Wednesday, December 30, 2009

CHANGAMOTO: Insha za Jamii

Leo nimechapisha kitabu kipya. Kinaitwa CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Ni mkusanyiko wa makala mbali mbali nilizoandika mwaka 2009, juu ya masuala ya uchumi, siasa, jamii, na utamaduni yanayoihusu Tanzania na dunia kwa ujumla.

Hiki ni kitabu changu cha kwanza katika lugha ya ki-Swahili. Naamini kuwa uzoefu niliopata utanisaidia siku zijazo.

Kwa kuanzia, kitabu hiki kinapatikana mtandaoni, pamoja na vitabu vyangu vingine. Bofya hapa.

5 comments:

Unknown said...

Hongera na asante sana Prof. Mbele...haya ndio maendeleo!Tungeomba tafsiri ya Kiswahili pia. Karibu Radio on:
http://radio.adelaide.edu.au/

Mzee wa Changamoto said...

Hongera Profesa.
Ni maendeleo na mafanikio katika kuendeleza jitihada zako za kuielimisha jamii. Sasa sisi webngine tusioweza kuandika vitabu tuielimishe jamii kupenda kusoma la sivyo hatutawezesha kupatikana kwa yale yaliyomo vitabuni.
Heri ya Mwaka mpya

Mbele said...

Mzee wa Changamoto, shukrani kwa ujumbe wako. Nashukuru kwa jinsi ulivyo mwepesi kuwa bega kwa bega na wengine katika kuendeleza majukumu yanayotuhusu, iwe ni kuelimishana au kuhamasishana. Mungu akubariki, uendelee hivyo hivyo.

Mimi kama mwalimu wa miaka mingi, nikiwa nimeanza kufundisha Chuo Kikuu Dar mwaka 1976, napenda kukuhakishia kuwa uwezo wa kuandika vitabu unao sana. Moyo wa kuandika unao, na mawazo mengi ya manufaa unayo.

Halafu, mimi kama mtafiti wa tamaduni mbali mbali, nakuhakikishia kuwa kuna imani katika tamaduni nyingi za ki-Afrika kuwa jina analokuwa nalo mtu lina nguvu fulani na athari katika maisha yake. Kwa hivyo, jina lako la Mzee wa Changamoto tayari limeonyesha njia ya kufuata. Jina lina majukumu; usililazie damu.

Unavyoandika kwenye blogu unajipatia uzoefu na unanoa akili yako. Ni maandalizi mazuri kwa uandishi wa vitabu. Wewe bado kijana. Ni wakati mzuri wa kujipanga kwa majukumu kama hayo.

Kwa ndugu Karibu, nasema asante pia kwa ujumbe wako. Kauli yako kuhusu tafsiri ni muhimu. Kwa bahati nzuri, nimekuwa nikijishughulisha na tafsiri kwa miaka mingi.

Nilipokuwa kijana Chuo Kikuu Dar, nilianza kurekodi hadithi za ki-Matengo na kuzitafsiri katika ki-Ingereza. Nimechapisha kitabu cha baadhi ya tafsiri hizo.

Halafu, kwa miaka mingi nimekuwa nikitafsiri kwa ki-Ingereza tenzi za kale na tungo zingine za ki-Swahili. Nawazia kutafsiri baadhi ya maandishi ya Shaaban Robert.

Nikirudi kwenye hiki kitabu changu kipya, nami nimekuwa na wazo la kutafsiri insha hizi kwa ki-Ingereza. Insha mojawapo nilishaitafsiri, na unaweza kuisoma hapa.

Mzee wa Changamoto said...

Asante saana Profesa.
Kwa mara ya kwanza najihisi hamu ya kuanza kujinoa kuandika kitabu
ASANTE KWA HILI NA LITAKAA MAISHANI MWANGU MILELE.
Kifuatacho ni kufanyia kazi hisia hizi nzuri ambazo sikuwahi kuwa nazo. Naamini nitaweza
Baraka kwako na kwa kila mmoja mwenye mapenzi mema

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Umefanya vizuri kuzikusanya makala zako na kuziweka pamoja kisha kuzichapisha - hasa ukizingatia kwamba gazeti la Kwanza Jamii lenyewe ndio hivyo liko ICU hata kabla ya kumaliza mwaka. Nitajaribu kujipatia nakala ya kijitabu hicho.

Jenerali Ulimwengu pia aliwahi kuchapisha makala zake zote alizokuwa akiziandika wakati ule akiwa mhariri na mmiliki wa gazeti la Rai (Rai ya Jenerali Ulimwengu). Nilikinunua kitabu hicho na ukikisoma unaweza kuona na kupata picha kamili ya mawazo na falsafa yake pevu kupitia katika makala zake. Natumaini pia kwamba wasomaji wa kijitabu hiki ulichochapisha wataweza kupata nafasi ya kumfahamu hasa Profesa Mbele ni nani na mtazamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya jamii na maisha kwa ujumla ni upi. Wengi watafaidika.

Mzee wa Changamoto - akitaka kuandika kitabu hata leo hii anaweza. Bado tu hajaamua!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...