Showing posts with label kusaini vitabu. Show all posts
Showing posts with label kusaini vitabu. Show all posts

Saturday, January 2, 2016

Kitabu Kinaposainiwa

Leo napenda kuirejesha mada ya kusainiwa vitabu, ambayo nimewahi kuileta katika blogu hii. Wanablogu wengine nao wameiongelea. Kwa mfano, Christian Bwaya amelielezea suala la kusaini vitabu kama jambo la ajabu, akatumia dhana ya muujiza. Nakubaliana na dhana hiyo, kutokana na uzoefu wangu kama mwandishi ambaye nimesaini vitabu vyangu mara nyingi, na pia mnunuaji wa vitabu ambaye nimesainiwa vitabu mara kwa mara. Hapa kushoto ninaonekana nikisaini kitabu changu mjini Faribault, Minnesota. Huyu ninayemsainia ni binti kutoka Sudan.


Ninafahamu muujiza huu unavyokuwa kwa pande zote mbili, mwenye kusaini kitabu chake na mwenye kusainiwa. Ninadiriki kusema kuwa kitendo cha kusainiwa kitabu kinafanana na ibada. Natumia neno ibada kwa maana ile ile ya dhana ya ki-Ingereza ya "ritual." Hapo kushoto anaonekana mwandishi Seena Oromia akinisainia kitabu chake mjini Minneapolis.

Ibada ni sehemu ya kila utamaduni, na kila ibada ina utaratibu wake, iwe ni misa kanisani, mazishi, au kitendo cha watu kula pamoja. Wahusika katika ibada wanapaswa kuzifahamu na kuzifuata taratibu hizo. Ibada ya kusainiwa kitabu ni tukio linalogusa nafsi na hisia ya anayesaini kitabu na yule anayesainiwa kitabu.

Ni tukio linaloambatana na heshima ya aina yake. Angalia tu picha nilizoweka hapa; utaona zinavyojieleza. Kuna usemi katika ki-Ingereza kwamba "A picture is worth a thousand words," yaani picha ina thamani sawa na maneno elfu. Hapa kushoto anaonekana mwandishi Jim Heynen akisaini kitabu chuoni St. Olaf.

Kwa ujumla wewe mwandishi huwajui watu wanaotaka kusainiwa vitabu. Inabidi uwaulize uandike jina gani. Wengine huwa wamenunua vitabu viwili au zaidi. Unawauliza usaini jina gani, kwa kila kitabu, nao wanakutajia jina lao au la mtu mwingine au watu wengine.  Hapa kushoto ninaonekana nikisaini vitabu vyangu katika mkutano Grantsburg, Wisconsin.

Kifalsafa, suala la kumsainia kitabu mtu ambaye humwoni ni jambo linalofikirisha. Mwandishi unajifanya unamjua unayemsainia, ingawa humjui. Naye, atakapokipata kitabu, atajiona kama vile kuna uhusiano baina yake na wewe mwandishi. Anafurahi kama vile mmeonana. Hii dhana ya kuonana imejengeka katika usomaji. Tunaposoma, tunakuwa na hisia ya kukutana na mwandishi, hata kama hayuko mbele yetu kimwili. Lakini tunaposhika kitabu ambacho tumesainiwa, ukaribu huo unakuwa mkubwa zaidi. Ni aina ya undugu.

Hapa kushoto naonekana nikisaini kitabu mjini Brooklyn Park, Minnesota. Ninayemsainia ni Adrian Mack, Mmarekani Mweusi.

Monday, October 19, 2015

Matamasha ya Vitabu: Tanzania na Marekani

Nimehudhuria matamasha ya vitabu Tanzania na Marekani. Kwa usahihi zaidi, niseme nimeshiriki matamasha hayo, kama mwandishi, nikiwa na meza ya vitabu vyangu. Nimeona tofauti baina ya Tanzania na Marekani katika uendeshaji wa matamasha haya. Hapa napenda kugusia kidogo suala hilo, nikizingatia kwamba ni suala linalowahusu waandishi, wasomaji, wachapishaji na wauza vitabu.

