Thursday, February 16, 2012

Watu Tuliosoma Darasa Moja

Kitu kimoja kinacholburudisha moyo wangu ninapokuwa Tanzania ni kukutana na watu tuliosoma pamoja. Mwaka jana, wakati napita Songea, nilionana na Bwana Alto Kapinga, ambaye anaonekana nami katika picha hapa kushoto. Anatoka Lundumato, katika wilaya ya Mbinga. Tulisoma darasa moja, kuanzia la tano hadi la nane, katika Seminari ya Hanga, 1963 hadi 1966. Hiyo ilikuwa ni shule bora kabisa mkoani Ruvuma. Ingawa tulisoma zamani vile, tumebahatika kukutana ghafla mitaani Songea mara kadhaa katika miaka iliyofuata.

Baada ya kupita Songea, nilienda hadi kwetu milimani u-Matengo. Wakati wa kutembelea Maguu, nilikutana na Padri Simon Ndunguru, ambaye anaonekana nami katika picha hapa kushoto. Picha tulipiga kijijini Chicago. Padri Ndunguru, mwenyeji wa Mbinga, tulisoma darasa moja, kuanzia la tisa hadi la kumi na mbili, katika Seminari ya Likonde, 1967-70. Hiyo ilikuwa ni moja ya shule bora kabisa Tanzania kwa kufaulisha wanafunzi.

Tunapokutana namna hii, tunamshukuru Mungu kwa kutuweka hai hadi leo, kwani ni mapenzi yake tu, wala hatustahili. Tunawakumbuka pia wenzetu ambao wameondoka duniani.

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nimefurahi kama ndo vile ilikuwa mimi. Inapendaza sana kukutana na mtu uliyekuwa ukisoma naye au hata kucheza naye au mwalimu aliyekufundisha. NAWATAKIENI MAISHA MEME NA MZIDI KUDUMISHA MAWASILIANO.

Mbele said...

Nimeona katika maisha yangu kuwa tunapokutana watu tuliosoma pamoja, au tulihenya pamoja JKT (ambayo kwangu ni shule muhimu) huwa tunafurahi kukumbushana na kuongea hili au lile.

Habari ya kuwepo kwangu Songea mjini mwaka jana iliwafikia jamaa wengine wawili ambao tulisoma darasa moja Hanga na Likonde. Hao ni Abel Mapunda (nadhani ni wa Tingi) na Mathias Nyera (wa Maguu). Hatukupata fursa ya kuonana, ila walinipigia simu. Ni miaka mingi sana hatukuwa na mawasiliano kabisa.

Shukrani kwa kutuombea, nawe na wale mliosoma pamoja nawaombea.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...