Friday, April 3, 2009
Santa Claus Anafanya nini Tanzania?
Miaka hii, Santa Claus anaonekana Dar es Salaam na sehemu zingine Tanzania. Zamani, tukiwa wadogo, hatukuwahi kumwona babu huyu, labda vitabuni. Siku hizi wakati wa Krismasi, anaonekana, hasa kwenye maduka makubwa mijini.
Santa Claus ametokea Ulaya. Wakati wa Krismasi, huko Ulaya na Marekani ni majira ya baridi kali, na theluji hutanda kila mahali. Wenyeji wa huko huvaa mavazi mazito kutokana na hali hiyo. Santa Claus naye anavaa hivyo, kutokana na hiyo baridi kali.
Sijui hao waliomleta Santa Claus Tanzania walisahau kuwa Tanzania hakuna baridi ya aina hiyo? Nashangaa kumwona Santa Claus sehemu kama Dar es Salaam, kwenye joto sana majira ya Krismasi. Au labda ndio maendeleo yenyewe?
(Foto kutoka PDPhoto.org)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
10 comments:
Tunaiga kila kitu na hili ni tatizo kubwa, tunaweka miti ya mikrismas na tunaweka theluji bandia ya kupulizia.
Tunaamua na kumweka baba krismas na nguo zake za kwenye baridi kali, kama ni kupata picha halisi labda wangemvisha nguo laini za pamba zenye rangi ile ile maana wakati wa hii sikukuu ya noeli sehemu kama dsm joto ni kali sana.
MFANO mbaya ni sikukuu ya wajinga tulivyo iiga, maana unaweza hata kuletewa habari za msiba na mtu unayemwamini sana na ni mtu mzima na heshima zake, baadae anakwambia APRIL FOOLS DAY
Ni kweli Santa Claus anafanya nini Tanzania. Tena hata jina lenyewe halifai kabisa. Nashangaa mambo mengine tunayoiga ni kinyume kabisa na tamaduni zetu.
Sio baada ya muda pia tutaiga kula mayai wakati wa PASAKA
Kuiga huku pasipokujua wenzetu wanafanya vile kwa misingi gani na kwa nini ni tatizo tulilnalo sana waafrika hususani watanzania.
Mavazi kama suti pengine ni ya kuvaliwa wakati fulani tu lakini huku kwetu ni kama fasheni. Tunashuhudia nguo wanazovaa kina dada, zenye kuchora maumbo yao, wanaiga tu pasipo kujua wale wenzetu wanavaa hivyo kwa sababu gani, na pia bila kujali misingi ya tamaduni tulizokulia.
Labda tuna Santa Klaus kwasababu anahitajika.
Asingehitajika unafikiri angehitajika?
Elimu inazidi kufifia Tanzania, na badala yake unashamiri ukoloni mamboleo na huu ukasuku tunaoongelea. Njia za kujikwamua ziko, kama vile kusoma na kutafakari yaliyoandikwa katika vitabu muhimu. Mifano ni Song of Lawino kilichoandikwa na Okot p'Bitek na Black Skin White Masks kilichotungwa na Frantz Fanon. Hivi ni baadhi ya vitabu muhimu sana katika ukombozi wa fikra zilizoathiriwa na ukoloni na ukoloni mambo leo.
mbona mengine hayawashangazi? mbona padri anavaa gauni hamshangai? mbona makanisa yote yanatokea nje ya nchi, hamshangai?
hili mbona dogo la kushangaza? mbona papa anaaagiza waumini wafanye nini wanafanya?
Kamala, huwa napendezwa sana na maoni yako na kila nikitembelea blogu siku hizi ni lazima kwanza nitafute kwenye comments nione umesema nini. Unachangamsha!
Ama kweli!! Nilipomaliza kusoma nilikuwa na mawazo kadhaa kuyaweka kwenye maoni, kisha nikaanza kupitia maoni na kukutana na ya Kakangu Kamala. Nimetafakari kwa kina aliyouliza nimeishia kuhitaji muda zaidi wa kujua "kwaninis" zake.
Naamini ntapata jibu punde kisha nirejee.
Amani kwenu
Ndugu Kamala, napenda kufuatilia suali lako kuhusu mapadri kuvaa gauni. Utaratibu uliopo ni kuwa wanawake ndio wanavaa gauni, na wanaume wanavaa suruali au kaptura. Lakini, tunapaswa kwenda mbali zaidi katika tafakari yetu.
Huu utaratibu wa wanawake kuvaa gauni au sketi na wanaume kuvaa suruali au kaptura hatukutunga sisi, bali tumebambikizwa na wazungu. Hili tayari ni suala ambalo linapaswa kutushangaza. Kwa nini wanaume tunavaa suruali au kaptura na wanawake wanavaa gauni au sketi? Kuna mantiki gani katika kuvaa mavazi haya? Mtu anaweza kusema tunafanya ukasuku.
Wako wanaume ambao kwa tamaduni zao, wanavaa vikoi. Wamasai nao wanavaa kivyao, kama tunavyoelewa. Wanawake wa Mashariki ya Kati na sehemu nyingine nyingi wanajifunika gubi gubi, kwa mujibu wa tamaduni zao. Hao wote ni wa kuheshimiwa, kwa vile wanatumia jadi na fikra zao, sio fikra tegemezi.
Tatizo ni sisi, ambao tumebambikizwa masuruali, kaptura na mashati kwa madai kuwa hayo ni mavazi ya wanaume, na tukakubali, na tukabambikizwa magauni na sketi kuwa mavazi ya wanawake, na tukakubali.
Kwa msingi huo, suali lako kuhusu mapadri kuvaa magauni, linatokana na wazo kuwa magauni wavae wanawake. Hili wazo tayari ni tatizo, kama nilivyoeleza hapo juu.
Safi broo nimeipenda bureee
Post a Comment