Kama nakumbuka sawa sawa, tulisoma The Merchant of Venice tulipokuwa kidatu cha nne. Tulikuwa tunafahamu ki-Ingereza kiasi cha kuweza kusoma na kuelewa maandishi hayo ya Shakespeare. Ni tofauti na leo, ambapo uvivu na uzembe vimesababisha ufahamu wa ki-Ingereza udidimie sana na hata kutoweka. Uvivu huo unajitokeza pia katika ufahamu wa ki-Swahili.
Nyerere aliichapisha tafsiri yake mwaka 1969, muda mfupi tu baada ya Azimio la Arusha. Kwa hivi, tafsiri yake ilikuwa na mvuto wa pekee miongoni mwetu, kwani tulikuwa tunavutiwa na nadharia za ujamaa. Hata neno mabepari lilikuwa likitumika sana, sambamba na maneno kama mabwanyenye. Ilikuwa rahisi kuelewa kwa nini Nyerere aliamua kuitafsiri tamthilia hii ya Shakespeare. Kwa kutumia tabia, fikra, na kauli za Shailoki, mfanyabiashara wa Venisi, Shakespeare alionyesha kwa umahiri mwenendo wa ubepari. Shailoki ni kielelezo bora cha dhana ya Nyerere kuwa ubepari ni unyama.
Nimekumbuka hayo yote, na nimekitafuta kitabu cha Mabepari wa Venisi ili kujikumbusha umahiri wa Nyerere katika lugha ya ki-Ingereza na ki-Swahili. Kama kweli unakijua ki-Ingereza na ki-Swahili, huwezi ukasoma tafsiri ya Nyerere usikiri kuwa alikuwa na akili na ufahamu usio wa kawaida wa undani wa lugha hizo mbili. Hata hivi, kama wewe ni mtu makini sana, unaweza kubadili neno hapa au pale, katika tafsiri ya Nyerere. Angalia, kwa mfano, alivyotafsiri maneno ya Antonio, mwanzoni kabisa mwa tamthilia:
Ant. In sooth, I know not why I am so sad.
It wearies me; you say it wearies you;
But how I caught it, found it, or came by it,
What stuff 'tis made of, whereof it is born,
I am to learn;
And such a want-wit sadness make of me
That I have much ado to know myself.
Tafsiri ya Nyerere ni hii:
ANTONIO: Kusema kweli sijui kisa cha huzuni yangu;
Inanitabisha sana; wasema yakutabisha;
Bali nilivyoipata, au kuiambukizwa,
Au imejengekaje, imezawa jinsi gani,
Ningali sijafahamu,
Na huzuni yanifanya kuwa kama punguani,
Kunifanya nisiweze kujifahamu mwenyewe.
Kama nilivyosema, miaka ya ujana wetu, tuliweza kuelewa lugha ya Shakespeare, tena kwa undani. Leo sijui ni wa-Tanzania wangapi wanaoweza kumwelewa Shakespeare. Ngoja nilete kisehemu cha hotuba maarufu ya Portia, halafu ujaribu kutafsiri, uone unakifahamu ki-Ingereza na ki-Swahili kiasi gani:
Por. The quality of mercy is not strained,
It droppeth as the gentle rain from heaven
Upon the place beneath. It is twice blest--
It blesseth him that gives, and him that takes.
'Tis mightiest in the mightiest. It becomes
The throned monarch better than his crown.
His sceptre shows the force of temporal power,
The attribute to awe and majesty,
Wherein doth sit the dread and fear of kings;
But mercy is above this sceptred sway,
It is enthroned in the hearts of kings,
It is an attribute to God himself;
And earthly power doth then show likest God's
When mercy seasons justice.
8 comments:
safi sana hii... ila ni vipi nitakipata kitabu kizima kupitia mtandao?
Ndugu Humphrey morise
Shukrani kwa kutembelea "hapakwetu" na kuweka ujumbe wako. Sijui kama kuna mahali kinapopatikana kitabu hiki, zaidi ya mtandaoni. Hata hivi, ingekuwa wa-Tanzania wana utamaduni wa kuvithamini vitabu, haingekuwa shida hata kwa wale walioko vijijini kuvipata. Kuna wa-Tanzania wengi huku ughaibuni, kama vile Marekani, ambao wangeweza kuvinunua na kuvipeleka huko Tanzania wakati wanaposafiri kuja huko.
Binafsi, kila ninapokuja Tanzania, ninabeba vitabu angalau vichache, na nimekuwa nikivitoa bure kwenye maktaba na vyuo. Kama wa-Tanzania hao wanaweza kubeba vipodojizi, marashi au mizinga ya "whisky," sielewi kwa nini washindwe kubeba vitabu viwili vitatu. Na wa-Tanzania walioko nyumbani kama wangekuwa wanaagiza waletewe vitabu, sidhani kama kungekuwa na tatizo. Lakini je, wanawazia vitabu au mizinga ya "whisky" na viatu vya Michael Jordan?
Kwa mara ya kwanza nilipokisoma kitabu cha "Merchant of Venice" nilipata wakati mgumu kielewa lakini niliposoma fasili yake iliyoandikwa na Mwl Nyerere hapo ndipo nilifurahia lugha.
Nakili Nyerere aliifaham na kuiishi lugha.
Nilifurahia alivyoweza kuongeza chumvi (figurate language)zilioendana na tamaduni na mazingira ya Tanzania kama "Nguo zake ni shaghala baghala"
Kweli lugha ina raha yake.
Habari.. Prof hujatusiadia bado namna ya kupata kitabu hicho na vingine vizuri. Na kama ni vyema ukafugua Maktaba huku tz ingesaidia kurudisha umuhimu wa kusoma vitabu kwa maarifa zaidi.
Ndugu Anonymous ulieandika June 11, 2016 at 2:10, ni kweli kuwa Mwalimu Nyerere alizifahamu hizi lugha mbili sana. Tukizingatia kwamba kutafsiri kunahitaji sio tu ufahamu wa lugha bali pia ubunifu, sijui kama kuna mtu ninayemfahamu katika nchi yetu anayemfikia Mwalimu Nyerere.
Ndugu Chrisper Malamsha,
Shukrani kwa ujumbe wako. Nimeona kuwa toleo la "Kindle" linapatikana kwenye mtandao wa Amazon.com, lakini madukani nadhani hakipatikani tena. Katika maktaba kubwa kubwa kinapatikana.
Kuhusu maktaba yangu binafsi, nina vitabu zaidi ya 3,000 na lengo langu ni kuanzisha maktaba binafsi huko huko Tanzania. Bado sijaamua mji gani, ila naona ni wazo bora kabisa.
Cultural aspects are an important ingredient that should be taken into account when translating a literary text. Discuss this assertion with plenty of examples from Shakespeare's Merchant of Venice and its Kiswahili translation Mabepari wa Venisi.
Nimefurahishwa pia na kitabu hiki Ila natamani ningepitia chapa ya kingereza kwani ya kiswahili ilinivutia sana library hiyo yaweza tusaidia sana hasa sisi tunaokua kielimu katika lugha. Asante sana
Post a Comment