Wednesday, January 25, 2012

Mfanya usafi akamatwa akimlawiti mtoto msikitini

Habari hii inahuzunisha, nikizingatia jinsi mtoto huyu alivyohujumiwa maisha yake na haki zake za kibinadamu, nikizingatia uchungu wa mama yake, ndugu, jamaa, marafiki na wapenda haki. Habari hii inapaswa kutangazwa, ijulikane, ili angalau iwe faraja kwa mtoto huyu na mama yake, kwamba tuko tunaojali utu na haki, na tuko pamoja nao.

Habari hii imetokea msikitini. Hivi juzi, wanafunzi wa ki-Islam walipoandika waraka wakiorodhesha hujuma walizosema wanafanyiwa wa-Islam mashuleni, niliandika ujumbe kuwaunga mkono katika kulaani hujuma hizo. Soma hapa. Nilisukumwa na maadili ya kuzingatia haki, niliyofundishwa katika imani yangu ya u-Katoliki.

Sasa basi, ni muhimu wa-Islam, wa-Kristu, na wengine wote tuungane kumpigania mtoto huyu aliyelawitiwa msikitini, na watoto wengine wanaotendewa vitendo hivi, na wengine wote wanaohujumiwa haki zao. Tuungane kukemea maovu yote na kupigania haki za wote.

Ni lazima tufanye hivyo, ili angalau kumpunguzia mtoto huyu matatizo ya kisaikolojia ambayo yatamwandama maishani. Akiwa ni mtoto mu-Islam, atakuwa anasikiliza mahubiri yanayosisitiza kwamba wa-Islam wanahujumiwa na wa-Kristu, hasa wa-Katoliki. Atakuwa anasikiliza mihadhara ambayo inawaongelea wa-Islam kama watu wasio na dosari, watu wasio na ubaya na mtu, bali wenye dosari ni wa-Kristo, na katika wa-Kristo, hasa wa-Katoliki. Ataambiwa adui yake mkuu ni mfumo Kristo. Hatasikia kuwa wa-Islam ni sawa na wa-Kristu katika uwezo wa kufanya mema au mabaya. Hatasikia kuhusu hujuma zinazoweza kufanywa na wa-Islam, hata dhidi ya wa-Islam wengine, kama ilivyomtokea yeye.

Hapa ndipo ninaposema pana hatari kubwa ya kumbebesha mtoto huyu mzigo wa machungu kisaikolojia. Kutokumweleza kuwa wa-Islam nao wanaweza kuwa wabaya itakuwa ni kumwongezea kejeli juu ya machungu. Tuungane kumwepusha na hayo, kwa kadiri iwezekanavyo. Labda kwa njia hii ya kuyatangaza na kuyakemea maovu yanayotokea nchini mwetu, tutayapunguza au kuyatokomeza.

--------------------------------------------------

Chanzo: MWANANCHI


Mfanya usafi akamatwa akimlawiti mtoto msikitini
Tuesday, 24 January 2012 20:40

Hamisi Mwesi, Dodoma
POLISI mkoa hapa inamshikilia mkazi wa Bahi Road, Manispaa ya Dodoma, kwa tuhuma za kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka tisa baada ya kumpa Sh500 ili kumfichia siri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen, alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni mfanya usafi wa Msikiti wa Ghazal uliopo eneo la Majengo, alitenda kosa hilo juzi saa 12:00 jioni.

Stephen alisema baada ya polisi kupewa taarifa na wananchi wa eneo hilo, walifika msikitini hapo na kumkamata mtuhumiwa akiwa ndani ya choo cha wanawake alipokuwa akifanyia mtoto kitendo hicho cha kinyama.

“Polisi walijulishwa na wananchi waliokuwapo eneo hilo kwamba mtuhumiwa alimuingiza mtoto huyo kwenye choo cha wanawake na kujifungia ndani, watu waliokuwa jirani na eneo hilo walifuatilia kwa makini ndipo waliposhuhudia mtuhumiwa akimlawiti mtoto huyo na kutoa taarifa polisi,” alisema Stephen.

