Saturday, February 6, 2010

Wamarekani Safarini Malawi

Leo nilikwenda mjini Chippewa Falls, katika jimbo la Wisconsin, umbali wa maili 123 kutoka Northfield, ambapo naishi. Nilienda kuongea na kikundi cha wa-Marekani wanaojiandaa kwenda Malawi kwa shughuli za kujitolea. Nilialikwa na Mama Diane Kaufmann, ambaye anaonekana kushoto kwangu, katika picha hapa juu. Yeye ameenda Malawi mara kadhaa, katika wadhifa wake kama mratibu wa mpango wa ushirikiano baina ya dayosisi ya Kanisa la kiLuteri Kaskazini Magharibi ya Wisconsin na Malawi. Ana uzoefu wa kupeleka vikundi vya wanadayosisi Malawi katika mpango huo. Vile vile tumeshirikiana kwa miaka kadhaa katika kuendesha mafunzo kwenye kituo cha Luther Point.
Kikundi nilichoenda kukutana nacho leo kinaenda Malawi kuwashughulikia watu wenye matatizo ya macho, na kuwagawia miwani. Wanatarajia kufanya shughuli hizo Karonga na Chitipa.
Baadhi yao wameshaenda Malawi, na kwa wengine hii itakuwa ni mara yao ya kwanza. Mama Kaufmann aliniita niongee nao kuhusu masuala ninayoongelea katika kitabu changu cha Africans and Americans. Alinieleza kabla kuwa washiriki wote watakuwa wamekisoma kitabu hiki kabla ya ujio wangu. Kama kawaida, mazungumzo na watu waliojiandaa namna hii yanakuwa ya kina, kwani yanalenga katika kufuatilia yale ambayo wamesoma.
Walifurahi kuwa nami, kwani walijisikia kama vile wameshanifahamu, kutokana na ninavyojieleza kitabuni. Nami nilifurahi kuwa nao na kuwasisitizia mambo ya msingi kuhusu kuishi au kushughulika na watu wa utamaduni tofauti na wetu. Kwa vile hao wanaenda kwa shughuli za matibabu, mazungumzo yetu yalilenga zaidi kwenye hali halisi ya kushughulika na watu katika hospitali. Tofauti za tamaduni zinajitokezaje katika mazingira ya hospitali.
Kwa bahati nzuri haya ni mambo ambayo nimeyawazia kwa muda mrefu, na katika kitabu changu nimeyagusia. Vile vile, nimekuwa nikijipatia uzoefu katika mazungumzo na wanafunzi wa masomo ya uuguzi wanapojiandaa kwenda Tanzania kimasomo.

Baadhi ya wasafiri hao walisoma katika chuo cha St. Olaf, na tulipata fursa ya kuongelea na kupiga soga kuhusu maisha chuoni hapa. Baadhi wamesoma maandishi yangu mengine, kama vile Matengo Folktales na Notes on Achebe's Things Apart. Niliona wazi kuwa hao ni watu makini ambao wanajishughulisha kufahamu habari za huko waendako.

2 comments:

Bennet said...

Nadhani walikuwa na maswali ambayo yalihitaji kukuuliza ana kwa ana, nawatakia safari njema wajiandae na malaria

Mbele said...

Kwa ujumla wa-Marekani huwa wanajitahidi kuulizia masuali na kujiandaa vilivyo na taarifa mbali mbali kabla hawajasafiria nchi ya nje. Tahadhari za malaria au hatari zingine wanakuwa nazo kichwani. Nimeelezea sana hayo kwenye kitabu changu.

Ni tofauti na sisi wa-Swahili. Sisi tukipata safari, ni kufungasha mizigo na kuelekea uwanja wa ndege. Hutamkuta m-Swahili ananunua kitabu asome kuhusu kule anakoenda. Ni kuingia pipa na kutokomea kusikojulikana. Hatuna wasi wasi. Humo pipani ni kukanyaga bia tu hadi mwisho wa safari :-)

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...