa ambazo hungeweza kuzipata kikamilifu katika tamasha, kwa sababu ya uwingi wa waandishi.




Hapa pichani anaonekana De'Vonne Pittman akiongea, na pembeni yake anaonekana Jasmine Boudah. Walitugusa kwa uchangamfu na ukarimu wao kipindi chote cha maandalizi ya tamasha na wakati wote wa tamasha ambalo lilidumu kuanzia saa tano asubuhi hadi saa kumi na moja jioni.









Jasmine Boudah naye anaongea.
















Waandishi tulikuwa tumeombwa kuwa tayari ukumbini kabla ya saa nne na nusu. Nilipofika, yapata saa nne na dakika kumi, nilikuta wengi wako tayari.











Wadau nao walianza kuja. Anwani ya ukumbi lilipofanyika tamasha ni 1007 Broadway Avenue West, ambayo ni eneo la kaskazini katika mji wa Minneapolis. Ni eneo linalokaliwa na wa-Marekani Weusi wengi.



Ukisikiliza propaganda za Marekani, utaamini kwamba wa-Marekani Weusi si watu makini katika mambo ya kutafuta elimu. Lakini ukweli ambao hausemwi sana ni kuwa kuna uhaba wa fursa kutokana na mfumo wa kihistoria wa kibaguzi.

Nilivyoshuhuda katika tamasha hili jinsi hao wa-Marekani Weusi wa kila rika, wanaume na wanawake, walivyokuja kwa wingi na ari ya kupata taarifa juu ya vitabu, kuongea na waandishi, na kununua vitabu, nilijiridhisha kuwa propaganda ni tofauti na hali halisi.

Hapa kushoto ninaonekana kwenye meza yangu. Nilipata fursa ya kuongea kwa kina na watu mbali mbali kuhusu vitabu na kazi zangu.

















Hapa kushoto niko na De'Vonna Pittman, mwandaaji wa tamasha. Alikuwa amefika kwenye meza yangu akaniambia kuwa anataka kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kauli yake ilinipa hisia kuwa alikuwa amenuia tangu kabla kujipatia kitabu hicho.













Huyu mama ni mmoja kati ya wale ambao tuliongea sana. Alitaka kujua kuhusu vitabu vyangu vyote, kisha akanunua hiki alichoshika, Matengo Folktales. Bahati mbaya sikuandika kumbukumbu ya jina lake.














Ingawa nilikuwa kwenye meza yangu karibu muda wote, sawa na waandishi wengine, nilipata pia fursa ya kufahaminana na baadhi ya waandishi. Hapa kushoto, ninaonekana nikiwa na Cavis Adams, ambaye ameshika nakala ya riwaya yake ya kwanza, ambayo aliileta kwenye tamasha, na mimi nimeshika vitabu vyangu.












Hapa kushoto ninaonekana nikiongea na Penny Jones, ambaye meza yake ilikuwa pembeni ya meza yangu, zikiwa zimegusana. Shughuli yake ni kuwapa watu ushauri na elimu juu ya kujiamini katika kukabiliana na masuala ya maisha. Tuliongea sana, tukaona jinsi mawazo yetu yanavyofanana au kukaribiana, kwani sote tunashughulika na masuala ya saikolojia. Nilinunua kitabu chake, Thirty Days of Motivation, A guide to Reaching Your Goals and Staying Focused, naye akanunua kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nitategemea tutaendelea kuwasiliana.









Hapa kushoto ninaonekana na Rita Apaloo, mwenye asili ya Liberia, mwandishi wa kitabu nilichoshika, African Women Connect. Huyu ni mmoja wa wadau na wapiga debe wa vitabu vyangu, hasa Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.
 Binti yangu Zawadi amekuwa akiandamana nami kwenye matamasha na mihadhara yangu tangu alipokuwa mdogo. Anafahamu shughuli zangu, na anaweza kuwaelezea watu hata akiwa peke yake kwenye tamasha.















Hapa kushoto tuko na dada ambaye binti yangu Zawadi alimwona katika umati akamleta kwenye meza yangu kututambulisha. Kumbe anafahamiana na Assumpta, dada mkubwa wa Zawadi. Ni maarufu katika kuandaa shughuli na matukio ya kuwakutanisha watu.

Taarifa yangu ni kielelezo na kumbukumbu ndogo tu ya tamasha ambalo lilifana sana. Waandaaji wanastahili shukrani tele. Wameshatangaza kuwa wanajipanga kuandaa tamasha la mwaka ujao. Nawatakia kila la heri.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...