Ukumbi wa Nkrumah ni moja ya sehemu muhimu sana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tangu nilipojiunga na Chuo hiki kama mwanafunzi, mwaka 1973, nilishuhudia umuhimu wa ukumbi huu wa mikutano.
Kwanza, napenda kusema kuwa ni jambo la heshima kuwa ukumbi huu ulipewa jina la Nkrumah, kiongozi maarufu wa harakati za ukombozi Afrika na duniani. Watu maarufu walihutubia katika ukumbi huu. Miaka niliyosoma na kufundisha pale, tuliwasikiliza watu kama Mwalimu Nyerere, William Tolbert, Gatsha Buthelezi, Robert Mugabe, Agostino Neto, Gora Ibrahim, Ali Mazrui, na Samir Amin.
Ukumbi huu ulikuwa ni sehemu ya mijadala baina ya watafiti na walimu maarufu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama vile Walter Rodney, Wadada Nabudere, Yash Tandon, Mahmoud Mamdani, na Issa Shivji.
Kila aliyesoma au kufundisha hapa chuoni atakuwa na kumbukumbu za mambo au matukio ya ukumbi wa Nkrumah. Nami nina kumbukumbu zinazonihusu moja kwa moja. Kwa mfano, nilipokuwa mhadhiri msaidizi, bado kijana, jumuia ya walimu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, UDASA, ilinichagua kuwemo kwenye jopo la wahadhiri ambalo lilipewa jukumu la kulumbana na Profesa Ali Mazrui. Tulipambana na Profesa Mazrui, ambaye alipenda kuja chuoni hapo kulumbana na wasomi, akihoji msimamo wa ki-Marxisti ambao ulikuwa unatawala hapa chuoni. Fursa hii niliyopewa na UDASA ilinifanya nijisikie vizuri sana.
Nakumbuka kuwa baada ya mjadala, Profesa Mazrui aliniita na tukaongea kwa zaidi ya saa nzima kuhusu masuali mbali mbali ya mwelekeo wa chuo, taaluma, siasa na kadhalika.
Tukio jingine ninalolikumbuka lilitokea kwenye mwaka 1986 mwishoni. Uliandaliwa mjadala kuhusu mwelekeo na athari za siasa za Marekani kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Niliteuliwa tena kuwa kwenye jopo ambamo alikuwepo Balozi wa Marekani, Bwana Don Petterson, na wahadhiri wengine kama wawili hivi. Nilikuwa nimerejea tu Tanzania kutoka Marekani, ambako nilisomea shahada ya uzamifu, 1980-86. Nilirejea na mawazo mengi na msisimko kuhusu suala hili la uhusiano baina ya Marekani na Tanzania. Ndio maana niliikaribisha kwa furaha fursa ya kuongelea mada hiyo mbele ya jumuia ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Kwa taarifa, Balozi Don Petterson ameandika kitabu kuhusu Sudan na kingine kiitwacho Revolution in Zanzibar: An American Cold War Tale, ambacho ninacho, na nakipendekeza kwa wadau wote.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
1 comment:
Kwa bahati mbaya mimi nilifika hapa wakati hali ya kiakademia ikiwa imeanza kufifia...
Naukumbuka ukumbi huu kama sehemu ambayo wanafunzi na DARUSO yetu tuliyokuwa tunakusanyikia ili kupanga mikakati ya migomo ili kuishinikiza serikali kutupatia/kutuongezea pesa za kujikimu.
Baada ya wanafunzi kuwa wengi sana ukumbi huu tukawa tunautumia kufanyia mitihani hasa katika yale madarasa makubwa yenye wanafunzi zaidi ya 100...
Post a Comment