Alisema mtoto huyo amelazwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma kutokana na maumivu, kutokana na kitendo hicho na hali yake inaendelea vizuri na uchunguzi juu ya afya yake unafanyika kubaini athari zaidi.

Alisema mama mzazi wa mtoto huyo, alimg’ata sikio la kulia mtuhumiwa huyo kwa hasira na kunyofoka nusu ya sikio lake na kwamba, hivi sasa wanashikiliwa.

Inadaiwa mtuhumiwa amekuwa na tabia hiyo muda mrefu na waumini wa msikiti huo waliwahi kumuonya, baada ya kutiliwa shaka kuhusu kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo hawakuwa na ushahidi, ndipo walipoamua kuanza upelelezi dhidi yake.

“Waumini walishamshtukia mtuhumiwa, wakaanza kufuatilia nyendo zake kwani yeye muda mwingi hukaa msikitini kwa ajili ya kufanya usafi, wakati mwingine kutoa adhana kwa ajili ya swala, leo (juzi) amenaswa na mtego baada ya kumtanguliza mtoto choo cha wanawake na yeye kumfuata,” alisema mmoja wa waumini wa msikiti huo.

6 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Kwa kweli inasikitisha sana hapo kwangu pia nimekutana leo na habari kutoka kwetu Ruhuwiko kijana kmbaka mamake...Tutafika kweli???

Mbele said...

Dada Yasinta, nami nilisoma ile habari ya Ruhuwiko. Ina sikitisha na inatisha. Zamani kulikuwa na miiko, ambayo ilizitunza jamii vizuri. Leo miiko inazidi kutoweka. Inatisha.

tz biashara said...

Masikitiko makubwa sana na ni maafa makubwa kwa jamii yetu hasa watoto wetu hawana amani ya maisha ya utoto wao.Na kama ingekuwa ni sheria ya kiisilamu hapo ni kifo tu.

Lakini kwa upande mwingine nawashauri wazazi wajaribu kuwa karibu na watoto wao.Hakuna maisha ya haki duniani na maovu yanaendelea kuzidi.Ikiwa mtu anaweza kumdhulumu kwa kumtendea ubaya mtoto wa miaka 9 tena ktk nyumba ya ibada basi tusiwe tunaishi maisha ya kumuamini kila mtu.

Utakuta watoto wadogo wanazurura mitaani na wazazi wao hawana habari nini kinachotokea.Watoto hawana nguvu na maarifa ya kujiwekea usalama wenyewe na hivo wazazi wanahitaji kuwaweka ktk mazingira mazuri na yenye usalama.

Kuna wale watoto wanaolala mitaani hawana sehemu za kuishi na hawana wazazi,wanabakwa kila siku.Kwanini suala hili halishughulikiwi na ustawi wa jamii?

Inabidi serikali iwajibike kuangalia watoto wanaozurura mitaani na kuwashitaki wazazi kwa kutowaangalia au kuwapa usalama.Au kuwanyang'anya watoto kwa muda fulani mpaka wajirekebishe.

Anonymous said...

NI HUZUNI KUBWA IMENIPATA BAADA YA KUSOMA HII HABARI.SIJUI NIANZE WAPI!!! JAMII NZIMA INA JUKUMU LA KUHAKIKISHA HAWA WATOTO WAKO KATIKA HALI YA USALAMA LAKINI JAMANI MTOTO WAKO YUKO MSIKITINI AU KAENDA KANISANI VILE VILE BASI MZAZI/JAMII IWE KATIKA HALI YA WASIWASI KUWA MTOTO KITAMTOKEZEA NINI AKIWA HUKO? JAMANI MBONA TUMEKUWA KAMA WANYAMA?MACHOZI YANANITOKA KWA KUANDIKA HAYA MAONI TU.

Simon Kitururu said...

DUH Jamani!:-(

Mbele said...

Na huyu ndiye mfanya usafi. Tumekwisha.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...