Monday, October 19, 2015

Matamasha ya Vitabu: Tanzania na Marekani

Nimehudhuria matamasha ya vitabu Tanzania na Marekani. Kwa usahihi zaidi, niseme nimeshiriki matamasha hayo, kama mwandishi, nikiwa na meza ya vitabu vyangu. Nimeona tofauti baina ya Tanzania na Marekani katika uendeshaji wa matamasha haya. Hapa napenda kugusia kidogo suala hilo, nikizingatia kwamba ni suala linalowahusu waandishi, wasomaji, wachapishaji na wauza vitabu.

Tofauti moja ya wazi ni kuwa matamasha ya vitabu ni mengi zaidi, maradufu, Marekani kuliko Tanzania. Marekani kuna matamasha makubwa ya kitaifa na matamasha makubwa kiasi ya kiwango cha majimbo, na pia matamasha ya kiwango cha miji. Mtu ukitaka, unaweza kuzunguka nchini Marekani ukahudhuria matamasha ya vitabu kila wiki, kila mwezi, mwaka mzima. Angalia, kwa mfano, orodha hii hapa. na hii hapa.

Kwa upande wa Tanzania, hali ni tofauti. Matamasha ya vitabu hayafanyiki mara nyingi. Tunaweza kuwa na tamasha la vitabu la kitaifa mara moja kwa mwaka. Lakini hatuna utamaduni wa kuwa na matamasha ya sehemu mbali mbali za nchi, kwa mfano tamasha la vitabu mikoa ya Kusini, tamasha la vitabu mikoa ya Magharibi, mikoa ya Mashariki, na kadhalika.

Tofauti hizi zinatokana na tofauti za utamaduni wa kusoma vitabu. Utamaduni wa kusoma vitabu umejengeka miongoni mwa watu wa Marekani, tangu utotoni. Watoto, hata wanapokuwa wadogo sana, husomewa vitabu; vijana, watu wazima, na wazee husoma vitabu. Utawakuta katika matamasha ya vitabu, kama ninavyoeleza mara kwa mara katika blogu hii.

Katika matamasha ya vitabu ya Marekani, ni kawaida waandishi kuwepo. Wengine huja kuonesha na kuuza vitabu vyao. Wengine huwa wamealikwa kama wageni rasmi. Waandishi huongelea vitabu vyao. Nilivyoona Tanzania ni kwamba wachapishaji ndio huleta vitabu kwenye matamasha. Mtu ukihudhuria matamasha hayo, ukawa na hamu ya kujua kuhusu vitabu vya mwandishi fulani, utaongea na mchapishaji. Mwandishi humwoni.

Ninaona kuwa hii ni dosari. Ni jambo ambalo tunaloweza kujifunza kutoka kwa wa-Marekani. Kuwepo kwa waandishi ni kivutio kimojawapo katika matamasha ya vitabu. Hapa Marekani, ni kawaida kuona matangazo katika vyombo vya habari, au mabango kwenye meza za waandishi yameandikwa "MEET THE AUTHOR." Ni kivutio. Watu hupenda kuonana na waandishi, kuongea nao, kununua vitabu na kusainiwa, na pia kupiga nao picha.

Utaratibu huu ungeweza kufanyika Tanzania, ungesaidia. Ninafahamu, kwa mfano, kwamba wengi wanalijua jina la Ngoswe. Wamesikia, na wanatumia usemi "Ya Ngoswe mwachie mwenyewe Ngoswe." Lakini hawajui asili ya jina Ngoswe. Kumbe, hili ni jina la tamthilia ya Ngoswe: Penzi Kitovu cha Uzembe iliyotungwa na Edwin Semzaba.

Kutokana na umaarufu wa jina la Ngoswe, kama waandaaji wa tamasha la vitabu wangeweka tangazo kuwa mtunzi wa Ngoswe atakuwepo katika tamasha, naamini itakuwa ni kivutio kwa watu kuhudhuria tamasha. Ninaweza kutoa mifano mingine. Jina kama Kinjeketile ni maarufu. Ebrahim Hussein, mwandishi wa tamthilia ya Kinjeketile akijitokeza katika tamasha la vitabu, atakuwa kivutio. Kadhalika Euphrase Kezilahabi, mwandishi wa riwaya maarufu kama Rosa Mistika na Dunia Uwanja wa Fujo.

Waandishi, wachapishaji, na wadau wengine wa vitabu tunakubaliana kwamba kuna haja kubwa ya kujenga utamaduni wa kusoma vitabu katika nchi yetu ya Tanzania. Hilo wazo langu la kuboresha matamasha ya vitabu huenda likachangia mafanikio ya ndoto yetu.

4 comments:

Pascal Bacuez said...

