Sunday, January 11, 2009

Matawi ya CCM Nje ya Nchi

Kwa miezi mingi sasa, kumekuwa na habari za kuanzishwa matawi ya CCM nje ya Tanzania. Naamini kila Mtanzania anaweza kuwa na maoni yake kuhusu jambo hili, na mimi ninayo pia, ingawa mimi ni Mtanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Niliishi nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza miaka ya 1980-86, nikiwa masomoni Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani. Nilipofika hapo, nilipokelewa vizuri na Watanzania waliokuwa wanasoma hapo. Walinipa kila msaada na ushauri niliohitaji ili kuzoea maisha yale mapya.

Jumuia hii ya Watanzania, ingawa haikuwa kubwa, ilikuwa kama familia huku ugenini. Wakati wa shida na raha tulijumuika. Na mara kwa mara tulikuwa tunakutana kwa maongezi na kustarehe pamoja. Kama mtu alishindwa kuja kwenye mikutano hii, ilikuwa ni sababu ya labda kuzidiwa na shughuli au kuwa safarini. Lakini hatukuwa na mtu aliyekuwa hatakiwi au aliyejiona hatakiwi au hahusiki katika mikutano hiyo.

Ningependelea Watanzania wanoishi nje waendeleze jadi hiyo. Mazingira ya huku nje ni tofauti na yale ya Tanzania. Mtu aliyeko Tanzania hana tatizo la upweke. Kuna ndugu, jamaa, marafiki na majirani muda wote. Mtanzania aliyeko Tanzania hana tatizo la kujikuta katika utamaduni mgeni na athari zake. Yuko kwake.

Watanzania walioko nje wanakutana na utamaduni usio wao, na hali hii ina athari za aina aina kwa kila mtu, na inaweza kuwa na madhara kisaikolojia. Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanahitaji kuwa karibu na Watanzania wenzao bila ubaguzi wa aina yoyote. Kuanzisha matawi ya CCM au chama kingine chochote cha siasa huku nje ni kuathiri hali ambayo tayari ni ngumu.

Nakumbuka tulivyoishi Wisconsin, halafu najiuliza: Je, ingekuwa ndio leo, tuko Wisconsin, halafu baadhi yetu waanzishe tawi la CCM, hali ya jumuia yetu ingekuwaje? Je, kama baadhi nao wangeanzisha tawi la chama kingine, au matawi ya vyama vingine, hali ya jumuia yetu huku ugenini ingekuwaje?

Vyama vya siasa Tanzania, kuanzia CCM, vimekuwa mstari wa mbele katika kuhujumu amani na mshikamano nchini, hasa wakati wa uchaguzi. Mifano iko wazi, kama vile yaliyotokea Zanzibar mwaka 2001, kama ilivyoelezwa hapa, Tarime mwaka 2008, na sehemu mbali mbali nyingine. Vurugu za Visiwani ziliendana na mauaji, uvunjwaji wa haki za binadamu, na uharibifu wa mali uliosababisha watu kukimbilia sehemu kama Kenya na hata Somalia, kama inavyoelezwa hapa na hapa. Ni ajabu sana, kwamba Watanzania wakimbilie Somalia. Haya yote ni matokeo ya ukosefu wa uongozi bora, uongozi wa busara na haki. Kama CCM, ambayo ilishika hatamu za uongozi nchini, ingekuwa na uongozi bora, wa busara na haki, matatizo au hayangekuwepo au yangetatuliwa bila ubabe na vurugu kama zile.

Wasi wasi wangu ni kuwa, yanapoanzishwa matawi ya CCM nje ya nchi, fujo zinazoletwa na vyama vya siasa huko Tanzania zitahamia pia nje. Utengano unaoimarika Tanzania, kutokana na siasa za vyama, nahisi utatokea pia huko nje. Na kama nilivyosema, afadhali Tanzania kuna fursa nyingi za mtu kujumuika na wengine, na hakuna upweke na matatizo ya kisaikolojia yanayohusiana na kuishi katika utamaduni wa kigeni.

Ni vema Watanzania wanaoishi nje waweke nguvu katika kuboresha mshikamano na utaifa. Watoto wa waTanzania na vijana wa kiTanzania wanaoishi nje wanahitaji kuelimishwa kuijua Tanzania, kujua historia, siasa, utamaduni na maisha ya Tanzania, na kulipenda Taifa lao. Katika mazingira ya huku nje, jukumu hili ni gumu sana. Hata waTanzania ambao ni watu wazima wanaoishi nchi za nje wana shida katika kudumisha uelewa wa nchi yao, kutokana na kuwa mbali. Wengi hawana fursa ya kwenda Tanzania mara kwa mara, na mengi yanawapitia mbali. Wangeweka kipaumbele katika kuifahamu Tanzania, ili waweze kuwafundisha pia watoto wao. Katika mazingira haya, kushughulika na matawi ya CCM ni kupoteza mwelekeo unaopasika.

