Monday, February 27, 2012

Kwa Kuzuia Misa, wa-Kwere Mmechemsha

Nimesoma taarifa kuwa waumini wa Kanisa Katoliki la Lugoba, wamemzuia padri asisome misa, eti kwa vile anawasema vibaya. Napenda kusema machache kuhusu suala hilo.

Wakwere mmechemsha, tena mno. Mimi ni mtani wenu, kwa hivyo lazima niwape vidonge vyenu!

Mimi pia ni m-Katoliki, na ninafahamu fika kuwa waumini hatuna wadhifa wa kuzuia misa isisomwe. Hapo mmekosea kabisa! Mbali ya hilo kosa lenyewe, tambueni kuwa mmewakwaza hata watoto, ambao tunapaswa kuwalea katika njia ya kuheshimu misa na mamlaka ya Kanisa. Tena bora mwende mkaungame.

Kama mlikuwa na malalamiko dhidi ya padri, mngeweza kabisa kukaa naye kikao, au kulalamika kwa askofu, na suluhu ingepatikana. Kuzuia misa ni kitendo kiovu sana. Sijawahi kusikia kitu kama hiki.

Inaonekana padri alikuwa anawatolea uvivu kwa yale aliyoyaamini kuwa yanakwamisha maendeleo yenu. Sasa nyinyi badala ya kutafakari ili kubaini kama alikuwa anasema ukweli au la, na kama ilikuwa ni ukweli, badala ya kukiri mnarukia hoja ya kwamba anawakera. Kumbukeni kuwa wakati mwingine ukweli unauma. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, ni kwamba padri ana uchungu na maendeleo yenu.

Mmekosea sana, wa-Kwere.

--------------------------------------------------------------------

Taarifa ya tukio imechapishwa katika gazeti la Habari Leo:

--------------------------------------------------------------------

PADRI wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Lugoba Jimbo la Morogoro, Philipo Mkude amezuiwa na waumini kuongoza misa baada ya kudaiwa kuwakashifu waumini wa kabila la Wakwere.

Padri Mkude alizuiwa kuongoza misa jana asubuhi parokiani hapo, baada ya waumini zaidi ya 200 kuandamana wakiwa na mabango zaidi ya 20 wakidai ahamishwe kwa kuwa amewatukana katika mahubiri yake, kwamba watoto wao ni wachafu na wao wamebaki kucheza ngoma badala ya kufanya maendeleo.

“Tumechoka na mahubiri ya huyu Padri, kila akihubiri kanisani lazima atuseme Wakwere,
tumemkosea nini?

Mara atuseme tu masikini, mara watoto wetu wachafu na hatuwapeleki shule tunashindia ngoma, tumechoka, hatumtaki,” alisema muumini ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.

“Leo tumemzuia asisome misa kabisa, hakuna haja maana hakuna amani kanisani, hatujui ana kitu gani na sisi, sijui kwa sababu parokia hii ipo kwa Wakwere?

“Hata Jumatano ya Majivu wiki iliyopita katusema tena, eti watoto wetu ni wachafu sana ukilinganisha na makabila mengine, hii ni kashfa.”

Wakwere ni moja ya makabila katika Mkoa wa Pwani linalopatikana wilayani Bagamoyo,
lakini katika mfumo wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Lugoba ipo chini ya Jimbo la Morogoro.

Muumini huyo aliyezungumza kwa simu na gazeti hili jana, alidai mahubiri ya Padri huyo ya kuwasema Wakwere hayakuanza siku za karibuni, bali ni ya muda mrefu na yamekuwa kama ya kusutwa badala ya kulishwa Neno la Mungu.

“Hali hiyo imesababisha watu kutokwenda kanisani wakijua leo Padri huyo anaongoza misa, lakini akiongoza Katekista, misa inajaa utadhani Askofu amekuja, tunachotaka hapa ni Padri mwingine, kama Askofu anatujali atuletee mwingine,” alisema muumini huyo.

