Monday, October 26, 2015

Shukrani kwa Wa-Tanzania Wadau wa Kitabu Changu

Blogu yangu ni mahali ninapojiandikia mambo yoyote kwa namna nipendayo. Siwajibiki kwa mtu yeyote, wala sina mgeni rasmi. Leo nimewazia mafanikio ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nimejikumbusha kuwa mtu hufanikiwi kwa juhudi zako pekee, hata ungekuwa hodari namna gani. Kuna watu unaopaswa kuwashukuru.

Nami napenda kufanya hivyo, kama ilivyo jadi yangu. Nimewahi kuwaongelea na kuwashukuru wanablogu wa-Tanzania, na nimewahi kuwaongelea na kuwashukuru wa-Kenya. Ninapenda kuendelea kuwakumbuka wa-Tanzania.


Mwanzoni kabisa, nilipokuwa nimeandika mswada wa awali kabisa wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, rafiki yangu Profesa Joe Lugalla, wa Chuo Kikuu cha New Hampshire, alipata kuusoma, akapendezwa nao.

Yeye, kwa jinsi alivyoupokea mswada ule, alikuwa kati ya watu wa mwanzo kabisa kunitia hamasa ya kuuboresha. Tangu wakati ule hadi leo amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha watu wakisome kitabu hiki. Kwangu hili ni jambo la kushukuru sana, nikizingatia kuwa Profesa Lugalla sio tu ni m-Tanzania mwenzangu anayefahamu ninachosema kitabuni, bali pia yeye ni mtaalam wa kimataifa wa soshiolojia na anthropolojia.


Mtu mwingine aliyenihamasisha tangu miaka ya mwanzo ya kuwepo kwa kitabu changu ni Mhashamu Askofu Owdenburg Mdegella wa dayasisi ya Iringa ya Kanisa la ki-Luteri Tanzania. Nakumbuka tulivyokutana katika eneo la shule ya Peace House, Arusha, na hapo hapo akaanza kuongelea kitabu changu, akisema kuwa ni muhimu wazungu wakisome ili watufahamu sisi wa-Afrika. Siwezi kusahau kauli yake hiyo na namna alivyoongea kwa msisimko. Nilimwelewa vizuri kwa nini aliongea hivyo, kwani yeye anahusika moja kwa moja na mipango ya ushirikiano baina ya wa-Marekani na wa-Tanzania, hasa wa Iringa.


Dada Subi, mwanablogu maarufu miongoni mwa wa-Tanzania, ni mtu mwingine ambaye namkumbuka kwa namna ya pekee, kwa yote aliyofanya katika kunihamasisha na kukipigia debe kitabu changu. Nakumbuka aliwahi kuwasiliana nami juu ya kitabu hiki, lakini cha zaidi ni kuwa alikipigia debe katika blogu yake.

Dada Subi alinisaidia sana katika shughuli zangu za kublogu. Ingawa hatujawahi kuonana, ninamfahamu ni mkarimu sana.




Napenda nichukue fursa hii kumtaja na kumshukuru Bwana Muhiddin Issa Michuzi, mwanablogu maarufu wetu wa-Tanzania. Ingawa tumewahi kukutana mara moja tu, Michuzi amekuwa mstari wa mbele kutangaza shughuli zangu katika blogu yake, ikiwemo kitabu changu. Kutokana na hayo tumekuwa kama watu tuliozoeana. Kwangu hilo ni jambo la kushukuru.

Sitachoka kuwashukuru wachangiaji wa mafanikio yangu. Kama nilivyosema, hakuna mtu anayefanikiwa kwa uwezo wake peke yake. Ule usemi wa ki-Ingereza, "No man is an island," yaani hakuna mtu ambaye ni kisiwa, una ukweli usiopingika.

Kwa wanaotaka, walioko Tanzania, Kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kinapatikana Burunge Visitor Centre, simu 0754 297 504.

2 comments:

Khalfan Abdallah Salim said...

Nikupongeze kwa ujasiri wa kukitangaza kitabu chako katika blogu yako. Nijambo la maana sana kwa mwandishi kulifanya hasa yeye mwenyewe, maana umeandika ili watu wasome!

Naomba unifahamishe iwapo unajuwa wapi hapa Nairobi naweza kupata kitabu hiki.

Ahsante.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim,

Shukrani kwa ujumbe wako.

Katika kusoma makala na vitabu kuhusu uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu, nimejifunza na ninaendelea kujifunza mengi. Moja ni kwamba mwandishi unapaswa kubeba jukumu la kutangaza vitabu vyako. Hata kama mchapishaji anachangia, mwandishi hutakiwi kujiziuka. Ukishachapisha kitabu, kazi yako imekwisha. Wanasema hapo ni mwanzo wa kazi nyingine kubwa. Nami, yale ninayojiifunza ninayaeleza katika blogu hii na kuyatekeleza, nikitegemea kuwa wengine watafaidika nayo.

Kuhusu upatikanaji wa kitabu hiki, kwa sasa kinapatikana Tanzania tu, kama nilivyoelezea hapa juu, ukiachilia mbali mtandaoni. Ningekuwa mfanyabiashara au mjasiriamali ningekuwa nimekisambaza sehemu nyingi huko Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.