Watoto, vijana, na watu wazima wanaoishi Tanzania hawana tatizo hilo, kwani wako katika mazingira muafaka ya kuifahamu nchi yao. Wanakomaa katika uTanzania, na hata wakiamua kujiunga na chama cha siasa, hakuna tatizo. Lakini je, ni sawa kwa vijana wa kiTanzania wanaoishi nje kujibidisha na CCM wakati suala la utaifa linayumba katika mazingira ya ugenini? Je, ni sahihi watoto wa kiTanzania wanaokulia nje, ambako tunashindwa kuwapa elimu kamili ya siasa ya kiTanzania, waanze maisha yao kwa kuona mfarakano baina ya waTanzania, badala ya kukuzwa katika fikra zinazoendana na ukweli kuwa Tanzania ni nchi inayozingatia sana utaifa?

Kuna wakati ziitokea taarifa za mpango wa kuanzisha tawi la CCM sehemu fulani hapa Marekani. Wazo hili lilizua hisia kali za upinzani. Sijui kama tawi hilo lilianzishwa, ila ilikuwa wazi kabisa kuwa wazo la kuanzisha tawi hilo hapa Marekani lingeleta mtafaruku miongoni mwa Watanzania. Taarifa mbali mbali zimeonyesha pia kuwa hata sehemu za Ulaya, kuanzishwa kwa matawi ya CCM kumeleta hisia kali ambazo hazichangii mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Hali hii ingetosha kuwafanya viongozi wa CCM Tanzania kutambua kuwa kuanzishwa matawi ya CCM huku nje kunaweza kuathiri mshikamano wa Watanzania na kuleta picha mbaya kuhusu Tanzania. Watanzania walioko nje wanapaswa kuwa na umoja na mshikamano kwa kila hali ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu, waweze kuwa mfano kwa Waafrika wengine tunaokutana nao huku nje, ambao wengi wao wanabaguana kwa msingi wa ukabila. Sisi Watanzania tulipokuwa Wisconsin, tukikutana pamoja na kuongea Kiswahili, baadhi ya Waafrika walikuwa wanatuuliza kama sisi ni kabila moja. Hawakuwa na namna nyingine ya kufahamu au kuelezea kitendo cha watu kuwa na mshikamano wa namna hii, nje ya dhana ya ukabila. Hayo ndio mazuri ya Tanzania na uTanzania, ambayo naamini yanatishiwa na vitendo vya kuanzishwa matawi ya CCM huku nje.

Hayo ndio mambo yanayonisumbua akilini ninaposoma taarifa za kufunguliwa kwa matawi ya CCM huku nje. Matawi ya CCM au chama kingine chochote yakifunguliwa nchini, mimi sioni tatizo. Ni sehemu ya haki na uhuru wa kila Mtanzania. Lakini picha inakuwa tofauti tunapozungumzia hali halisi ya jumuia za Watanzania wanaoishi nchi za nje. Nilitegemea viongozi wa CCM wangefanya uchambuzi wa kina wa suala hilo, lakini sijaona dalili zozote za kunipa matumaini.

5 comments:

Omohiri Kebhose said...

Mimi naona hakuna haja ya kuanzisha matawi ya vyama vya siasa nje ya nchi kwa sababu zifuatazo:

1. Kwanza Watatanzania waliyo nje ya nchi huwa hawapewi fursa ya kupiga kura, kwa hiyo hakuna sababu ya ya kuwa na matawi ambayo kazi yao kubwa ni kuendeleza chama.

2. Pili, matawi yataleta mgawanyiko kwa wale waliyo nje. Tunachohitaji umoja wa Kitanzania na siyo umoja wa kivyama.

3. Tawi linaunganisha watu waishiyo karibu kijiografia. Ukichukuwa wanaTZ Marekani wanaishi mbali kutoka wengine, dhana ya tawi ni ngumu kwa vile hawawezi kuwa kukutana. Je, mwanaCCM wa tawiu la Ubungo akija Marekani atakuwa katika matawi mawili kwa wakati mmoja?

4. Katika chaguzi fulani imeonyesha kuwa panapotokea matatizo katika kura mara nyingine hii inakuja na uhasama, "case in point" Tarime, Pemba, n.k. Uhasamu huu hugeuka kuwa vurumai na uchafuaji wa hali ya hewa. Kinaschotakiwa tunapokuwa nje ya nchi ni mshikamano na siyo mgawanyiko kwa vikundi vya vyama vya siasa, baadaye vikundi vya kimikoa, kiwilaya, kidini,na hatimaye kikabila. Tinataka kuwa Watanzania na siyo wanachadema, wanaCCM, waCUF waNCCR n.k. Hii itaua umoja wetu.

