Sunday, February 14, 2010

Fursa za Kuwatoa Upepo wa-Tanzania

Pamoja na kuwa kazi yangu ya msingi huku Marekani ni kufundisha, ninajishughulisha pia na mipango ya uhusiano baina ya vyuo vya Marekani na Tanzania na nchi zingine za Afrika. Mipango hii ni ile ya kupeleka wanafunzi Afrika. Kwa upande wa Tanzania, napata pia fursa ya kufanya mahojiano (intavyuu) na wasomi wanaotafuta nafasi ya kuja Marekani kwa masomo zaidi au utafiti.

Hizi ni kazi za kujitolea, lakini nazifanya kwa moyo moja, nikizingatia umuhimu wake kwa upande wa Marekani na nchi zetu, kwani, pamoja na kutoa fursa mbali mbali kwa wahusika, zinakuza maelewano duniani.

Mtu unapokuwa na fursa au wadhifa kama wangu, wa-Tanzania wanasema umeula. Wanaamini unalipwa hela nyingi sana, tena dola, si madafu. Pili, wanategemea kuwa unatumia fursa hizi kujitajirisha sana kifedha kwa msingi wa "akili mkichwa." Zaidi ya yote, wa-Tanzania wanataka wakuone unaishi maisha ya hali ya juu, si uwe unakula pilau au chapati kwenye vihoteli vya Ubungo au Kinondoni.

Siku moja, miaka ya tisini na kitu mwishoni, nikiwa Chuo Kikuu Dar es Salaam kwenye shughuli hizi za intavyuu, nilipanda dala dala pale Mwenge kuelekea Tegeta. Niliposhuka kituoni Tegeta, nilikutana na wa-Tanzania wanaonifahamu. Walishangaa kuniona nimepanda dala dala, wakaanza kunisema kwa nini ninahangaika na dala dala, wakati ningeweza kujipatia gari kutokana na hizi hizi intavyuu ninazowafanyia wasomi.

Mmoja wao aliniambia: "Sisi hapa Bongo, intavyuu ya kufagia ofisi za kampuni tunatoa laki tatu kwa bosi. Sasa je intavyuu za kwenda Marekani? Mbona mtu atakupa milioni, tena kwa hiari yake! Profesa Mbele unajitakia mwenyewe matatizo ya dala dala."

Sikujua namna ya kujitetea, nao waliendelea kunipa vidonge vyangu. Nategemea kwenda tena Tanzania, miezi ya usoni, kwenye shughuli nilizoongelea, na nafahamu kuwa vidonge zaidi vinaningoja.

4 comments:

Anonymous said...

Profesa Mbele,

Waswahili wanasema,"kutoa ni moyo sio utajiri".Nadhani kwakujitolea kwako unapanda mbegu zitakazo zaa matunda ya kudumu;na kudumu kweli kweli!

Aluta Kontinua.Ndimi,

Majaliwa

Albert Kissima said...

Hongera sana Mzee Mbele. Binafsi najivunia sana na juhudi zako. Ni ishara ya wazi kabisa kuwa popote ulipo, wawawaza wa-Tanzania na Tanzania kama nchi ktk swala zima la maendeleo. Wakwambiao kuwa unapanda daladala nami nashindwa kuwaelewa ni watanzania gani, pengine ndio wale wale wanaoshinda kwenye vilabu vya pombe na huku watoto hawapati ada ya shule,na wanakufa njaa, pia ndio hao hao,walalamikao kuwa viongozi wa serikali wanafuja mali za uma kwa kumiliki magari ya bei ghali na mambo mengine chungu mbovu. Wa-Tanzania tulio wengi yaonekana twapenda sana "Lakshari" na pengine ndio hasa kwa namna moja ama nyingine inatukosesha maendeleo. Wengi wetu hatuna issue ya"lazima" na "ihari". Ufahari twauona ndio hasa mafanikio.

John Mwaipopo said...

kasumba ya kuwa kitu kama gari ni ufahari bado i miongoni mwa watanzania wengi. gari ni kitu cha kuonyeshea (show off), na sio kitu cha kufanyia kazi. wakati fulani huwa naamua kuacha gari yangu na kutembea kwa miguu umbali fulani kwa malengo mawili. mosi ni kuona maendeleo ya sehemu nitakayotembea maana ukiwa ndani ya gari unatakiwa utazame barabara tu(ambayo haina maendeleo mageni). pili huwa nataka kunyoosha viungo. katika pilikapilika hii hukutana na watu ninofahamiana nao na wao huniuliza vipi mbona gari nimeiacha. kwao gari inafaa ikupeleke kokote ikiwezekana hata bafuni.

nikipanda daladala huwa najifunza na kujionea mamboa mengi yatokeayo ndani ya dala dala na nje ya dala lala.

tabia ya kuendesha gari kupindukia ina hasara zake. niliwahi kuendesha kwenda kutafuka kitu fulani mbali sana ilhali kitu kama hicho kipo mtaa wa pili ambao sikuwahi kuutembelea kwa mguu wala kwa gari.

Jaduong Metty said...

Professor,

Kama ulivyosema, hii kitu ni utamaduni tu. Wote tunakuwa na matarajio na tafsiri ya vitu kutokana na uelewa wetu, uelewa ambao mara nyingi unatokana na mazingira.

Kuna ndugu yangu, wakati ametua tu Marekani kwa mara ya kwanza, aliwahi kuniuliza naenda kutafuta PhD lini. Nilipomuuliza kwa nini, jibu ikawa ni kwamba PhD sasa hivi mali Tanzania. Niliishia kutikisa kichwa.

Naelewa kwa mtazamo wake, nilikuwa napoteza "nafasi" wakati mimi najiuliza kwamba hiyo PhD ina nafasi gani kwenye malengo yangu mapana ya maisha.

Swali, ambalo ni gumu, ni hili: unawezaje kuvua ujuzi wako wa tamaduni nyingine, mfano wa Kimarekani, unaporudi nyumbani ili kukwepa migogoro?

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...