Leo nimeagiza mtandaoni kitabu cha hadithi za Luis Bernardo Honwana wa Msumbiji kiitwacho We Killed Mangy Dog and Other Stories. Kwa wiki kadhaa, nimemwazia sana mwandishi huyu, ambaye kitabu chake hiki nilikipenda sana nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1973. Nilivutiwa na jinsi alivyoielezea maisha nchini Msumbiji, ambayo ilikuwa daima mawazoni mwetu kutokana na vita vya ukombozi vilivyoongozwa na FRELIMO.Nimeamua kununua kitabu hiki wakati huu kwa sababu katika wiki hizi nimeandaa orodha ya vitabu vya kufundishia kozi yangu ya "Post-colonial Literature" muhula wa kiangazi, mwezi Julai na Agosti. Kwa mara ya kwanza tangu nianze kufundisha hapa Chuoni St. Olaf, nimeamua kuingiza kazi ya fasihi kutoka Msumbiji.
Sitafundisha We Killed Mangy Dog and Other Stories, ingawa ningeweza kufanya hivyo kwa furaha kabisa. Badala yake, nitafundisha riwaya ya mwandishi mwingine maarufu Mia Couto iitwayo The Tuner of Silences, ambayo sijaisoma. Hata hivyo nimeona nijipatie hiki kitabu cha hadithi za Honwana, nilichokipenda enzi za ujana wangu, nikisoma tena wakati nangojea kufundisha The Tuner of Silences,
Ninangojea kwa hamu kusoma na kufundisha The Tuner of Silences. Ninangojea kwa hamu kujikumbusha na kuwaeleza wanafunzi kuhusu Msumbiji, historia yake, historia ya utamadini na fasihi yake. Ninapangia kuandika zaidi kuhusu hayo katika blogu hii wakati utakapowadia.