5. Katika hali ya maendeleo duniani sasa ni rahisi wanaCUF
wanaCCM,wanaCHADEMA, wanaNCCR kuendelea kuwa hai matawini kwao bila tatizo na kuondoa ulazima wa kuwa na na matawi!

6. Mimi ninadhani nia kubwa ya haya matawi ni kwa wachache kujipendekeza kwa serkali ya CCM, ili kama kuna cha kufaidi waitumie mwanya huu. Hii inaweza kuwa "economic venture in disguise". Ili kama kuna cha kufanyoika kwa wanaTZ kipitie tawi ili wajanja wawatumie waliyo nje kwa faida zao wenyewe.

7. Ubalozi ndiyo wenye jukumu la kulinda haki za Wataanzania, sasa haya matawi yatakuwa na kazi gani zaidi ya kutafuta mianya ya kuendeleza na kuficha UFISADI.

NO TO CCM BRANCHES ABROAD. BECAUSE THEY MIGHT BE DIVISIVE. NO TARIME OR PEMBA ABROAD.

Mbele said...

Ndugu Kebhose, shukrani kwa changamoto yako. Tuzidi kutafakari masuala haya, kwani ni muhimu kwa Taifa letu, leo na kesho.

Mzee wa Changamoto said...

Shukrani sana Prof kwa maelezo haya. Kama ulivyosema ni mtazamo wako na twasubiri wenye mitazamo tofauti nao watupe yao. Ndugu Omohiri nawe shukrani sana. Mmesema mengi lakini naomba niseme kuwa KABLA HATUJAJENGA CHAMA POPOTE PALE TUJENGE UTANZANIA. U-Tanzania utakaokubali UMOJA NA MSHIKAMANO na kujua kuwa ndani mwetu kuna heshima inayotuwezesha kukubali kutofautiana bila kutofautiana. Nikimaanisha kuweka tofauti kati ya mitazamo, itikadi na imani pembeni wakati unapostahili kufanya hivyo. Hili ndilo lililotushinda ambapo sasa Imani, Itikadi na hata makabila ama asili ya mtu vinaingia kwenye maongezi na maamuzi mbalimbali na kujikuta yakiibua utengano na madaraja.
Kabla hatujawa na umoja wa kuyaepusha haya sidhani kama tunahitaji vyama huku.
Lakini pia kwanini Jumuiya zife nasi tuanzishe matawi ya vyama? Kama jumuiya za waTanzania (ambazo sasa zaonekana kufanya kazi nyakati za majira ya joto na kwenye misiba) zinatushinda kuziendeleza kwa kutokuwa na umoja na mshikamano, kwanini tuendekeze na kuendeleza u-vyama? Na huu ni mtazamo wangu kwa namna nionavyo tatizo, yawezekana nilionavyo ndilo tatizo.
Asante

Simon Kitururu said...

Bado najiuliza kwa nini CCM iwe na matawi nje ya NCHI wakati naamini demokrasia ya Tanzania ili ikomae inahitaji vyama vya upinzani vijijini Tanzania !:-(

Ni ujanja kuwa mwana CCM sasa hivi, lakini kwa astukiaye kitokeacho kwa CHAMA cha Zuma na Mbeki South Afrika na ni opotyunisti, ajiandae kukosea kama anafikiria ujanja ni kuwagawa hata wabongo Ughaibuni.

malkiory said...

Kwa heshima na taadhima, napenda kuwapongeza wanablog KEBHOSE, MBELE, MZEE WA CHANGAMOTO NA KITURURU kwa mchango wenu ambao kwa mtizamo wangu ni wa hali ya juu na wenye kuonesha ukomavu wa kimawazo, kimtizamo na busara.

Watanzania wenye uchungu na nchi yao hawapawaswi kuongelea habari ya kuanzisha matawi ya CCM ughaibuni hasa kwa kuzingatia kuwa serikali ya CCM ndiyo imeifanya taifa letu kuwa kati ya mataifa masikini na duni kuliko zote duniani.

Tunachohitaji sasa hivi ni kuongelea jinsi ya kuikomboa taifa kwenye janga la umasikini ambao kwa namna moja au nyingine umechangiwa na ufisadi na utawala mbovu wa serikali ya CCM.

Badala ya kufungua matawi ya CCM ughaibuni tungeweza kujadili mambo muhimu kama vile ufisadi, ubinafsi, ukiritimba ambao umekithiri ndani ya taasisi mbali mbali za serikali.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...