Showing posts with label somalia. Show all posts
Showing posts with label somalia. Show all posts

Thursday, November 14, 2019

Kijana Msomali Amekipenda Kitabu Hiki

Jana, nilikuwa posta hapa chuoni nikipata huduma. Ghafla nikasikia kwa nyuma ninaitwa, "Professor Mbele!" Nilipinduka nikamwona kijana mmoja, mwanafunzi wetu mSomali ananisogea. Aliniambia amesoma kitabu changu, akimaanisha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Nilifurahi, ila sikujua nimwambie nini, ila aliongezea kuwa alitamani kipatikane kama "audio book" ili mama yake aweze kusikiliza. Niliguswa sana, kwa sababu ninaelewa hali ya waSomali hapa Minnesota na Marekani kwa ujumla.

Wako wengi sana, wakimbizi au wahamiaji kutoka nchini kwao. Jimbo hili la Minnesota lina idadi kubwa ya waSomali kuliko sehemu nyingine duniani ukiachilia mbali Somalia yenyewe.

Ninafahamu pia kuwa waSomali hawakuwa na jadi ya maandishi. Utamaduni wao ni wa masilimuzi. Walipata mwafaka wa namna ya kuandika lugha yao mwaka 1972. Watu wazima wengi hawajui kuandika na kusoma, na wazee ndio kabisa.

Wote hao wako hapa Marekani, ambapo utamaduni ni wa maandishi. Ninafahamu changamoto zinazowakabili, kwani nina uzoefu katika masuala yao, ikiwemo fasihi simulizi na elimu. Kijana huyu alivyoniambia kuhusu mama yake, niliguswa sana. Nimeshampelekea ujumbe rafiki yangu mSomali kumwelezea suala hilo. Huyu tulishaongelea kutafsiri kitabu changu kwa kiSomali. Nimemwambia kuwa kutokana na kauli ya huyu kijana ya kutaka mama yake asome kitabu hiki, inabidi tukamilishe tafsiri halafu irekodiwe kama "audio book." Itachukua muda, lakini hii si hoja.

Saturday, June 13, 2015

Nimepata Kitabu "Infidel" cha Ayaan Hirsi Ali

Leo nimepata kitabu Infidel cha Ayaan Hirsi Ali ambacho nilikinunua mtandaoni tarehe 3 Juni. Ayaan alizaliwa Somalia, akakulia Somalia, Saudi Arabia, Ethiopia na Kenya. Kisha alihamia u-Holanzi, ambako aliwahi hata kuwa mbunge.

Katika kukua kwake alianza kuhoji malezi ya ki-Islam aliyoyapata, na hatimaye alijitoa katika dini hii na kuwa mtu asiye na dini. Hayo amekuwa akisimulia katika vitabu na mihadhara yake. Kitabu chake cha kwanza, ambacho sina, ni The Caged Virgin: An Emancipation Proclamation for Women and Islam, ambacho Salman Rushdie amekielezea hivi:

This is an immensely important book--passionate, challenging, and necessary. It should be read as widely as possible, because it tells the truth--the unvarnished, uncomfortable truth.

Mtazamo wa Ayaan Hirsi Ali umemletea matatizo makubwa tangu mwanzo. Anatafutwa kuuawa. Alikuwa chini ya ulinzi u-Holanzi na hatimaye alihamia Marekani. Bado anaandika, anatoa mihadhara na anafanya mahojiano.

Baada ya kusikia habari zake kwa miaka kadhaa, niliamua kutafuta ukweli mimi mwenyewe. Nilinunua kitabu chake kiitwacho Nomad, nikakisoma, kama nilivyoandika katika blogu hii. Nilifahamu kuwa kitabu chake kingine kinachofahamika sana ni Infidel. Sikuwa na haraka nacho, kwani ninanunua na kusoma vitabu vingine muda wote.  Lakini, hatimaye, nimeamua kukinunua nikisome. Sijui anasema nini katika kitabu hiki, na duku duku inanisukuma nisome.

Wednesday, October 26, 2011

Mwandishi Nuruddin Farah Katutembelea

Jana jioni, mwandishi maarufu Nuruddin Farah, mzaliwa wa Somalia, alikuja chuoni Carleton, hapa Northfield, kuongea na wadau kuhusu riwaya yake mpya, Crossbones, ambayo imechapishwa mwaka huu.









Nilienda kumsikiliza. Kama ilivyo kawaida katika shughuli za aina hii, vitabu vyake vilikuwepo, vinauzwa. Kwa vile ninavyo vitabu vyake vingine, nilinunua hiki kipya. Hapa pichani mwandishi anasaini nakala yangu. Bei yake ni dola 27.95, yapata shilingi 50,000 za Tanzania. Hiki ni kiasi kidogo sana ukifananisha na hela tunazotumia wa-Tanzania kwenye ulabu na makamuzi mengine. Bora kununua kitabu.




Ingawa bado sijaisoma riwaya ya Crossbones, kwa kufuatilia mazungumzo ya jana na kuiangalia kijuu juu, ni riwaya inayohusu Somalia kabla tu na baada ya uvamizi wa kijeshi uliofanywa na Ethipia miaka michache iliyopita. Ni riwaya inayoelezea athari za matukio hayo katika maisha ya wahusika.













Kwa bahati, nimeshamwona Nuruddin Farah mara kadhaa akihutubia, hapa Marekani. Vile vile, nimepata kufundisha baadhi ya maandishi yake. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1974. Nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kwa vile nilikuwa nasomea ualimu, nilienda shule ya wasichana ya Iringa kufanya mazoezi ya kufundisha. Kitabu cha Nuruddin Farah From a Crooked Rib kilikuwa kinatumika katika somo la "Literature."

Miaka ya hivi karibuni, hapa chuoni St. Olaf, nimefundisha pia riwaya zingine za Nuruddin Farah. Ni mmoja wa waandishi bora kabisa kutoka Afrika, ambaye ameshapata tuzo nyingi kwa uandishi wake.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...