Juzi tarehe 31, Dr. Charlotte (Shoonie) Hartwig na mimi tulitoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Minnesota, juu ya mwandishi Aniceti Kitereza. Huyu ni mwandishi muhimu ambaye, hata hivyo, hafahamiki sana. Mama Shoonie amekuwa akiandika kitabu ambacho nami nimechangia, na mhadhara wetu ulihusu kitabu hiki ambacho tunategemea kukichapisha.
Kitereza alizaliwa mwaka 1896 katika kisiwa cha Ukerewe kilichomo katika Ziwa Victoria, upande wa Tanzania. Alisomea katika shule za wamisheni, na alipomaliza aliajiriwa kazi kadhaa. Alivyozidi kukua alipata dhamira ya kuhifadhi mila na desturi za zamani za wa-Kerewe, ili zisipotee. Kama sehemu ya juhudi hiyo aliandika riwaya katika lugha ya ki-Kerewe, ambao aliukamilisha mwanzoni mwa mwaka 1945. Andiko hili ni hazina ya mila na destruí za wa-Kerewe wa zamani, ila Kitereza aliandika kwa mtindo wa hadithi ya kubuni, ili wasomaji wasichoke kusoma.
Baada ya juhudi na mahangaiko ya miaka mingi ya kutafuta mchapishaji, na kufuatia ushauri wa marafiki zake wa-Marekani, Kitereza aliutafsiri mswada wake kwa ki-Swahili. Hata hivyo, aliendelea kungoja kwa miaka mingi hadi mwaka 1980 ambapo mswada ulichapishwa kama kitabu, Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka na Ntulanalwo na Buliwhali.
Mama Shoonie ni mtu pekee aliyesalia mwenye taarifa za ndani za Kitereza, kwani yeye na mumewe, Dr. Gerald Hartwig, walimfahamu vizuri Kitereza baada ya kuonana naye kwa mara ya kwanza mwaka 1968 Ukerewe. Mbali ya kukutana naye mara kwa mara miaka ile ya mwanzo, waliendelea kuandikiana barua hadi miaka ya mwisho wa maisha yake. Kitereza alikuwa hodari wa kuandika barua; ananikumbusha waandishi kama Ernest Hemingway na Shaaban Robert.
Katika mhadhara wa juzi, Mama Shoonie alielezea maisha ya Kitereza na mambo aliyofanya kama mwandishi. Maelezo yake aliyaambatanisha na picha za Kitereza, mke wake, na familia nzima ya Hartwig. Watoto wa familia ya Hartwig walikuwa wadogo sana wakati huo. Mama Shoonie alielezea kuwa Kitereza alikuwa anajituma sana katika shughuli yake ya kuhifadhi mila na destruí za wahenga kwa kusukumwa na suali ambalo alilitunga mwenyewe, "Tunawajibika kuwafundisha nini watoto wetu?"
Ilipokuja zamu yangu, nilielezea kwa ufupi uandishi wa Kitereza kwa mujibu wa mtazamo wangu kama mwana fasihi. Nilisisitiza masuala kadhaa muhimu yanayojitokeza katika taaluma ya fasihi ya Afrika, hasa suala la uandishi katika lugha za ki-Afrika na suala la tafsiri. Niligusia jinsi riwaya ya Bwana Myombekere inavyoweza kutupa mtazamo mpya kuhusu historia ya riwaya ya ki-Afrika, na jinsi inavyoweza kuchambuliwa sambamba na kazi za waandishi kama Daniel O. Fagunwa na Amos Tutuola wa Nigeria, Gakaara wa Wanjau wa Kenya, na Shaaban Robert wa Tanzania. Huu utakuwa ni mtazamo wa fasihi linganishi.
Nimesoma tafsiri ya Kitereza ya riwaya yake. Ki-Swahili chake, ingawa kinatofautiana na ki-Swahili sanifu, kina ladha na mtiririko wa hadithi simulizi za lugha za ki-Bantu kama vile lugha yangu ya ki-Matengo. Kwa msingi huo, ninaipenda tafsiri ya Kitereza. Riwaya yake imetafsiriwa kwa ki-Faransa na ki-Jermani, lakini tafsiri hizo, kwa mujibu wa Profesa Gabriel Ruhumbika, zina walakini. Kauli ya Profesa Ruhumbika ina uzito sana, kwani lugha mama yake ni ki-Kerewe na pia yeye ni mashuhuri katika uwanja wa kutafsiri.
Profesa Ruhumbika mwenyewe ametafsiri kwa ki-Ingereza riwaya ya Kitereza kama ilivyoandikwa ki-Kikerewe, na tafsiri yake imechapishwa kama Mr. Myombekere and His Wife Bugonoka, Their Son Ntulanalwo and Daughter Buliwhali. Katika kuisoma tafsiri hii, nilivutiwa nayo, sawa na nilivyovutiwa na tafsiri ya ki-Swahili ya Kitereza mwenyewe. Ni tafsiri ambayo ninapendekeza isomwe na yeyote. Hivyo hivyo, ninakipendekeza kitabu cha Mama Shoonie kijacho. Ni kitabu chenye taarifa nyingi, zikiwemo barua na picha, ambazo ulimwengu haujaziona.

No comments:
Post a Comment