Tofauti moja ya wazi ni kuwa matamasha ya vitabu ni mengi zaidi, maradufu, Marekani kuliko Tanzania. Marekani kuna matamasha makubwa ya kitaifa na matamasha makubwa kiasi ya kiwango cha majimbo, na pia matamasha ya kiwango cha miji. Mtu ukitaka, unaweza kuzunguka nchini Marekani ukahudhuria matamasha ya vitabu kila wiki, kila mwezi, mwaka mzima. Angalia, kwa mfano, orodha hii hapa. na hii hapa.

Kwa upande wa Tanzania, hali ni tofauti. Matamasha ya vitabu hayafanyiki mara nyingi. Tunaweza kuwa na tamasha la vitabu la kitaifa mara moja kwa mwaka. Lakini hatuna utamaduni wa kuwa na matamasha ya sehemu mbali mbali za nchi, kwa mfano tamasha la vitabu mikoa ya Kusini, tamasha la vitabu mikoa ya Magharibi, mikoa ya Mashariki, na kadhalika.

Tofauti hizi zinatokana na tofauti za utamaduni wa kusoma vitabu. Utamaduni wa kusoma vitabu umejengeka miongoni mwa watu wa Marekani, tangu utotoni. Watoto, hata wanapokuwa wadogo sana, husomewa vitabu; vijana, watu wazima, na wazee husoma vitabu. Utawakuta katika matamasha ya vitabu, kama ninavyoeleza mara kwa mara katika blogu hii.

Katika matamasha ya vitabu ya Marekani, ni kawaida waandishi kuwepo. Wengine huja kuonesha na kuuza vitabu vyao. Wengine huwa wamealikwa kama wageni rasmi. Waandishi huongelea vitabu vyao. Nilivyoona Tanzania ni kwamba wachapishaji ndio huleta vitabu kwenye matamasha. Mtu ukihudhuria matamasha hayo, ukawa na hamu ya kujua kuhusu vitabu vya mwandishi fulani, utaongea na mchapishaji. Mwandishi humwoni.

Ninaona kuwa hii ni dosari. Ni jambo ambalo tunaloweza kujifunza kutoka kwa wa-Marekani. Kuwepo kwa waandishi ni kivutio kimojawapo katika matamasha ya vitabu. Hapa Marekani, ni kawaida kuona matangazo katika vyombo vya habari, au mabango kwenye meza za waandishi yameandikwa "MEET THE AUTHOR." Ni kivutio. Watu hupenda kuonana na waandishi, kuongea nao, kununua vitabu na kusainiwa, na pia kupiga nao picha.

Utaratibu huu ungeweza kufanyika Tanzania, ungesaidia. Ninafahamu, kwa mfano, kwamba wengi wanalijua jina la Ngoswe. Wamesikia, na wanatumia usemi "Ya Ngoswe mwachie mwenyewe Ngoswe." Lakini hawajui asili ya jina Ngoswe. Kumbe, hili ni jina la tamthilia ya Ngoswe: Penzi Kitovu cha Uzembe iliyotungwa na Edwin Semzaba.

Kutokana na umaarufu wa jina la Ngoswe, kama waandaaji wa tamasha la vitabu wangeweka tangazo kuwa mtunzi wa Ngoswe atakuwepo katika tamasha, naamini itakuwa ni kivutio kwa watu kuhudhuria tamasha. Ninaweza kutoa mifano mingine. Jina kama Kinjeketile ni maarufu. Ebrahim Hussein, mwandishi wa tamthilia ya Kinjeketile akijitokeza katika tamasha la vitabu, atakuwa kivutio. Kadhalika Euphrase Kezilahabi, mwandishi wa riwaya maarufu kama Rosa Mistika na Dunia Uwanja wa Fujo.

Waandishi, wachapishaji, na wadau wengine wa vitabu tunakubaliana kwamba kuna haja kubwa ya kujenga utamaduni wa kusoma vitabu katika nchi yetu ya Tanzania. Hilo wazo langu la kuboresha matamasha ya vitabu huenda likachangia mafanikio ya ndoto yetu.

