Sunday, October 30, 2011

Wa-Islamu Vyuoni Marekani

Leo tulikuwa na mjadala mjini Faribault, Minnesota, kuhusu wa-Islam vyuoni Marekani. Walioandaa mjadala ni Anna na Rachel, wanafunzi wa Chuo Cha Carleton. Walengwa walikuwa ni wazazi na vijana wa ki-Somali, ambao ndio jamii ya ki-Islam inayofahamika hapa Minnesota ya Kusini Mashariki. Hapa kushoto tunaonekana wanajopo tukiwa mzigoni.




Rachel amejishughulisha na wa-Somali kwa kitambo. Aliwahi kufanya mahojiano nami miezi kadhaa iliyopita kuhusu changamoto zinazowakabili wa-Islam Marekani.

Rachel na Anna waliniomba nikawe mwanajopo katika mjadala wa leo, kwa vile wanafahamu ninafahamika na kukubalika katika jamii ile. Mjadala ulilenga kuwapa fursa wazazi na vijana kufahamu hali halisi, faida na changamoto za vyuo kwa wa-Islam ambao pia ni wahamiaji kutoka Afrika.

Wazazi na vijana walipata fursa sawa ya kuelezea mawazo yao, mitazamo, mategemeo, wasi wasi na mapendekezo. Zilijadiliwa changamoto wanazokabiliana nazo vijana wa kiIslam wanapowazia au kujiandaa kupeleka maombi ya kujiunga na vyuo vikuu, hadi masuala ya tofauti za dini na tamaduni wanazokabiliana nazo kwenye vyuo.





Mjadala ulihusu pia namna ya kujizatiti na hali hizo, na misaada iliyopo ya kuwawezesha wanafunzi wa ki-Islam kufanikiwa katika masomo vyuoni hapa Marekani. Msichana anayeonekana kwenye picha ya mwanzo pale juu, mwanajopo, ni mwanachuo. Alisema yeye kama mu-Islam anaona kuwa changamoto zilizopo vyuoni si kikwazo cha kumfanya kijana asiende chuoni.




Wazazi wote walisema na kusisitiza kuwa wanataka watoto wao wafanikiwe shuleni na vyuoni. Tatizo moja, ambalo walilitaja na kulisisitiza ni utaratibu wa shule za Marekani wa kuwaweka watoto katika darasa fulani kufuatana na umri. Kwa watoto wa ki-Somali ambao wamezaliwa au kukulia hapa Marekani, hili halina utata.





Lakini, watoto wa ki-Somali wanaofika kutoka Somalia, wanaweza kuwa na umri mkubwa lakini hawakupata nafasi ya kusoma kule watokako, kwa mfano kwenye makambi ya wakimbizi. Wanapowekwa katika darasa la watoto wa umri wao hapa Marekani, wanakuwa hawana msingi wa kuweza kufanikiwa katika masomo hayo, hata tu kwa upande wa lugha. Matokeo yake ni watoto hao kushindwa na kuishia kuacha kwenye vyuoni.

2 comments:

Christian Sikapundwa said...

Hongera sana Profesa,kwa kazi waliyokuomba ya kuwa mwanajopo,hawakukosea kwakuwa wewe ni mwanafalsafa ya maadili,hawakukosea.Walifahamu utatoa maadili mema kwa wanafunzi bila kujali imani zao.Kaza kamba bado Dunia inatambua mchango wako.

Mbele said...

Nashukuru Mzee Sikapundwa, kwa kutembelea kijiwe changu na kutoa maoni. Namshukuru Mungu kwa kunipa uzima na uwezo, ambayo ndio hazina ninayotumia katika kujielimisha kuhusu haya masuala ya jamii na kujumuika na wanajamii, kwa miaka yote hiyo, hadi nikafikia hatua ya kuwa mshauri makini katika masuala yanayowahusu, hasa yale yatokanayo na tofauti za tamaduni.

Kwenye huo mjadala niliombwa mahsusi niongelee changamoto zitokanazo na ukweli kwamba vyuo, kama taasisi zingine, zimejikita katika utamaduni husika, na kwa hivi mategemeo, taratibu, na mambo mengine ya vyuo katika utamaduni fulani yanaweza kuwa magumu kwa mtu wa utamaduni tofauti. Bahati nzuri hili ni somo ambalo nimelishughulikia kwa miaka, na jamii hapa Marekani zinatambua ufahamu na uzoefu nilio nao.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...