Tahania na pongezi za dhati zikufikie mwenzangu kuona kwamba huchoki hapo kuhamasisha watu wasome ! Ila najiuliza, ni kweli kwamba katika nchi za magharibi (pamoja na mashariki…) vitabu vinaonyeshwa katika matamasha mbalimbali na vinauzwa kwa vingi sana, lakini je kweli vinasomwa ? Unajua jinsi soko huria imekuwa kichocheo kikubwa katika maisha ya watu hadi wengi wanakubali kuzugwa au kushawishiwa na mazonge haya ya ununuzi ilhali hawana hamu ya ndani ya kusoma vile vitabu wanavyoona. Wengi hununua vitabu kisha wanaviacha juu ya rafu zao kama pambo tu au souvenir ! Lakini hata hivyo, afadhali huko huko Uzunguni kuliko EAC ambapo… najiuliza, kweli wapo wasomaji huko ?? Wa salaam, tushike uzi bwana !

Mbele said...

Ndugu Pascal Bacuez,

Masuali yako ni mazuri na muhimu kuyazingatia. Uzuri wa mazungumzo kama haya katika blogu ni maongezi ya kawaida ya kupeana taarifa, kubadilishana mawazo na uzoefu, na hata hisia. Kuishi kwangu Marekani kumenijengea ufahamu, fikra, na hisia mbali mbali, ambazo ninazielezea bila kusita, kama ninavyofanya katika kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Ajabu ni kwamba, ingawa ninayosema kuhusu wa-Marekani katika kitabu hiki ni yale niliyojione na ninayojionea, bila utafiti wa kisayansi, wao wenyewe wanavutiwa wanapoyasoma, na yale ninayosema kuhusu wa-Afrika nayo pia yanawavutia wa-Afrika. Wananiambia kuwa nimesema ukweli, ingawa sehemu nyungi za Afrika sijafika na sitafika.

Basi ni hivyo hivyo kuhusu yale nisemayo juu ya usomaji. Lazima nikiri kuwa kwa kiasi fulani ni "anecdotal," kwa ki-Ingereza. Siku chache zilizopita, kwa mfano, nilikwenda kuonana na daktari katika hospitali moja kubwa mjini Minneapolis. Kwenye sehemu ya mapokezi, nilikaa karibu na bwana mmoja na mama mmoja, ambao niliona wamenizidi umri kiasi. Niliwasikia wakiongelea vitabu walivyosoma. Nilikaa nikawa najiuliza, Je, jambo hili lingeweza kutokea nchini mwangu Tanzania?

Basi katika kuishi hapa Marekani na kukutana na mambo ya namna hii na mengine mengi, siku hadi siku, mtu unafikia uamuzi kwamba hao wenzetu wana utamaduni wa kusoma vitabu, tofauti na sisi.

Pascal Bacuez said...

Sawa sawa ndugu Mbele, lakini tukiangalia mwelekeo katika kipindi kirefu, mathalan Ufaransa, tunaona kwamba utamaduni huo, ambao ulikuwa mkubwa sana si zamani sana, umeregea sana siku hizi kiasi cha kuathiri lugha yenyewe ya kifaransa. Wengi katika wasayansi huafiki kwamba kuvurugika kwa utamaduni huo umesababishwa na hali mpya ya maisha ambayo imeletwa, kwa kifupi, na "soko huria" au utandawazi. Na tuko wengi katika nchi hizo kuamini kwamba kujikomboa itakuwa kazi ngumu sana. Tatizo lililopo Tanzania ni kwamba watanzania hawasomi, na itakuwa vigumu "kuwapandikizia" utamaduni huo kwa sababu Tanzania, kama ilivyo Ulaya na kote duniani sasa hivi, kumeingia katika utamaduni wa "jumbe pepe" kupitia simu, kompyuta na teknolojia mpya ambazo hazimjengei mtu utamaduni wa kusoma. Hilo ni balaa kwa sababu eti ni maendeleo ! Hata hivyo, mimi nazidi kujiuliza kuhusu umuhimu wa kusoma. Huko Kilwa nilikoishi miaka mingi, nilibahatika kukutana na watu ambao walikuwa hawana elimu kwa maana ya elimu rasmi (ya serikali), bali walikuwa na maarifa asiliya, kama wataalamu wanavyosema siku hizi, basi hawa jamaa wana muono, mtizamo, ujuzi, hekima na « elimu » ya juu, jambo ambalo hata Profesa ya Chuo kikuu yeyote ya dunia yetu litamshinda.

Mbele said...

Ndugu Pascal Bacuez

Mimi pia naviona vitabu kama njia moja tu ya kupatia elimu. Sio njia pekee. Na ingawa nimesoma sana elimu ya shuleni na vyuoni, utafiti wangu nafanya zaidi nje ya maktaba, katika jamii, hadi vijijini. Ninawatambua wazee wa vijijini kama wale ulioishi nao Kilwa kuwa ni hazina kubwa ya elimu, maarifa, na hekima. Masimulizi kama yale uliyorekodi ni ushahidi tosha wa hoja hiyo. Ninaijali sana elimu ya kijijini.