Monday, August 4, 2014

Furaha ya Kusainiwa Kitabu

Wapenzi wa vitabu wakishajipatia nakala ya kitabu cha mwandishi fulani, huguswa pale mwandishi anaposaini kitabu hicho. Aghalabu mwandishi huandika ujumbe mfupi kwa mteja huyu na kasha kuweka sahihi. Ni jambo linalowagusa sana wasomaji. Mimi mwenyewe, kama mwandishi, nimeshasaini vitabu vyangu vingi. Ninazo baadhi ya picha za matukio haya kutoka miaka iliyopita.

Msomaji makini na mwanablogu Christian Bwaya hivi karibuni ameelezea vizuri katika blogu yake, hisia zake baada ya kujipatia kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differencesambacho nilikuwa nimekisaini:

Namshukuru kwa dhati mwandishi wa kitabu hiki, Prof. Mbele kwa kunitumia kitabu hiki bila malipo, tena kwa gharama zake. Si jambo linalowatokea wengi. Ni furaha iliyoje hatimaye nimekipokea leo asubuhi. Naanza kukisoma kitabu hiki kwa mara nyingine, safari hii kikiwa na saini ya mwandishi. Ni upendeleo na muujiza wa pekee kunitokea katika siku za hivi karibuni. Ni lazima nimshukuru kwa dhati. Asante sana Profesa.

Utamaduni wa kusaini na kusainiwa vitabu nimeuzoea. Hata juzi tarehe 2 Agosti, niliposhiriki tamasha la Afrifest kule Brooklyn Park, Minnesota, nikiwa na vitabu vyangu, wadau kadhaa walionunua vitabu vyangu waliomba kusainiwa.

Hapa kushoto anaonekana mdau akiniangalia wakati nasaini nakala ya Matengo Folktales, ambayo alikuwa amenunua hapo.
Baada ya kusainiwa nakala yake, aliona furaha ya ziada kupiga picha nami huku akiwa ameshika kitabu hicho. Hiyo nayo ni kawaida hapa Marekani; wadau wakishanunua kitabu na kusainiwa, wanapenda kupiga picha na mwandishi, ikiwezekana.

Mdau huyu, aitwaye Adrian, m-Marekani Mweusi, alinifahamu tangu miaka kadhaa iliyopita. Alikuwa anasoma katika chuo fulani mjini Minneapolis. Kulikuwa na mkutano wa kitaaluma, nami nilikuwa mmoja wa wanajopo, nikitoa mada. Adrian alivutiwa sana. Halafu, alinisikiliza tena mwaka jana, nilipokuwa naongea katika jopo la watu wawili, nikiwa na Profesa Mahmud el-Khati, m-Marekani Mweusi, tukiongelea mbele ya umati, mahusiano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi.

Adrian ni msomi kijana makini. Tayari naona nyota yake imeanza kung'ara katika medani ya uongozi katika jamii. Nina imani atafika mbali katika jamii ya wa-Marekani weusi na Marekani kwa ujumla.
Hapa kushoto ni picha nyingine, kutoka hiyo hiyo juzi katika tamasha la Afrifest, nikiwa na mdau kutoka Liberia, ambaye alikuwa amenunua kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, nami nikiwa nimekisaini. Inaonekana aliguswa sana, na hakuweza kujizuia kuniwekea mkono wake begani pangu.

Suala hili la kusaini au kusainiwa vitabu linastahili  kutafakariwa. Naamini lina vipengele kadhaa muhimu, kama vile kiutamaduni, kisoshiolojia, kisaikolojia, na kifalsafa. hata katika maduka ya vitabu hapa Marekani, aghalabu utaona vimepangwa vitabu vya mwandishi vikiwa na ujumbe "Signed copy." Jambo hili linaisukuma akili yangu kutaka kulielewa zaidi. Ningependa kujifunza zaidi kuhusu suala hili, kwa kusoma maandishi mbali mbali na kufanya tafakari mwenyewe.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...