Sunday, February 1, 2015

Uandishi ni Kazi ya Upweke

Waandishi kadhaa maarufu wametamka kuwa uandishi ni kazi ya upweke. Mmoja wa waandishi hao ni Ernest Hemingway, ambaye picha yake inaonekana hapa kushoto.

Katika hotuba yake ya kupokea tuzo ya Nobel, alisema:

Writing, at its best, is a lonely life. Organizations for writers palliate the writer's loneliness but I doubt if they improve his writing. He grows in public stature as he sheds his loneliness and often his work deteriorates.

Najaribu kuitafsiri kauli hii:

Uandishi, katika hali yake bora kabisa, ni maisha ya upweke. Vyama vya waandishi hupunguza upweke wa mwandishi lakini sidhani kama vinaboresha uandishi wake. Hadhi yake katika jamii hukua kwa kadiri anavyoupunguza upweke wake na aghalabu ubora wa kazi yake hudorora.

Hemingway alilitafakari na kuliongelea sana suala la uandishi. Alifanya hivyo katika riwaya, insha na barua zake na pia katika mahojiano na maongezi mengine. Nami ninajifunza mengi kutoka kwake.

Katika makala yangu ya juzi nilitamka kwamba ninapoandika katika blogu yangu hii, ninajiandikia mwenyewe. Sijui na sijali kama kuna atakayesoma ninachoandika. Lengo langu la msingi ni kutimiza haja yangu ya kuutua mzigo uliokuwepo mawazoni mwangu.

Ni wazi kuwa fikra yangu hii inahusiana na yale ninayojifunza kutoka kwa Hemingway. Siko tayari kusukumwa na imani kwamba ninaiandikia jamii. Ningependa kuzingatia kauli ya Hemingway kwamba, "Writing, at its best, is a lonely life."

2 comments:

emu-three said...

''Lengo langu la msingi ni kutimiza haja yangu ya kuutua mzigo uliokuwepo mawazoni mwangu.''

Nimeipenda hii ..mkuu tupo pamoja

Mbele said...

Ndugu emu-three, shukrani kwa ujumbe wako.

Naamini kuwa mtu ukiamini kuwa unawaandikia wasomaji maana yake ni kuwa umeitenga nafsi yako na kile unachoandika. Hujielezi kwa uhalisi na ukweli ("truth," kwa mujibu wa Hemingway).

Kwa maneno mengine uandishi wako unakosa kile ambacho kwa ki-Ingereza tunaweza kukiita "authenticity." Ni tatizo ambalo kifalsafa, hujulikana kama "alienation" kwa ki-Ingereza.

Yeyote ambaye anatafiti au kusomea nadharia ya fasihi anapaswa kulitafakari jambo hilo, na kama anaweza, atuletee fikra tofauti.