Kwa mujibu wa muumini huyo, walifanya maandamano ya amani kuanzia saa moja asubuhi kabla ya misa iliyopaswa kuanza saa 2.30 asubuhi huku wakiimba nyimbo za dini na mabango yenye ujumbe mbalimbali ukionesha kauli tofauti za padri huyo na namna walivyomchoka.

Alidai pia hali hiyo ilisababisha misa isifanyike baada ya Polisi pamoja na Diwani wa Msoga,
Mohamed Mzimba kufika kanisani hapo na kumshauri Padri huyo aondoke eneo hilo na kwenda Parokia ya jirani ya Chalinze umbali wa kilometa 22 ili kurejesha amani eneo hilo.

Diwani Mzimba alipoulizwa alikiri na kusema; “nilifika hapo nilipopewa taarifa kwamba hali si
shwari, mimi si wa Kata ya Lugoba, lakini mwenzangu anaumwa…kweli wameandamana,
lakini kwa amani na wana madai yao.”

“Ujumbe wameutoa kwa mabango, mengine yaliandikwa hatumtaki kapoteza kikombe chetu
cha dhahabu cha divai na mengine anatukana Wakwere, mimi si Mkristo sasa sijui zaidi, ila kuondoa jazba waliyokuwa nayo, Polisi walimshauri Padri aende kanisa la Chalinze huku viongozi wa kanisa wakimaliza mzozo,” alisema Mzimba.

Katekista (Mwalimu wa Mafundisho wa Dini) wa Parokia hiyo, Prosper Semindu alipoulizwa
kuhusu tukio hilo, alikiri kutokea na kueleza kuwa haelewi sababu ni nini ila waumini hao walikuwa na mabango huku wakiimba nje ya kanisa na kusababisha misa isifanyike.

Padri Mkude alonga
Padri Mkude alipoulizwa jana alikana kuwatukana na badala yake alidai kuwa katika mahubiri yake amekuwa akiwasisitiza kusoma kama ambavyo viongozi kadhaa, akiwemo Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiwaeleza.

“Watu kuwasema Wakwere kuhusu elimu ipo tangu zamani, nilikuwa nawasisitiza hata
wachimbe vyoo, hawataki, wanauza mashamba ambayo ni urithi kwa watoto, niliwaambia
jamani msiuze mtashindwa kusomesha watoto, hawanisikii, wanabaki kucheza ngoma, sasa
nimewatukana wapi?

“Jumatano ya Majivu niliwaambia wabadilike hasa kuhusu elimu, kwamba tufanye bidii katika shule yetu hapa Lugoba kidato cha nne wapo wanafunzi 250 kutoka Pwani, angalau 70 waende kidato cha tano na tukipata watoto angalau 10 vyuo vikuu miaka 10 ijayo tutakuwa na
wasomi wengi, leo wanasema unatunyanyasa na kututukana,” alisema Padri Mkude.

Alisema alipoona maandamano aliwaeleza kuwa kama amefanya makosa ya jinai watoe taarifa kwa vyombo vya usalama na kama ni makosa ya kikanisa, wafikishe mahali husika, lakini si kuvamia ibada na kufanya maandamano bila ruhusa.

Walivyoanzisha vurugu
Akielezea hali ilivyokuwa, Padri Mkude alisema wakati akijiandaa kuanza ibada baada ya kengele ya kwanza na ya pili kulia, muumini mmoja alimfuata kumsalimu na kisha alimwambia hawataki aongoze Misa na kama akifanya, hakutakuwa na usalama kwenye Misa.

“Wakati huo tofauti na siku nyingine, hakukuwa na mtu kanisani, niliwauliza kwa nini,
wakasisitiza niondoke, huko nje walikuwa wengi wanaimba, nikawaambia kama mmekataa misa, basi.

Viongozi wa Baraza la Walei walitoa taarifa Polisi, wakaja na mimi nikaondoka,” alisema Padri Mkude.

