Friday, December 10, 2010

Laiti Ningekuwa Kama Hemingway

Laiti ningekuwa kama Hemingway, mwandishi maarufu sana duniani. Ningeandika kuhusu nchi yangu na watu wake kwa umakini, ubunifu, na ukweli wa kumgusa kila msomaji. Ningeandika kuhusu maziwa, mito, milima na mabonde. Ningeandika kuhusu fukwe, nyanda na visiwa. Ningeandika kuhusu miji na vijiji, mitaa na vitongoji.

Nimetamka hayo, na nimeanza kufanya mazoezi. Lakini bado njia ni ndefu mbele yangu.

Laiti ningekuwa kama Hemingway, aliyeangalia mazingira, matukio, na tabia za wanadamu kwa macho na akili yote, aliyejawa nidhamu ya kutumia lugha, akiangalia kila neno, tena na tena, akibadili na kusahihisha tena na tena, akitafuta namna ya kuandika sentensi sahihi yenye ukweli mtupu.

Laiti ningekuwa kama Hemingway, aliyetufundisha kuwa kazi ya mwandishi ni kujitoa mhanga ili nafsi yake yote ibakie katika kitabu tu, asibakishe hata chembe nje ya kitabu. Kila kitabu kiwe ni mauti ya mwandishi, vinginevyo kitabu hiki ni mzaha na udanganyifu. Je, nitayaweza hayo?

Hemingway aliandika kuhusu nchi mbali mbali alizozitembelea, ikiwemo nchi yangu. Nimekutana na watu wa nchi mbali mbali wanaomshukuru Hemingway kwa hilo. Tutalipaje fadhila, isipokuwa kwa kujijengea nidhamu ya kuyaangalia mazingira na maisha, nidhamu ya kuiheshimu lugha na sentensi, tuweze nasi kuandika mambo ya thamani? Tutalipaje fadhila kama hatuna ushujaa wa kuwa wakweli kama Hemingway?

22 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nimeipenda hii mada, Na ninaamini Pro.Mbele wala haupo mbali kuwa kama Hemingway yaani jinsi ulivyoandika hii mada yaani mtu unasoma na mwisho unaona ooh nimemaliza yaaani utamu sana kwa hiyo nakuomba endelea tu na ufanyavyo wewe ni Hemingway wetu.

Mbele said...

Dada Yasinta, nimetabasamu kusoma ujumbe wako. Nitajitahidi niwe Hemingway kama unavyoniombea :-)

Sasa basi safari ijayo nitakapokuwa Songea, nitajichimbia mzigoni niandike kuhusu sehemu zile, kuanzia Matogoro, Bombambili, Mfaranyaki hadi Ruhuwiko :-)

Simon Kitururu said...

Mie naamini Prof . unaweza!Na ikibidi kazi uliyoianza ukistaafu ndio ipate chachu zaidi ili hii kitu itimie.

Ila Hemmingway nasikia alikuwa MLEVI maana kila nipitiapo wamkumbukao mpaka CUBA .....{wasomao vitabu na WASIOSOMA].....- ni wapi alikuwa anakaa kwenye BAA na alikuwa anakunywa KIKILEVI nini.:-(

Mbele said...

Ndugu Kitururu, ni kweli Hemingway alikuwa anapiga ulabu sio kawaida, iwe ni asubuhi au mchana au jioni.

Lakini, cha ajabu ni kuwa akili yake ilikuwa timamu kama nilivyodokeza. Hata mkipiga naye tungi sana, na nyinyi wengine mkaanza kutambaa na kisha kutumbukia kwenye mitaro, Hemingway alikuwa mzima, anaendelea na tungi. Hii ni ajabu mojawapo.

Lakini, pamoja na ulabu, Hemingway alikuwa na nidhamu ya ajabu ya kuandika. Alikuwa hafanyi mchezo kabisa na hii kazi. Na kazi alizoandika ni nyingi, kuanzia riwaya, hadithi fupi, barua, insha, na hata mashairi.

Nimefanya utafiti kuhusu mwandishi huyu kwa miaka yapata kumi sasa, na ananivutia kwa namna ambayo sitaweza kueleza, hata kama ningetaka. Maandishi yake yana ladha, hisia, na mtazamo wa pekee sana. Mfano mmoja unaothibitisha hayo ni riwaya yake ya "The Old Man and the Sea." Alipata tuzo ya Nobel mwaka 1954.

Kitu kimoja kinachonisikitisha ni kuwa ingawa aliandika kuhusu nchi yetu, waTanzania wenyewe hawana habari, maana hawagusi vitabu. Ingekuwa nchi nyingine, watu wangetumia maandishi hayo kujitangaza. Lakini Bongo hatuna utamaduni huo.

Nimejaribu sana kuwazindua wanaohusika na sekta ya utalii, lakini hakuna mwamko nilioona wa kufuatilia. Hawashtuki.

Simon Kitururu said...

Prof. Mbele nakuelewa! halafu sababu ya kudokezea kuwa alikuwa mtu wa ULABU ilikuwa ni kwamba nimestukia kila sehemu wanavyostukia jinsi ya kumtumia huyu NGULI. Baa karibu Ulaya nzima mpaka CUBA hujaribu kumtumia. Huku ulaya ndio kabisa mpaka hawakwepi na kuita BAA kabisa Hemmingway na ukiingia mapambo ni vile wahisivyo alikuwa anatumia. Na nikweli hilo huvutia watu. Sasa jiulize je kitu alichoandikaia kama nchi ya Tanzania tungeshindwa hata kuwasiliana na yeyote mhusika ambaye ana hati miliki ya alivyo simulia Tanzania na kushindwa kumhusisha na Tanzania wakati tunajua kwa hata UTALII ingelipa?


Ila nimekumbuka mambo ya Tanzania sio ya utaifa .:-(
Na hata ukimtumia MUNGU bado utakuta itakuwa sio kweli kwa manufaa ya WATANZANIA wote ingawa kitumikavyo ni MUNGU asifiavyo TANZANIA.


Nje ya topiki:
Samahani Prof. Mbele ,...
...ila naamini unauwezo wa kuHEMINGWAY ingawa labda wajukuu wako ndio watastukia ka kipimo ni WALIO WENGI.

Na samahani tena kwa kuwa saa nyingine lugha yangu hata hapa nikikomenti sio safi sana ila ndio nilivyo kikauli!:-(Ila heshima YANGU KWAKO ni bonge la Kilo milioni.

Simon Kitururu said...

Na ukweli ni kwamba Profesa: Walevi wetu Tanzania walio BAA wako baa KULEWA na ukimuulizia MLEVI hata msomi hapo baa alijifunza nini,...
...anaweza kukuambia kikubwa ni kwamba aliopoa DEMU na kwanza demu mwenyewe alistukia mpaka kuwa aendeshacho ni BOMBA la gari . Na hapa siongelaei WANASIASA ambao wengi au baadhi ndio walitaja mpaka kuwa wanataka kuitwa WAHESHIMIWA hata kabla hawajafanya CHAKUHESHIMIWA.:-(

Nikigusia nukuu hiii:``...
Bongo hatujali kama nyumba fulani aliishi Hemingway au Shaaban Robert. Mafisadi wanaivunjilia mbali na kujenga kikwangua anga. Na raia nao wanashangilia hivi vikwangua anga, kwamba ni maendeleo. ´´.mwisho wa nukuu.

Hapo Prof.J Mbele nahisi umeenda mbele kwa kuwa nahisi itahitaji semina kunyambulisha hicho kitu.
Lakini Prof.Mbele si unajua kwa wastani VIONGOZI wa TANZANIA wanaongoza kwa kwenda semina na kozi za uongozi kwa ``avereji´´mara 300 kwa mwaka kwa kila aitwaye kiongozi ingawa uongozi wao ni swa la kujadili wanaongoza nini?

Mbele said...

Ndugu Kitururu, unayosema ni kweli kabisa. Huku ughaibuni, kuanzia Urusi (ambako sijapita), Ulaya, Marekani, na kadhalika, wenzetu ni wepesi sana kutumia fursa za aina hiyo. Wanahifadhi hizi sehemu na kuzitumia.

Bongo hatujali kama nyumba fulani aliishi Hemingway au Shaaban Robert. Mafisadi wanaivunjilia mbali na kujenga kikwangua anga. Na raia nao wanashangilia hivi vikwangua anga, kwamba ni maendeleo.

Ninatamani niwe mwandishi bora. Itabidi kujifunza upya maana ya kila neno na matumizi yake katika sentensi, kiasi kwamba kila neno ninaloandika liwe na umuhimu hapo lilipo, na liwe ni neno hilo tu, si jingine. Kipimo itabidi kiwe hao hao akina Hemingway na akina Shakespeare kwa upande wa ki-Ingereza, au akina Mgeni bin Faqihi, mtunzi wa "Utendi wa Rasi l'Ghuli," kwa upande wa ki-Swahili. Hii itakuwa ni nidhamu ya kuumiza kichwa, lakini ndio inayohitajika.

Mbele said...

Samahani ndugu Kitururu, nilibandika ujumbe wangu, halafu nikauondoa, kurekebisha kitu kidogo, kumbe wakati huo ulishausoma. Nilivyokuja kuubandika tena, inakuwa dakika zinaonekana kama uliandika kabla yangu.

Nchi yetu ndio hiyo. Semina elekezi haziishi, lakini hatuna mwelekeo :-)

Simon Kitururu said...

:-) Samahani Prof. Unajua nikiingiaga hapa siondoki mapema na nakuwa ``sensitivu´´ na chochote kinachoingia hapa.

Ila haki ya nani nikiingia hapa siku hizi huwa naanza na ``atiko za mwanzo´´ ulizo andika hapa ingawa nakitekenelojia naweka usensitivu nistukie yeyote anaye chezea unacho andika siku hizi.

Ndio,...
...
niko BAA,...

...ila peke yangu kisa nina MOOD ya kusoma na sio kuongea!:-(

Emmanuel said...

Mungu aibariki hilo unalolipenda na uliloanza. Penye nia pana njia na Mungu ni mwema anamjalia kila mmoja kadiri anavyojituma.
Aksante pia kwa kuijali nchi yetu hii
Sulle

Martin Walsh said...

na Kiswahili chake je?!
http://notesandrecords.blogspot.com/2010/10/bad-swahili-and-pidgin-swahili-in.html

Mbele said...

Shukrani kwa suali lako, ndugu Walsh. Kwanza, nakupongeza kwa blogu yako ambayo niliigundua siku kadhaa zilizopita, nikasoma mambo kadhaa, pamoja na taarifa yako kuhusu Hemingway. Unafanya kazi nzuri sana.

Kuhusu ki-Swahili cha Hemingway, ni kweli kuwa ni cha matatizo sana. Tangu niliposoma "Green Hills of Africa," kwa mara ya kwanza, miaka mingi iliyopita, nilitambua hilo.

Katika kutafakari suala hili la ki-Swahili cha Hemingway, nimeona kuwa kuna mambo kadhaa ya msingi.

Kwanza, Hemingway hakukaa sana hapa Afrika Mashariki. Alikaa miezi kadhaa wakati wa safari yake ya kwanza, yaani 1933-34 na tena miezi kadhaa katika safari yake ya pili, yaani 1953-54.

Vile vile, alikuwa Kenya zaidi, na wazungu wa kule na pia watu wa makabila ya kule, kama vile Wakamba na Wamasai. Kiswahili alichokuwa anakisikia ni cha watu wa kule.

Lakini, kuna suala pana zaidi. Hemingway alikuwa mtu aliyezipenda na kuziheshimu tamaduni za watu popote alipoishi, nje ya nchi yake, iwe ni Ufaransa, Uhispania, Cuba, au Afrika Mashariki. Aliipenda sana Afrika, tangu utoto wake, na alisema tena na tena kuwa hapo Afrika, roho yake ilitulia na kuwa na furaha muda wote.

Sasa basi, kwa kuzingatia hayo yote, nimekuwa tayari kusamehe ki-Swahili chake. Alijitahidi kwa muda na mazingira aliyokuwa nayo angalau kujua hicho kidogo.

Hili ni fundisho kwetu wote, juu ya kujifunza kuhusu tamaduni mbali mbali, na lugha, hata kama hatutaweza kujua kila kitu. Hemingway ametufundisha kuheshimu tamaduni za wengine.

Nina imani kuwa, kama angepata muda zaidi wa kuishi Afrika Mashariki, Hemingway angejiongezea ufahamu wake wa ki-Swahili. Alikuwa ni mpenda lugha, na alikuwa mtu wa kutafuta maarifa muda wote. Alikuwa anatumia si hiki ki-Swahili tu, bali lugha zingine pia, kama vile ki-Faransa na ki-Hispania.

Huu ndio mtazamo wangu kuhusu ki-Swahili kibovu cha Hemingway.

Martin Walsh said...

Nakushukuru sana Prof. kwa maoni yako ya busara. Ni kweli "Papa" Hemingway alijitahidi kujifunza lugha na kuheshimu tamaduni mbalimbali. Nimegundua kwamba baada ya safari yake ya kwanza ya kwenda Afrika Mashariki (na baada ya kuanidika 'Green Hills of Africa') aliendelea kukusanya kamusi na vitabu vingine vya Kiswahili. Matunda yake yalionekana wakati wa safari ya pili, hasa alipoandika 'Under Kilimanjaro', kitabu kilichohaririwa na kuchapishwa hivi karibuni. Hata hivyo anajitambua: "Miss Mary said I could not write one correct sentence in Swahili nor speak one either and I agreed with her very sadly that this was true", uk.204).

