Tuesday, February 24, 2015

Ziara Yangu Mankato Imeenda Vizuri


Ziara yangu Mankato, kutoa mihadhara katika
Chuo cha South Central, imekuwa njema kabisa. Shughuli yangu ya kwanza ilikuwa ni kukukutana na wanafunzi wa Mwalimu Fjelland Davis, kama inavyoonekana pichani hapa kushoto. Wanafunzi hao walikuwa wamesoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kwa sababu hiyo, sikutaka kutoa mhadhara, bali nilitoa maelezo mafupi juu yangu na shughuli zangu za uelimishaji wa jamii, kisha nikatoa fursa ya masuali. Tulitumia zaidi ya saa nzima kwa masuali na majibu.
Baada ya hapo, nilipelekwa katika ukumbi mkubwa uliojaa watu, nikatoa mhadhara kuhusu "Writing About Americans."  Katika picha hapo kushoto ambayo nimeitoa kutoka ukurasa wa Facebook wa Chuo Cha South Central ninaonekana nikitoa mhadhara huo.
Hapa kushoto ni picha nyingine ya mhadhara wa "Writing About Americans," ambayo nimeitoa kutoka ukurasa wa Facebook wa Mwalimu Davis.

Baada ya kumaliza mhadhara huu, katika ukumbi uliojaa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Mwalimu Davis alitangaza kuwa vitabu vyangu viko katika duka la vitabu hapa chuoni, na kwamba nilikuwa tayari kusaini vitabu hivyo. Ndivyo ilvyokuwa. Watu walikimbilia dukani, wakanilietea nakala niwasainie.  Pichani hapa kushoto ninaonekana nimesimama na dada mmoja kutoka Peru, akiwa ameshika nakala yake niliyomsainia.

Katika kuandaa na kutoa mhadhara wa "Writing About Americans," na kwa jinsi watu walivyoufurahia, nimepata motisha ya kuandika kijitabu kuhusu mada hiyo.

Alasiri hii, niliporejea hapa kazini kwangu,  mjini Northfield, nimeanza kuona taarifa katika mtandao wa Facebook, kuhusu ziara yangu. Watu wamefurahia maongezi yangu, na wamemshukuru Mwalimu Becky Fjelland Davis kwa kunialika.

2 comments:

Mr Mfuko said...

Hongera kwa ziara kazi hiyo Mzee Mbele, nafurahi kukufahamisha nimetimiza lengo langu lililotokana na muamsho wako .Nimeweza kukipata hatimye kukisoma kitabu cha Bw Leo.B Helzel A GOAL IS A DREAM WITH A DEADLINE. Nimefurahi sana kwani kitabu hiki na kile chako cha Africans and Americans Embracing cultural Differences vitakua ni kumbukumbu yangu kwako siku zote,Asante na kila la heri Mzee Mbele.

Mbele said...

Ndugu Mfuko, hizi ni habari njema, nami nakupongeza na kukuhimiza uendelee katika njia hiyo hiyo. Elimu haina mwisho.