Thursday, February 9, 2012

Mfanya Usafi Anajivunia Kitabu Hiki

Jioni hiii, hapa chuoni St. Olaf, nikiwa katika jengo kubwa ambamo kuna mgahawa, posta, na vyumba vya mikutano, amenizukia mzee moja ambaye ni mfanya usafi. Nimefahamiana naye miaka kadhaa.

Alivyoniona tu, kwa mbali kidogo, alinipungia mkono akiniita, "Come, come, come!," kama vile kuna dharura. Sikujua kuna nini, bali nikamfuata.

Alitangulia kuelekea kwenye sehemu alipokuwa anafanya usafi. Wakati ametangulia, akienda kwa kasi, aliniambia kuwa anataka nisaini kitabu. Alitokomea ndani kisha akaibuka na nakala ya Matengo Folktales. Niliguswa sana, nikasaini, naye akafurahi sana, kama vile amepata tuzo fulani.

Mzee huyu, ambaye jina lake ni Maurice, alishaniambia miezi mingi ilyopita kuwa anasoma kitabu changu. Sikushangaa kwa jinsi ninavyowafahamu wa-Marekani. Mtu aliyelelewa katika utamaduni usiothamini vitabu atashangaa inakuwaje mzee achape kibarua cha kusafisha majengo, halafu atumie dola nyingi kununulia kitabu. Kwa jinsi ninavyowafahamu hao wa-Marekani, kwenye suala la vitabu wako makini. Hudhuria tamasha la vitabu, au nenda kwenye maduka ya vitabu, utajionea mwenyewe.

3 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Inafurahisha kwa kweli yaani naamini ni raha gani unajisikia. Na naamini huyu baba naye alifurahi sana. Ingekuwa hivi wengi wanatumia vicent vyao kununu vitabu ingekuwa safi sana.

Mbele said...

Huyu ni mfanya usafi wa Marekani. Kwetu sijui kama hata waziri, mkurugenzi, au mbunge ananunua na kusoma vitabu.

Hao watu wanapitapita sana huku ughaibuni, na kuna maduka ya vitabu kwenye viwanja vya ndege. Sijui kama yuko anayepita humo na kununua vitabu vya kwenda navyo nyumbani.

Anonymous said...

Big up sana kwa kutufagilia Wamatengo, nami walau najisikia naishi. Ujue wasomi wa kimatengo ni wengi ila tukishaingia miji ya makabila mengine...too bad, hatukumbuki kwetu. NAIPENDA SANA MATENGO LAND!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...