Thursday, May 17, 2012

Safari ya Afrika Kusini

Nimepata mwaliko kutoka mamlaka inayojumuisha vyama vya taaluma hapa Marekani, ACLS. Ni mwaliko wa kwenda kushiriki mkutano wa wanataaluma utakaofanyika katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, Afrika Kusini, Juni 15-17. Tutakutana katika kitengo cha utafiti kiitwacho WISER. Ni fursa ya wanataaluma mbali mbali kubadilishana mawazo na kutathmini hali na mwelekeo wa taaluma katika Afrika na ulimwenguni.

Sijawahi kukanyaga Afrika Kusini. Kwa hivi ninaingojea safari hii kwa hamu. Chuo Kikuu cha Witwatersrand ni maarufu. Kwa upande wangu, ninaposikia jina la Witwatersrand, au Johannesburg kwa ujumla, huwa nakumbuka mengi. Mbali ya harakati za ukombozi kama zile zilizoibuka Soweto, na mbali ya maandishi mbali mbali ambayo nimesoma na kufundisha katika masomo ya fasihi, jambo jingine muhimu kwangu ni kwamba baadhi ya vitabu vya Shaaban Robert vilichapishwa na Witwatersrand University Press. Hii ni kumbukumbu muhimu sana kwangu, na ningependa kuitembelea taasisi hiyo, ikiwezekana.

Kama kawaida, ninapokuwa katika mizunguko, nitachukua kamera yangu. Insh'Allah, wadau mtaona picha katika blogu hii.

3 comments:

batamwa said...

ahsante mheshimiwaProfesa Mbele ninakutakia safari njema na usikosekutujuza ya huko Inshaalah!

John Mwaipopo said...

bila shaka utatuwakilisha vema. safari njema

Mbele said...

Shukrani wadau, kwa mshikamano. Nitawawakilisha waBongo kwa kiwango cha juu kabisa. Nikitoka kule, natatinga Bongo kwa siku kadhaa. Nitapata fursa tele za kuwahadithia wadau wa baa kuhusu safari yangu, huku Kilimanjaro na Heineken za baridi zikitembea :-)

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...