Nilipokuwa Tanzania mwaka huu, nilikutana na rafiki yangu, mwandishi Edwin Semzaba, kama nilivyoandika hapa. Jambo moja tuliloongelea ni kutafsiri tamthilia yake ya Tendehogo. Basi, niliporejea hapa chuoni St. Olaf ninapofundisha, nilienda maktaba na kuagiza nakala ya tamthilia hii. Kwa vile nakala haiko hapa, waliniagizia kutoka Maktaba ya Congress iliyoko Washington DC.Nimeshapata nakala hiyo, na sasa inabidi nianze mikakati ya kuitafsiri. Kazi ya kutafsiri kazi ya fasihi ni ngumu, yenye changamoto nyingi, hata kama mtu unazijua lugha husika vizuri sana. Hata kama lugha husika ni zako za kuzaliwa nazo au za tangu utotoni, kama kilivyo ki-Matengo na ki-Swahili kwa upande wangu.
Ninasema hivyo kutokana na uzoefu. Nimejishughulisha na kutafsiri tungo za ki-Swahili na hadithi za ki-Matengo kwenda ki-Kiingereza. Niliwahi hata kuandika makala kuhusu kutafsiri hadithi ya ki-Matengo. Soma hapa.
Miaka michache iliyopita nilianza kutafsiri Tendehogo, lakini nakumbuka nilitafsiri kurasa labda mbili au tatu. Sasa, pamoja na wasi wasi nilio nao kuhusu uwezo wangu, itabidi nijipige moyo konde na kuanza kuogelea.