Monday, April 9, 2012

Foleni Ubungo

Tatizo moja kubwa la mji wa Dar es Salaam ni msongamano wa magari na vyombo vingine vya usafiri mabarabarani. Picha hizi nilipiga leo eneo la Ubungo, nikiwa nateremka kwa mguu kukaribia kituo cha daladala.

Kuna sababu kadhaa zinazoleta msongamano huu, kama vile barabara kuwa ndogo. Hata hivyo, sababu nyingine, ambayo haisemwi, ni tabia ya kila mwenye gari kutaka kutumia gari lake, hata kama watu wawili wanakaa mtaa moja na wanafanya kazi sehemu moja kule mjini.

Wenzetu Marekani wana utamaduni wanaouita "car-pooling," yaani watu mnasafiri pamoja katika gari la mmoja wenu, hata kama wote mna magari, Tanzania mambo ni tofauti. Wote wanaendesha magari yao, hata kama wanatoka mtaa mmoja na wanakwenda sehemu hiyo hiyo ya kazi kule mjini. Halafu, mwenye gari anaona ni lazima apande gari hata kama anakwenda sehemu ya karibu, ambapo angeweza kwenda kwa mguu.

Magari binafsi yanawazuzua wa-Tanzania. Je, kuna anayekumbuka kuwa kutembea kuna manufaa kwa afya? Kuna anayekumbuka kwamba utitiri wa magari katika barabara za mahali kama Dar es salaam unachafua sana hewa? Kwa hoja hii ya uchafu wa hewa, siamini kama Dar es Salaam ni mahali salama kama ilivyo vijijini.

5 comments:

Anonymous said...

nikweli profesa dsm sio salama hatakidogo kwanza pananuka harufu mbaya watu sio wastaarabu,moshi wa magari yaani tabu tupu lakini kijijini burudani kabisa kwanza unakuvyakula ambavyo bado ni freshi kutoka shambani hivyo dar si sehemu salama kabisa

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

"Car-pooling" kwa Bongo? Thubutu! Nani aonekane masikini? Watu watamjuaje kuwa ana gari? Atapataje wanawake kirahisi kwa kufanya "car-pooling?"

Niliwahi kumuuliza rafiki yangu mmoja ambaye ndiyo kwanza alikuwa amenunua Land Cruiser V8 mpya kwa milioni 94 sababu yake ya kununua gari la bei mbaya namna hiyo wakati angeweza kununua Toyota Corolla na akabakiza pesa kibao kwa kufanyia shughuli zingine? Nilimuuliza hivi kwa sababu alikuwa na mke na mtoto mmoja tu na hakukuwa na sababu ya kununua Land Cruiser - gari kubwa lenye uwezo wa kubeba watu wanane. Unajua jibu nililopata?

"Land Cruiser ni gari linalokuongezea status"

Jibu hili lilinishangaza sana. Watu wako tayari kutumia mamilioni ili tu kuonekana wana "status" kubwa katika jamii. Na wakati huo huo unaweza kumwona mzungu milionea akiendesha baisikeli kwenda kazini. Hana tatizo na mambo ya "status"

Jamii yetu imesimika amali zake katika mihimili tenge na ndiyo maana mimi huwa naamini kuwa ufisadi hautakaa uishe bila kuwa na mabadiliko ya kifikra kwanza. Leo hii Profesa Mbele ikitokea JK akakupa uwaziri au "ulaji" mwingine, ukija kuacha kazi ukiwa masikini basi jamii itakucheka. Waziri mzima umestaafu ukiwa masikini kwa nini? Kwa nini hukuiba ukatajirika? Mbona umestaafu ukiwa una "status" ya chini? Land Cruiser liko wapi? Hekalu je? Usishangae ukiishia kuitwa "fala" tu!

Lakini ukifisadika kikwelikweli na kutajirika kupita kiasi walaaa! Utasifiwa sana na kuonwa kuwa ni "shujaa" Waangalie mafisadi ambao sasa ni mabilionea; na waadilifu wachache waliostaafu wakiwa masikini utaona.

Inasikitisha lakini hii ndiyo jamii yetu !!!

Anonymous said...

Masangu sawa kabisa mimi hapo inavaa katambuga makusudi na sio kwamba sina uwezo wakununua viatu sasa inakuwa tabu kwa mkewangu anayetaka hiyo status maana mimi ninachokifanya niwajenge wanangu kusudi wajewakue wakielewa kuwa kumbe hata ukivaa kawaida haina tabu.

Mbele said...

Enzi za Nyerere, busara fulani kuhusu mambo hayo ilitumika, sawa na tunavyoona kwenye nchi tunazoziita zilizoendelea, ambako unawakuta wazito katika basi, treni, au hata baiskeli. Soma, kwa mfano, hapa.

Egidio Ndabagoye said...

Masangu ngoja wenyewe wakusikie.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...