Tuesday, April 7, 2009

Ninakuja Tanzania: Nisome Vitabu Gani?

Jana nimepata barua pepe kutoka kwa kijana mmoja Mmarekani ambaye alikuwa mwanafunzi wetu hapa St. Olaf College, Minnesota miaka michache iliyopita. Ameniambia kuwa anaenda kutembelea Tanzania na Kenya wiki chache zijazo. Anauliza kama ninaweza kumpa ushauri wowote kuhusu namna ya kujiandaa, ikiwa ni pamoja na vitabu vya kusoma au filamu za kuangalia kabla hajasafiri.

Kwa waMarekani, kuuliza masuali ya aina hii na kujiandaa namna hii ni kawaida. Nazungumzia suala hilo mara kwa mara, kama unavyoona hapa. Tatizo ni upande wetu waTanzania. Sijawahi kumwona Mtanzania ambaye, anapopata fursa ya kwenda nchi ya nje, anatafuta vitabu vya kusoma kama sehemu ya maandalizi ya safari. Mtanzania huyu inawezekana anakwenda kufanya ziara au biashara au kutembelea ndugu na marafiki, kusoma au kufanya kazi. Anaondoka nchini na kwenda, bila kujishughulisha kama hao waMarekani wanavyojishughulisha. Ubalozi wa Marekani katika Tanzania una programu za kuwapeleka waTanzania Marekani kwa masomo. Wanajitahidi kutoa semina pale Ubalozini kuhusu hali ya Marekani, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya safari. Lakini sisi wenyewe waTanzania hatuna utaratibu kama huo. Tunawapeleka watu wetu nje, kwa mtindo wa "bora liende," au waende wakitegemea kudra ya Mwenyezi Mungu.

Je, hii ni sahihi? Tutaweza kuwa na ufanisi katika shughuli zetu nchi za nje ikiwa tunaingia huko bila ufahamu wa hali ya huko, tabia za watu, mila, desturi, na kadhalika? Tunaishije na watu wa huko? Tunaongeaje na watu wa huko? Tunafanyaje madajiliano na watu wa huko? Wanatuelewaje, nasi tunawaelewaje? Tunawaelewa wanaposema au kufanya jambo au tunabahatisha? Isije ikawa tunashangaa pasipo sababu, au tunakerwa na vitu ambavyo, kama tungekuwa tunavielewa, havingetukera. Isije ikawa tunawaudhi wengine kwa kufanya mambo yanayokubalika katika utamaduni wa kiTanzania, wakati huko ugenini hayakubaliki, ila sisi hatujui. Isije ikawa tunajikwamisha kwa kutofahamu hili au lile.

Katika dunia ya leo, tutaweza kweli kufanikiwa kwa kiwango tunachotegemea iwapo hatuna tabia ya kusoma vitabu?

5 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kuna rafiki zangu walokole wataenda marekani kuubiri injiri, mimi najuliza ni title za vitabu gani niwaagize. kama mnajua vizuri basi niandikieni lakini napendelea vya self realization kama vile vya eckharttolle.com, osho.com na vinginevyo. sio vile vya mahubiri, mapenzi na mafarakano.

John Mwaipopo said...

Profesa Salaam! Hii ni changamoto. binafsi naona aibu kutojua vitabu vya kuvipendekeza hapo. ingawaje kwa sasa nahenyeshwa na shule lakini siko na ufahamu wa kujua ni vitabu gani viko kwenye chati. sana sana kwa mtu mwingine ntampendekezea vile vitabu vyako viwili ulivyovipigia chapuo siku za nyuma.

ninachojifunza hapa ni kuwa watu wa mataifa ya magharibi huwa hawapendi kusimuliwa. wanapenda kusoma wenyewe ili waweze kutambua mbichi. ila huwa wana udhaifu mmoja- wa kuamini wanavyosoma pasi na kufanya uchunguzi wao binafsi.sio yote yaandikwayo ni ya kweli.

Christian Bwaya said...

Mswahili anapokwenda ughaibuni, sana sana atajiuliza wapi panapofaa kula 'raha' anazoziona-ga kwenye luninga. Kwa mtindo huu, maendeleo ya kweli tusahau. Tabia hii itaendelea kutuzalishia mafisadi wabobevu.

Mitaa imejaa baa kuliko maktaba. Tunatembeza mdomo kuliko kusoma. Maendeleo yanaendelea kuwa ndoto.

Bennet said...

Sisi tukisafiri bwana tunaenda kama wawindaji kwa sababu mwindaji hajui atamuwinda mnyama gani? mpaka amuone huko huko mawindoni, anachojua yeye ni kwamba atawinda mahali gani basi.

Mbele said...

Loo, jamaa mmenivunja mbavu leo, kwa michapo yenu, ambayo ni ukweli mtupu.

Suala hili la kujielimisha kuhusu tamaduni za wenzetu, na wao kujielimisha kuhusu tamaduni zetu, ni zito na muhimu sana. Huwa najiuliza, kwa mfano, viongozi wetu wanapokwenda ughaibuni, hawafurundi kweli?

Afisa wa ubalozi wetu mojawapo wa ughaibuni aliwahi kunidokeza kuwa vigogo wetu wanapotembelea ughaibuni huwa ni vigumu wakati mwingine kuwafanya wafuate taratibu za ughaibuni, kama vile kuwahi "appointments." Wanajisahau, wakidhani huku ughaibuni ni sawa na Bongo. Kumbe huku ughaibuni mambo ya kuchelewa ni mwiko.

Ndio matokeo ya kutozingatia elimu. Kama Bwaya anavyosema, Mswahili anaenda ughaibuni akiwa na wazo la kutanua matanuzi anayoyaona kwenye TV, au kama Bennet anavyosema, anaenda kwa staili ya mwindaji.

Kazi tunayo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...