Friday, October 9, 2015

Nimepata Toleo Jipya la "Green Hills of Africa"

Leo ni siku ya furaha kwangu. Nimepata nakala ya toleo jipya la Green Hills of Africa, kitabu cha Ernest Hemingway, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1935. Taarifa kwamba toleo hili lilikuwa linaandaliwa nilielezwa na Mzee Patrick Hemingway, kama nilivyoandika katika blogu hii. Kwa hivi, nilipogundua kwamba limechapishwa, niliagiza nakala hima.

Katika Green Hills of Africa, Hemingway anaelezea mizunguko yake katika nchi ya Tanganyika, mwaka 1933-34, akiwa na mke wake wa pili Pauline Pfeiffer. Anaelezea uzuri wa nchi, watu wa makabila, tamaduni, na dini mbali mbali, na wanyama katika mbuga alimowinda, kama vile Serengeti na eneo la Ziwa Manyara. Anaelezea miji alimopita, kama vile Mto wa Mbu, Babati, Kondoa, Handeni, na Tanga.

Toleo hili la Green Hills of Africa lina mambo ambayo hayakuwemo katika toleo la mwanzo, kama vile maandishi ya awali ambayo hayakutokea kitabuni, picha, na hata "diary" aliyoandika Pauline alipokuwa safarini na mumewe. Nilijua kuwa "diary" hii imehifadhiwa katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Stanford, na nilikuwa nawazia kwenda kuisoma. Kuchapishwa kwake katika toleo hili ni jambo la kufurahisha sana.

Kutokana na jinsi Hemingway alivyoielezea nchi yetu, tukio la kuchapishwa kwa toleo hili la Green Hills of Africa mwaka huu ilipaswa tulipokee kwa shamra shamra. Pangekuwa na shughuli za uzinduzi wa toleo hili, makongamano, na tahakiki magazetini. Nakala zingejaa katika maduka ya vitabu, na wateja wangekuwa wanapigana vikumbo kuzinunua.

Sehemu zingine duniani wanatumia vilivyo bahati ya kutembelewa na Hemingway na kuandikwa katika maandishi yake. Ni kivutio kikubwa kwa watalii, kama ninavyosema katika blogu hii. Sisi tumeifanya nchi yetu kuwa kwenye miti ambako hakuna wajenzi.

No comments: