Thursday, June 19, 2014

Tamthilia ya Shakespeare Imenijia Katika Ndoto

Usiku wa kuamkia leo, niliota ndoto fupi, na katika ndoto hii nilijikuta nakumbuka maneno ya Morocco, mhusika katika tamthilia ya Shakespeare, "The Merchant of Venice." Maneno yenyewe ni haya:

As much as he deserves! Pause there, Morocco,
And weigh thy value with an even hand,
If thou be'st rated by thy estimation,
Thou dost deserve enough; and yet enough
May not extend so far as the lady....

Nimefurahi kuwa nimeikumbuka ndoto hii, na maneno haya ya Morocco, wakati akijaribu bahati yake ya kumpata mrembo Portia.

Nilipokuwa kijana, kati ya waandishi niliowapenda sana ni Shakespeare. Marafiki zangu na mimi tulipenda sana hotuba za wahusika wa tamthilia za Shakespeare, tukafurahia kuzikariri, tukistaajabu umahiri wa Shakespeare katika kutumia lugha na kuelezea masuala mbali mbali.

Shaaban Robert alimwenzi sana Shakespeare. Alisema kuwa akili ya Shakespeare ilikuwa kama bahari, ambayo mawimbi yake yaligusa kila pwani ya dunia.

Labda wakati umefika wa kusoma tena tamthilia za Shakespeare.

2 comments:

Anonymous said...

Wanasema ndoto ni tokeo la ubongo kujipanga na kurekebisha seli za ubongo.
Lakini huwa nashindwa kuelewa ni kwanini ndoto nyingine huwa zinakuja na kama utabiri fulani?

Mbele said...

Asante kwa ujumbe wako. Nikiongezea hapo hapo, ni kwamba wataalam mbali mbali wameongelea suala hili la ndoto. Mfano ni Sigmund Freud, mmoja wa waasisi wa taaluma ya "psychoanalyisi".

Kwa mujibu wa wataalam ni kuwa ubongo haulali, hata tuanpokuwa fofofo usingizini, bali huwa katika kuchambua matukio yaliyojiri na kuyapanga kwa namna ambayo akina Freud walitufundisha namna za kuyaelewa.

Watu wa kale walizichukulia ndoto kama utabiri wa mambo yajayo. Hawakuzichukulia kijuujuu au kuzipuuza tunavyofanya leo.

Ninapofundisha somo la "folklore" ninahusisha sana mada hii ya taaluma ya ndoto.

Narudia tena, asante, kwa kutupeleka katika mkondo huu wa fikra.