Thursday, February 12, 2015

Kitabu Kimetimiza Miaka Kumi

Kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kimetimiza miaka kumi tangu nilipokichapisha, tarehe 5 Februari, mwaka 2005. Siku hiyo niliuingiza muswada katika mtandao wa lulu nikalipia namba ya utambulisho wa kitabu, yaani ISBN. Siku hiyo hiyo niliagiza nakala ya kwanza, nikaipata baada ya wiki moja hivi. Wiki hii ni kumbukumbu ya miaka kumi ya kuwepo kwa kitabu hiki.

Mambo mengi yametokea katika miaka hii kumi kuhusiana na kitabu hiki. Nimepata fursa ya kusikia maoni ya wasomaji wengi. Baadhi wameandika maoni hayo na kuyachapisha, kama vile katika tovuti, blogu, na majarida. Wengine wameniandikia maoni yao katika barua pepe. Wengine wamenieleza maoni yao katika maongezi ya ana kwa ana.

Watu waliotoa maoni yao kuhusu kitabu hiki ni wa aina mbali mbali. Baadhi nawakumbuka vizuri, kama vile Mhashamu Askofu Owdenburg Mdegella wa dayosisi ya Iringa ya Kanisa la Kiluteri Tanzania, ambaye alisema kuwa kitabu kimemfurahisha sana na anataka wageni wakisome ili watuelewe wa-Tanzania. Aliniambia hayo siku tulipokutana kwenye chuo cha Peace House, Arusha, na alikuwa anaongea kutokana na uzoefu wake mkubwa wa kuwapokea na kushughulika na wa-Marekani wanaokuja Tanzania katika mpango wa ushirikiano baina ya waumini wa-Marekani na wa-Tanzania uitwao Bega kwa Bega.

Mwingine ninayemkumbuka vizuri ni Balozi Mstaafu Andrew Daraja. Alikisoma kitabu hiki wakati akiwa balozi wa Tanzania hapa Marekani, na alinipigia simu akaniambia jinsi alivyokipenda kitabu hiki kama nyenzo ya kuweka maelewano baina wa wa-Marekani na sisi wa-Afrika.

Mzee Patrick Hemingway, katika maongezi naye, amekuwa akikisifia kitabu hiki. Siku tulipomtembelea, alisema kuwa kitabu hiki ni "tool of survival." Mzee huyu m-Marekani anajua anachokisema, kwani aliishi Tanganyika (baadaye Tanzania) kwa miaka yapata 25. Ninaguswa na maoni ya watu kama yeye, ambao wanajua hali halisi ya tofauti baina ya utamaduni wao na wetu.

Katika miaka hii kumi, nimepata mialiko kadha wa kadha kutoka kwenye vyuo, taasisi, makampuni, na vikundi, kwenda kutoa mihadhara kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake. Ingawa kitabu hiki ni kifupi tu kilichoandikwa kwa lugha rahisi, wala si cha kitaaluma, kimenisaidia kuendesha mihadhara hiyo na pia warsha, na hata kutatua migogoro ya kutoelewana baina ya wa-Marekani na wahamiaji na wakimbizi kutoka Afrika.

Ninawashukuru kwa namna ya pekee watu waliochangia kwa namna moja au nyingine kwa kukisoma kitabu, kuwaelezea wengine, na kunipa maoni yao. Wiki hii nitawakumbuka kwa namna ya pekee.

Mambo ni mengi sana yaliyotokea katika miaka hii kumi, ambayo ningeweza kuyaandikia kitabu. Panapo majaliwa, nitafanya hivyo.

No comments: