Friday, April 10, 2009

Watanzania Wanaoishi Bloguni

Hivi karibuni nilianzisha mada hii hapa kuhusu Watanzania wanaoishi baa. Katika mjadala, ndugu Bwaya alishauri kuwa tunapozungumia suala hilo, tukumbuke pia kuna Watanzania wanaoishi vijiweni.

Nafikiri hili ni wazo muafaka. Na wazo hilo limenifanya nifikirie hizi blogu zetu. Tunaweza kuzichukulia blogu zetu kuwa ni vijiwe. Zinatoa huduma ile ile kama vijiwe. Ndugu Kamala ni mkweli, maana blogu yake ameiita kijiwe. Tuko Watanzania wengi ambao tunaishi bloguni, kama vile wenzetu wanavyoishi baa au vijiweni.

Jumuia ya wanablogu inaongezeka. Tumeshaanza kuwa kama kabila. Tunajitambua, na tunao utamaduni wetu, kama vile Wapogoro, Wakwere, au Wasukuma wanavyojitambua na tamaduni zao.

Tofauti na kijiwe asilia, ambacho labda kiko Buguruni au Magomeni, na ambacho wateja wake kwa kawaida ni wakaaji wa hapo hapo mtaani, hivi vijiwe vya mtandaoni, yaani blogu, vinajumuisha wateja kutoka pande zote za dunia. Hii ni ajabu, kwamba mtu unaweza kuanzisha kijiwe chako, yaani blogu, popote ulipo na kompyuta yako, halafu wateja wa kijiwe chako wakawa wanatoka pande zote za dunia.

Tofauti na vijiwe asilia, ambavyo ukitaka kuhudhuria, ni lazima utoke nyumbani mwako na kwenda vilipo, mtu anahudhuria vijiwe vya mtandaoni bila kutoka nyumbani au ofisini. Anakaa hapo hapo na kutembelea vijiwe vingi apendavyo. Hii ndio mila na desturi ya hili kabila jipya linalojumuisha wanablogu na wateja wao. Wanapita kwenye blogu nyingi na kusikiliza yanayozunguzwa huko na kuchangia. Mimi mwenyewe natumia muda mwingi kuzungukia hivi vijiwe vya mtandaoni. Nimeshakuwa mmoja wa Watanzania wanaoishi bloguni.

10 comments:

Bennet said...

Hii ya leo kali

Kwa kweli hizi blog zetu ni kama vijiwe maana tunashinda humo mida ambayo hatuna la kufanya na kila mtu anaongea lake kutokana na upeo wake au mawazo yake.

Uzuri wa hivi vijiwe vyetu ni kwamba tunapata habari mbali mbali, na pia tunaburudika, halafu tunaelimika kutokana na mafunzo mbali mbali, na wakati mwingine tunapata marafiki muhimu katika vijiwe vyetu.

vijiwe vya mitaani kama kwetu ilala mara nyingi huwa hamna jambo la maana sana linaloongelewa sana sana ni story, ubishani wa michezo, siasa, vichekesho na umbea kidogo.

Mbele said...

Blogger Mbele said...

Ndugu Bennet, huku ughaibuni, tayari vijiwe hivi vinafanyiwa utafiti wa kitaalam na watu wa taaluma mbali mbali. Tasnifu za shahada za juu zinaandikwa, na makala zinachapishwa, na pia vitabu. Kitabu kimoja ambacho nilikinunua mwaka jana, na kinavuma sana, ni The Psychology of the Internet, kilichotungwa na Dr. Patricia Wallace.

Utafiti kuhusu vijiwe hivi unatuelimisha mengi kuhusu hali na hulka ya sisi binadamu: kijamii, kisaikolojia, na kadhalika.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

wewe achana na vijiwe hivi. bila kuvitembelea kwa siku moja naijihisi mapungufu. ni vijiwe vilivyotulia na vina mengi sana. nakiri kuishi na kuendelea kushi vijiweni mapaka unamilifu wa dahali. Amina

Simon Kitururu said...

Tatizo ni unaweza kulia ukitafuta kujua ni asilimia ngapi ya Watanzania wangapi wamewahi kugusa kompyuta hata kabla hujauliza Internet ni nini!


Mwaka jana tu niliwahi kukutana na mwalimu wa chuo kikuu cha Dar na alikuwa hajui kuna kitu kinaitwa blog:-(

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

wakati hayo yanatendeka, mwana simon anaishi bloguni.

je hilo ni daraja?

Simon Kitururu said...

@Kamala: Hata sijui!:-(

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

siku inakuja hata usipotafuta kujua utajikuta ukijua tu

Simon Kitururu said...

@Kamala: Sina uhakika maana kuna mengine kama vile MBINGUNI unaweza ufe hujayajua. Na ukifa labda ukastukia hakuna mbinguni ila ni zamu yako kuzaliwa upya kama mjusi.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

hayo ya mbinguni na kuzaliwa mjusi iabidi uyaeleza kinagaubaga mzee.

ukikana kuishi bluguni wakati mpaka sasa uko namimi niishiye bloguni basi umepotea kama padri anayejisema kwenda mbinguni mbele ya waumini wakati anafanya yale awazuiayo waumini kufanya.

labda unaogopa gharama za kukubali au kukataa maana zina nongwa yake pia.

sio lazima ukbali kwani swali nimeliuliza nikiwa na jibu mkononi

Simon Kitururu said...

@Kamala:Sina Uhakika:-(

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...