Wednesday, July 25, 2012

Nimesifiwa kwa Kutumia Lugha Vizuri

Jana jioni nilikuwa kwenye baa moja karibu na Lion Hotel, Sinza, ambapo nilikutana na daktari mmoja rafiki yangu wa miaka mingi. Alikuwa na kaka yake, ambaye naye ni msomi. Kisha akaja rafiki yao mmoja, ambaye ni mfanyabiashara.

Baada ya takriban saa moja ya maongezi yetu, huyu mfanyabiashara alisema ameguswa na namna ninavyoongea ki-Swahili vizuri, ingawa nimekaa Marekani miaka mingi. Alisema ameguswa na jinsi ninavyoongea bila kutumia maneno ya ki-Ingereza. Daktari akachangia mada hii kwa kusema kuwa hata ninapoongea ki-Ingereza, huwa siigi namna wanavyoongea wa-Marekani.

Hapo waheshimiwa hao wakalalamika kuhusu watu ambao hata wakienda Marekani kwa miezi sita tu, wanakuja hapa na kujifanya hawawezi kuongea kama wa-Tanzania. Daktari aliigiza mikogo ya watu hao, tukawa tunacheka.

Nilifurahi kusifiwa hivyo. Nilichukua fursa hii kuwaeleza kuwa hata ninapokuwa kijijini kwangu watu wanashangaa jinsi ninavyoongea ki-Matengo vizuri kabisa, ingawa nimekaa Marekani miaka mingi. Tena nina uwezo wa kutumia maneno na misemo ya zamani, ambayo vijana wa leo hawaijui.

Mazungumzo hayo yalinikumbusha jinsi ninavyokerwa ninapowasikia watu wakichanganya lugha. Kwa mfano, wabunge wetu wengi wanafedhehesha kwa tabia yao ya kuchanganya ki-Swahili na ki-Ingereza wanapoongea Bungeni. Ninakerwa pia ninaposikiliza vipindi mbali mbali vya redio, ambamo watangazaji au waongeaji huchanganya ki-Swahili na ki-Ingereza.

Kila lugha ina heshima yake, na kuitumia ipasavyo ni namna ya kuienzi. Katika mazingira rasmi kama vile bungeni au redioni, ni sherti kutumia lugha rasmi kwa ufasaha. Kuiheshimu lugha yako ni kielelezo kizuri kujiheshimu, kwani lugha ni chombo kinachohifadhi utamaduni, na utambulisho wa kila binadamu au jamii. Ki-Swahili kinajitosheleza, sawa na lugha nyingine yoyote. Kutokitumia ipasavyo, kwa kukichanganya na ki-Ingereza, ni dalili mbaya.

Kwa kuzingatia yote hayo, ninajivunia kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, nilichoandika kwa kiSwahili. Nilikiandika ili kujipima uwezo wangu wa kutumia lugha hii, kujithibitishia kuwa ninaiheshimu. Hii ilitokana na ukweli kwamba maandishi yangu mengi yamekuwa katika ki-Ingereza, somo ninalofundisha katika Chuo cha St. Olaf. Kwa maoni zaidi kuhusu suala hili, soma makala yangu hii hapa, ambayo ilizua mjadala mzuri katika ukumbi wa Readable Blog.

2 comments:

Anonymous said...

nikweli prof wangu unaandika kiswahili safi na hata ukisoma mtiririko wake safi na inaingia kichwani mojakwamoja asante sana

Mbele said...

Anonymous, shukrani kwa ujumbe. Wale watu walikuwa wanaongelea jinsi ninavyoongea bila kuchanganya lugha.

Katika blogu hii, nimekuwa nikijiuliza kama nitumie ki-Swahili sanifu muda wote, au kama nitumie pia ki-Swahili cha mitaani. Bado ni mtihani kwangu.

Blogu hii ninaiona kama kijiwe, na mara moja moja natumia lugha ya kijiweni. Utaona, kwa mfano, natumia maneno kama "ulabu."

Nasema ni mtihani. Katika taaluma ya lugha tunaambiwa kuwa matumizi ya lugha ya mitaani ni chimbuko mojawapo la lugha rasmi. Ni kitendawili kabisa, lakini ndio tabia ya lugha. Sio kwamba maneno ya kijiweni yanaingia haraka katika lugha rasmi. Aghalabu inachukua muda, pengine muda mrefu.

Hatujui, labda maneno kama ulabu yatakuja kukubalika katika ki-Swahili sanifu.

Mfano wa juhudi ambayo nimefanya katika kutumia ki-Swahili sanifu bila kutetereka ni kitabu changu kiitwacho CHANGAMOTO. Hapa katika blogu, ingawa najitahidi, lakini naona bado nina duku duku, kama nilivyoelezea hapo juu.

Shukrani kwa kunipa moyo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...