Pamoja na hayo nakupongeza kwa kazi zako nzuri: endelea kusonga blogu yako Mbele!!

Samehani kwa Kiswahili changu cha kikoloni... :~}

Mbele said...

Mzee Walsh, asante tena. Ndio hivyo tunavyosema, Hemingway alikuwa na kiu sana ya kusoma, na alikuwa ananunua vitabu kila alikoenda.

Kitabu cha "Under Kilimanjaro" nimekisoma. Taarifa zake, kabla hakijachapishwa, zinanisikitisha, kwa vile Hemingway alijiua wakati hajausahihisha mswada huu kwa kiwango alichozoea. Mswada alikuwa ameuhifadhi Cuba. Sehemu kubwa ya mswada huu ilichapishwa kama kitabu, "True at First Light," na mtoto wake Patrick Hemingway.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

sio shakespares?

Mbele said...

Ndugu Kamala

Kwa uandishi wa ki-Ingereza kwa ujumla, Shakespeare ndiye maarufu kuliko wote waliowahi kuishi. Aliandika tamthilia na mashairi.

Lakini kwa uandishi ninaoongelea, wa kuelezea mazingira ya mahali: mito, milima, mabonde, misitu, mapori, watu na wanyama, Hemingway yuko mstari wa mbele kabisa katika uandishi wake wa riwaya, hadithi fupi, na insha.

Kuna tofauti za msingi baina ya Shakespeare na Hemingway, ikiwamo tofauti ya aina ya ki-Ingereza walichoandika. Cha Shakespeare ni cha zamani, miaka mia tano iliyopita, wakati cha Hemingway ni cha siku zetu hizi.

Tofauti nyingine ni kuwa Hemingway aliandika sana kuhusu uandishi. Shakespeare naye alisema mambo kadhaa kuhusu suala hilo, lakini sio sana kama Hemingway. Ukisoma riwaya za Hemingway, kama vile "Green Hills of Africa," utaona fikra zake nyingi kuhusu kazi ya uandishi. Katika barua zake nyingi, ambazo nyingi zimechapishwa, aliandika kuhusu uandishi.

Ndio maana nimemtaja Hemingway. Kwenye blogu yangu ya ki-Ingereza ninamtaja pia. Kwa mfano, soma hapa.

emuthree said...

Kwangu mimi mkuu Mbele, nakuona upo sambamba na huyu jamaa, sijui katika tabia ya ulabu, lakini kiutafiti na unavyofuatilia mambo haya, upo SAMBAMBA, na kwa vile tu wenzetu wameweza kuwaenzi watu wao, waandishi na watu wa fani tofautitofauti na kuwaweka kwenye vitabu vya historia.
Napenda kupiga hodi sana hapa kwako kwani huwa napata hivi viti adimu, nashukuru sana, na mungu atakuzidisshia, nina imani hiyo kuwa wewe ni kama yeye, hilo liweke akilini mwako!

Mbele said...

Shukrani emu-three kwa kufuatilia kijiwe changu hiki. Kwa vile unasema unafaidika na yaliyomo, naona niseme kuwa unaweza kufaidi zaidi ukisoma vitabu vyangu, ambavyo vinapatikana hapa Dar, simu namba 0754 888 647 au 0717 413 073.

Karibu sana kwenye kibaraza hiki. Nafurahi kuwa tuko pamoja.

emuthree said...

Nashukuru sana kwa kunipa mawasiliano hayo, nitayahifadhi kwenye simu yangu, kwani hata mimi ni mpenzi wa kuandika hasa visa katika mfumo wa `tamithilya' karibu sana kijiweni kwangu uniunge mkono

Mbele said...

Dada emu-three, shukrani kwa ujumbe wako. Usiwe na wasi wasi; mimi ni mdau wa kutupwa wa blogu yako, tangu zamani :-)

Simon Kitururu said...

@Prof.Mbele: Nahisi M3 ni KAKA lakini , ingawa sijui jina lake la kikweli.:-)

Mbele said...

Ndugu Kitururu,

Duh, hii mbona kali :-(

Nilikuwa nasoma "profile" siku zote nikaona miram nikidhania ni miriam!

Hebu tungoje atufafanulie. Ila uwongo mbaya, makubwa haya :-(

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...