Hotuba zilisisitiza mambo muhimu aliyofanya na kusema Martin Luther King, Jr. Wasemaji walikumbushia wosia wake katika masuala kama haki, usawa, na elimu.
Walihudhuria watu wa kila aina: wa rangi na mataifa mbali mbali, watoto, watu wazima, na wazee, wake kwa waume. Hapo mtu ulijionea mwenyewe kuwa kweli Martin Luther King alikuwa mtu wa pekee sana, ambaye katika maisha yake aligusa mioyo ya watu sana na bado anawagusa na ataendelea hivyo kwa vizazi vijavyo.
Kulikuwa na vikundi kadhaa vilivyofanya maonesho. Waliburudisha kwa nyimbo, muziki, na staili za kucheza. Hapa kushoto ni kwaya ya watoto wavulana, ambayo ni ya watawa wa-Katoliki wa Monasteri ya St. John, iliyopo mjini Collegeville.
Hapa kushoto ni msichana Naajee Dennis, aliyeghani kwa umahiri mkubwa hotuba nzima ya Martin Luther King, Jr, "I Have a Dream." Hakuwa anaisoma, bali alikuwa ameikariri.
Kwenye shughuli kama hizi, sikosi kukutana na watu ninaofahamiana nao. Hapa kushoto ninaonekana na wa-Marekani Weusi wawili. Inapendeza kuongea na watu wa aina hiyo, kwa sababu mtazamo wao kuhusu masuala mbali mbali ya historia, maisha na ulimwengu kwa ujumla ni tofauti na wangu mimi niliyekulia Afrika.
Kulikuwa na sehemu ya maonesho ya kuelimisha umma. Nilikuwa mmoja wa washiriki. Hapa kushoto inaonekana meza yangu, nikiwa nimeanza kupanga vitabu vyangu. Kama kawaida, nilipata fursa ya kuongea na watu wengi waliofika hapa kwenye meza yangu.
3 comments:
Na kumbukumbu yake izae matunda mema! Amen!
Ndugu Kitururu, huu uliosema ndio ulikuwa ujumbe mahsusi wa wahutubiaji. Walisema kwamba haki bado haitendeki na usawa haujapatikana Marekani na duniani kwa ujumla. Kwa hivi walisisitiza umuhimu wa kuendeleza harakati.
Nashukuru kuwa watu bado wanakumbuka hilo! Kwa kuwa kirahisi anaweza kugeuzwa siasa tu kwa kuwa ana jina ambalo kirahisi huweza kutumiwa kisiasa tu hasa ukizingatia kizazi cha IPAD , IPOD na IPHONE labda wala hakina uhakika na umuhimu wake:-(
Post a Comment