Saturday, February 11, 2012

Matangazo ya Biashara

Wengi tumeshaliona tangazo hilo hapa kushoto, kwani limetokea sana mitandaoni. Linachekesha na kuvutia. Linatosha kumfanya mtu atafute mgahawa huu ili akashuhudie mwenyewe huduma za huyu Hassan.

Mtangazaji ametumia ubunifu wa kuwateka watu kisaikolojia. Anatafuta biashara, lakini anafanya ucheshi pia. Hiyo ni mbinu ya aina yake.

Kuna biashara za namna mbali mbali. Ziko zinazouza bidhaa na nyingine zinauza huduma. Kwa vyovyote vile, ubora wa kinachouzwa ni msingi wa mafanikio kwa mfanyabiashara.

Lakini, pamoja na ubora wa kinachouzwa, ni muhimu kwa mfanyabiashara kuielewa saikolojia ya wateja. Mteja ajisikie amekaribishwa vizuri, sio tu auziwe alichokitafuta. Ajisikie amethaminiwa. Kumvumilia na kumjibu vizuri mteja mkorofi ni muhimu. Kumshukuru mteja ni muhimu.

Mfanya biashara daima ajiulize mteja wake anajisikiaje wakati wa kuhudumiwa na baada ya kuhudumiwa. Mteja asiyeridhika, au aliyeudhika ni balaa. Atakwenda kuwaambia wengine maudhi yaliyomfika, nao hawataenda mahali hapo, labda iwe hakuna mahali pengine. Ni silika ya binadamu kuwa tukiwa na machungu moyoni, tunahitaji kumpata mtu au kuwapata watu wa kuwaelezea, watusikilize. Ndivyo mteja aliyeumia anavyofanya. Biashara ikididimia, mfanyabiashara ajitafakari mwenyewe kwanza, kabla ya kutafuta wachawi

Kwa upande mwingine, mteja aliyeridhika na kufurahi ni mpiga debe mkubwa. Hatakosa kuwaeleza wengine. Ni ukweli usiopingika kuwa maamuzi yetu ya nini cha kununua, au wapi, mara nyingi tunafuata ushauri wa watu wengine. Mwulize mtu mahali kama Dar es Salaam akuambie teksi ipi uchukue au ukalale gesti ipi, au uende mgahawa upi, au baa ipi, hutakosa kuelezwa. Atakuelekeza kule ambako alipata au anapata huduma bora. Kila mmoja wetu ni mpiga debe, kwa maana kwamba tunawaambia wenzetu wapi kwa kupata huduma au bidhaa bora. Tunafanya hicho kibarua kwa furaha, bila malipo, na mfanyabiashara mwenyewe tunayempelekea wateja huenda hajui. Mambo yanakwenda kwa mtindo wa watu kuambiana. MMambo

Masuala haya yananivutia na yana umuhimu kwangu kwa vile nami naendesha kikampuni ambacho nilielezea habari zake hapa. Ninapata changamoto kadha wa kadha, lakini kwa kusoma vitabu na kuhudhuria warsha, najifunza namna ya kuzikabili na kuiboresha kampuni yangu. Suala la kumridhisha kila mteja, kwa mfano, iwe ameagiza kitabu au ameomba ushauri, ninalizingatia sana.
(Mchora katuni inayoonekana hapa juu ni Nathan Mpangala)

4 comments:

tz biashara said...

Hiyo ni customer kero.Kwa wenzetu ktk makampuni mengi huwa wanajaribu kuwapa mafunzo muhimu kila baada ya muda wa miezi fulani au baada ya mwaka ili kujenga sifa ktk kampuni.Lakini kwetu mtu akipewa kazi huifanya kwa ubinafsi wake ili mwisho wa mwezi apate mshahara wake akatanue mjini.Na utakuta hakuna nidhamu kazini kuanzia kwa bosi wake hadi wa chini.Maana pengine bosi wa kampuni anatembea na wawili watatu humo humo.Sasa nidhamu itatokea wapi.Na kingine kinachochangia nadhani kupata vijikozi vya bure humo kazini ili kukumbusha wafanyakazi jinsi ya ufanyaji kazi pamoja kuwa karibu na kuwaenzi wateja wao na sio kuwakebehi na kujiona kama umefika.Na kama bosi mwenyewe hana nidhamu ya kujiheshimu basi siku zote wafanyakazi wa chini watakuwa wanafanya kazi bila nidhamu.Kama bosi ni mkali na hapendi utani na wafanyakazi wake na kuonyesha nidhamu basi wafanyakazi wote watafanya kazi kwa uangalifu na kuwajali wateja.

Mbele said...

Mwaka jana mjini Mbeya nilikumbana na kastama kero iiliyonikasirisha karibu nipasuke kichwa, katika hoteli niliyofikia. Ipo karibu tu na stendi, ila nimesahau jina lake. Sidhani kama nimewahi kukasirika namna hii maishani, na mhudumu badala ya kukiri makosa yake, akawa anafanya kiburi! Bahati yake alikuwa upande wa pili wa kaunta, na palikuwa na vyuma vinavyokuzuia kumfikia. Vinginevyo, leo tungeongea mengine.

Halafu, mwaka juzi nilipata kastama kero ya mwaka kwenye hoteli niliyofikia Arusha, sio mbali na Golden Rose. Nilikasirika, lakini wahudumu walinisikiliza tu, na baada ya muda mfupi, walipoona nimeenda zangu baa hapo pembeni, wakaanza kupiga stori zao na meneja ambaye naye nilishampa vidonge vyake.

Yaani nilihisi, kama unavyosema, hao mabinti na meneja wana yao. Waliendelea tu kusogoa kama vile hakuna kastama aliyeudhika kupita maelezo. Sina hata hamu ya kuiona hoteli ile. Na hiyo ya Mbeya ndio kabisa. Sitaki hata kuifikiria, ingawa ni nzuri. Kastama kero yake imeniumiza sana.

CHARLES NAZI said...

Nataka kutangaza biashara kwenye blogu yako jee mnaruhusu?

Anonymous said...

iiShukran kwa maelezo yako mufti , lakini dhana ya matangazo kamwe haija penya kwa njia sawa barani afrika,huku bidhaa nyingi zikiwa zatengenezewa ng'ambo na na matangazo yako bado yanabuniwa huko huko, ndio unaona vitu kama "minute maid"ile juisi iko sokoni, Guiness wanasema "made of more"endapo tutabuni matangazo yetu sisi wenyewe tunawasiliana vizuri zaidi na hata mauzo yatakwea, utamanduni una jukumu kubwa katika mawasiliano ukiangalia chaneli za ngámbo an yale wanayotuandaliaulinganishe na vipindi vyetu vya humu afrika utapata kuwa hawa wazungu hawa tuelewi mimi nimekuwa nikifanya matangazo ya radio na televisheni zaidi ya miaka 20 sasa na nimesafiri kote katika afrika ya mashariki nanina mengi naweza sema kuhusu matangazo ya biiashara

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...