Alisema hivi sasa yupo Parokia ya Chalinze na anasubiri uamuzi wa kikao kati ya Ujumbe wa Askofu wa Morogoro na kundi la waumini hao ili kumaliza suala hilo. Mpaka jana jioni, kikao hicho kilikuwa kikiendelea.

2 comments:

tz biashara said...

Tatizo wananchi hawapendi kuambiwa ukweli na sasa nimeamini ikiwa hata kuelimishwa na mkuu wa kanisa pia ni ngumu.Sasa hapa kuna kazi kubwa maana hata chama kingine kikichukua nchi basi sio kazi ndogo kuelimisha watu.

Watu kwa ngoma,pombe na ngono hapo humuelezi mtu anaona kama unampotezea wakati wake.Unapomwambia jambo jema mtu anaona unamnyanyasa kumbe unamtengenezea maisha yake.

Sifahamu lugha ipi aliitumia padri kuwaambia hawa waumini lakini analowaambia padri ni ukweli na wajirekebishe.Maendeleo hayaletwi na ngoma na lazima wajue namna ya kulea watoto na kuwapeleka shule wakaelimike.

tz biashara said...

Profesa naomba niende nje ya mada kidogo.
Nilikua nauliza kuhusu mfumo wa elimu kwa Tanzania unauonaje kwakuwa wewe ni Profesa na ni mwalimu vilevile.Kulikuwa na ishu mtu ameiweka ktk globalpublisher jana na ilihusiana na mwalimu kama sikosei na ametokea America.Alikutana na wanafunzi wa chuo kikuu dar lakini alisikitishwa kwakuwa wanafunzi hawakuweza kujieleza vizuri ktk lugha ya kiingereza.Na kingine alisema ni wavivu wakufikiri.Labda kama unamuda upitie mtandao na uitafute ilikuwa ni jana.

Sasa ktk majadiliano kila mtu alikuwa na ujumbe wake.Na mimi nikaona ni vizuri kukuuliza nione mapendekezo yako.

Mimi binafsi naona elimu inapatikana kwa lugha yoyote na maendeleo ya elimu yanapatikana zaidi ktk lugha unayoitumia ili kurahisisha masomo na kuelewa kwa undani zaidi.Na vilevile nadhani kama itapendekezwa lugha ya kingereza basi nadhani ilipaswa itumike kutokea shule ya vichekechea ili kumpa mtoto confidence zaidi ktk masomo yake ya mbele.

Nadhani huu mfumo tuliokuwa nao sio mzuri kwasababu kwa imani yangu naona inamchanganya mtoto ktk masomo na kumvunjia confidence.Mimi binafsi nilipomaliza shule ya msingi nilipoingia secondary ilikuwa ni shida tupu kwani sikuwa naelewa kitu chochote kwasababu masomo yanabadilika na kuwa ktk lugha ya kingereza.

Yaani elimu yetu ingewekwa ktk lugha moja kuanzia vichekechea kama ni English au kiswahili kwani huku nchi nyingine za ulaya zinatumia lugha zao na hawajui kingereza na utakuta mtu ana elimu ya hali ya juu.

Na kingine tuangalie Kenya jinsi walivotupita kielimu na nadhani kiliwasaidia sana kuchagua lugha moja tu kuitumia ktk elimu na hii inamfanya mwanafunzi kuwa na confidence nzuri ktk masomo.

Sijui wewe unasemaje ktk hili au nakosea nikisema lugha ktk elimu itumike moja kama ni kiswahili au kingereza na isiwe ya kuanza na kiswahili na kumalizia na kingereza hii mimi naona inachangia kushushia kiwango cha elimu kwetu.Na kuna mtu alisema kwamba kutumia kiswahili ktk elimu itakuwa ngumu kwasababu kiswahili ni lugha bado changa yaani haijakamilisha maneno mengi hasa ktk somo la sayansi hususan physics chemistry na biology.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...