Saturday, February 18, 2012

Sera ya Madini Tanzania: Wizi Mtupu

Nimeguswa na katuni hii ya Kijasti, ambayo nimeiona wavuti. Naamini kuwa sera ya madini Tanzania ni wizi mtupu. Hebu fikiria, kwa mfano: serikali ya CCM inatuambia kuwa inaipitia mikataba mibovu ya madini, ili kuziba mianya inayoliletea Taifa hasara, na ili kuhakikisha kuwa Taifa linafaidika na madini hayo.

Hapo nina suali: Je, waliosaini mikataba hii mibovu walikuwa wajinga wasioweza kuelewa kilichoandikwa, au walikuwa wamelewa gongo waliposaini, au walikuwa ni mafisadi? Na je, kwa nini hawawajibishwi?

Halafu, kwa kuzingatia kuwa serikali ya CCM bado inawaambia hao wanaoitwa wawekezaji waje nchini, je, imeshaandaa mikataba mipya ambayo inatoa kipaumbele kwa nchi? Kukosekana kwa uwazi katika suala hili la madini kunanipa hisia kuwa serikali ya CCM kwa makusudi inaihujumu nchi.

Ni fedheha kwa Tanzania kuonekana kuwa ni nchi maskini, na hata hao tunaowaita viongozi wanasema Tanzania ni nchi maskini, wakati ni nchi tajiri kwa rasilimali mbali mbali. Dhahabu yetu, kwa mfano, inayaneemesha makampuni kama Barrick Gold. Ni aibu kwa Tanzania.

2 comments:

Emmanuel said...

Wanapitia kwa miaka kumi bado tunaibiwa. Halafu waziri anatuambia ni tatizo la Africa wakati anajua wazi Botswana wala Namibia hawaibiwi kitu kwenye madini yao.

Sisi yetu ujinga na kukumbatia uwizi kama ulivyosema "wizi mtupu"

Mbele said...

Kwangu kama mwananchi ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa, tafsiri yangu ya uchaguzi wa 2010 ni kuwa CCM ilifanya kila juhudi na hila ibaki madarakani kuulinda huu ufisadi.

Naamini kwa dhati kuwa kama Dr. Slaa angekuwa rais, angekuwa ameufumua mfumo huu wa ufisadi. Naamini anajua mengi kuhusu huu ufisadi, na amethibitisha kuwa haogopi mtu. Tatizo tu ni kuwa hana nguvu za dola.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...