
Kwa vile kitabu cha aina hiyo niliyowazia hakikuwepo, niliamua kukiandika mimi mwenyewe. Niliona kuwa hakuna maana kukaa tu na kulalamika. Tatizo haliondoki kwa malalamiko, bali kwa vitendo.
Kitabu nilichoandika kinaitwa Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Napenda kuwashukuru wasomaji waliotoa maoni yao kuhusu kitabu hiki kwenye kumbi mbali mbali. Mmoja wa hao ni Dada Sophie ambaye ameandika maoni yake kwenye blogu mbali mbali.
Miaka ya karibuni, nimefahamiana na kikundi cha vijana wa Mto wa Mbu, Tanzania, wanaojishulisha na utalii. Hao vijana wananitia moyo kwa jinsi wanavyotambua umuhimu wa elimu, katika kufanikisha shughuli na miradi mbali mbali, na katika maisha kwa ujumla. Unaweza kusoma baadhi ya maelezo yao hapa na unaweza kusoma maelezo yangu hapa.
Sote tungefaidika iwapo wengine wangejitokeza na kuandika mawazo yao. Tunahitaji maandishi kuhusu tamaduni mbali mbali. Mimi niliandika kuhusu Wamarekani na Waswahili kwa vile hao ndio ninaowafahamu. Naendelea kuandika, hasa makala fupi fupi magazetini na katika majarida, kuhusu masuala hayo hayo. Panapo majaliwa, nitatoa kitabu kingine. Lengo ni kumsaidia Mmarekani na Mswahili kuepuka migongano isiyo ya lazima.
Kwa yeyote atakayependa, kitabu hiki na vingine vinapatikana Dar es Salaam, simu namba 0754 888 647 au 0717 413 073.
1 comment:
Asante saana Profesa. Nakumbuka kuna aliyesema kuwa TUMEBARIKIWA kuwa na mtu mwenye uwezo wa kushiriki BUSARA zake nasi (ambao kwa mtazamo wa wengine hatustahili kuzipata) na naamini kwa watakaokipata na kukisoma wataweza kuunganishwa na kuelimika na pengine kukomboka (ukombozi wa kiakili) katika kile kidhaniwacho na kilichopo.
Baraka kwako
Post a Comment