Jana nilijirekodi katika video nikisoma kwa sauti shairi la W. B. Yeats liitwalo "The Second Coming." Niliweka video hiyo katika mtandao wa Facebook, katika You Tube, na katika blogu hii. Niliiweka katika You Tube baada ya kushindwa kuiweka katika blogu moja kwa moja, na katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo, nilisoma mtandaoni kuwa kwa kuanzia kuiweka You Tube kunaweza kutatua tatizo. Ndivyo ilivyokuwa. Kutokea You Tube, nilifanya "embedding" kwenda kwenye blogu.
Napenda kwanza nikiri kuwa nimefurahishwa na jinsi usomaji wangu wa "The Second Coming" ulivyopokelewa na watu wa mataifa mbali mbali. Ni wazi kuwa wameguswa, nami nashukuru. Labda nitaandika zaidi kuhusu hilo. Lengo langu hapa ni kuongelea masuala ya kinadharia na kifalsafa juu ya usomaji wa shairi kwa sauti. Nilidokeza masuala haya katika ujumbe wa jana.
Kwanza, tutafakari dhana ya uandishi. Tuanzie na chimbuko lake, yaani utungaji. Utungaji wa shairi, au kazi yoyote ya sanaa, hufanyika mawazoni mwa mwandishi au msanii, katika hisia za mwandishi au msanii. Utungaji huu mawazoni au katika hisia ndio unaomwongoza mwandishi au msanii katika kuunda kazi ya sanaa tunayoiona, kama vile andiko au picha, au sanaa tunayoisikia, kama vile wimbo, muziki, au mapigo ya ngoma. Mpiga ngoma ana mtihani mkubwa kuliko wengine kwa kuwa uundaji na upigaji vinakuwa ni papo kwa papo, kwa kasi ya ajabu.
Hapa ninapenda kuongelea shairi. Shairi kama "The Second Coming" lilitungwa katika mawazo na hisia za Yeats, akaliandika ili tuweze kulisoma. Haikuwa lazima aliandike. Lingeweza kubaki mawazoni mwake na katika hisia zake. Angeweza kulighani kama wafanyavyo washairi wa jamii mbali mbali, kama ilivyokuwa jadi katika jamii zisizo na utamaduni wa maandishi.
Lakini Yeats aliamua kuliandika shairi lake, na hivyo kutuwezesha kulisoma. Kwa kuliandika na kulichapisha, ameliwezesha shairi lake kuenezwa popote duniani ambapo ki-Ingereza kinatumika kimaandishi. Hata pale ambapo ki-Ingereza hakitumiki, kuna uwezekano wa shairi hili kutafsiriwa kimaandishi, na tafsiri zikasomwa katika lugha mbali mbali.
Suala hili la tafsiri ni kubwa na tata, na siwezi kuliongelea sana. Lakini tukumbuke kwamba shairi kama "The Second Coming" likitafsiriwa katika ki-Swahili, ki-China, ki-Jerumani, ki-Zulu, na kadhalika, litakuwa si shairi lile lile aliloliandika Yeats. Lugha na tamaduni hazifanani kiasi cha kuwezesha utungo katika lugha moja kutafsirika kwa lugha nyingine. Mabadiliko hayakwepeki.
Nikirejea kwenye suala la usomaji wangu wa "The Second Coming," napenda kusema kwamba nilichofanya ni kutafsiri shairi lile. Ingawa nilisoma shairi katika lugha yake ya asili ya ki-Ingereza, nililisoma kwa sauti, vituo, na viashiria vingine vya mawazo na hisia zangu. Kwa maana hiyo, kwa usomaji wangu nilikuwa ninalitafsiri shairi.
Yeats mwenyewe kama angelisoma kwa sauti angelisoma kwa sauti, vituo na viashiria vingine vya hisia na mawazo yake. Wewe unayesoma makala hii ukilisoma shairi la Yeats kwa sauti utakuwa pia unalitafsiri kwa namna yako.
Roman Jakobson aliongelea vizuri dhana ya tafsiri katika makala yake, "On Lingustic Aspects of Translation," akabainisha aina tatu za tafsiri ambazo aliziita "interlingual," intralingual" na "intersemiotic." Niliwahi kugusia mchango wa Jakobson katika makala niliyoandika kuhusu nilivyotafisiri hadithi ya ki-Matengo. Bila shaka, kulisoma shairi kwa sauti kama nilivyofanya ni aina ya tafsiri ambayo Jakobson anaiita "intersemiotic."
Ninategemea kuwa wanafunzi, wafundishaji, na watafiti wa fasihi na nadharia ya fasihi watazitafakari dondoo nilizoweka hapa katika kuendeleza taaluma.
2 comments:
Nimefurahiswa na jinsi ulivyosoma shairi hili maana mimi ni mdhaifu sana wa kusoma na kusikiliza mtu asomapo mashairi. Ahsante
Dada Yasinta,
Nimefurahi kuwa umenitembelea hapa na nashukuru kwa ujumbe wako. Nilijitahidi kutoa hisia ninazokuwa nazo ninapolisoma shairi hili. Linanigusa sana. Imekuwa hivyo tangu wakati wa ujana wangu, nilipokuwa nasoma Mkwawa High School, Iringa, 1971-72. Nakutakia kila la heri.
Post a Comment