Sunday, June 29, 2014

Maelezo Mafupi Kuhusu Kitabu Changu cha "Africans and Americans"Wiki kadhaa zilizopita, katika blogu hii, walijitokeza watu kwa jina la "anonymous" wakisema hili au lile kuhusu kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kitu cha kushangaza ni kuwa hapakuwa na dalili yoyote kuwa watu hao walikuwa wamekisoma. Jambo hili halikubaliki popote, nami niliwashutumu hao akina "anonymous."

Kitu kingine cha kushangaza ni kuwa wote wametokomea gizani; hawajasikika tena. Ingekuwa ni watu makini, walioelimika, wangeonyesha kile kinachoitwa "intellectual curiosity." Wangeweza kukitafuta kitabu hiki wakakisoma, halafu wakaja na uchambuzi wao uliojikita katika kuelewa wanaongelea nini.

Utaratibu ni kuwa mtu unasoma kitabu na kisha unakijadili. Tena ni bora ukinukuu vifungu kutoka katika kitabu hicho, ili kuthibitisha kauli zako. Huu ndio utaratibu unaotegemewa na kukubalika. Hakuna hata "anonymous" moja aliyenukuu neno lolote kutoka katika kitabu changu. Kama kitabu hujakisoma, ni bora ukae kimya, uwasikilize waliosoma.

Kuna wanablogu kadhaa ambao wamekisoma kitabu hiki na wamekiongeleqa kwa msingi huo. Mifano ni Jeff Msangi, Simon Kitururu, Yasinta Ngonyani, Dada Subi, Bwaya, na Sophie Becker. Hao wote, baada ya kukisoma kitabu changu hiki, wamekiongelea mtandaoni.

Haingekuwa lazima akina "anonymous" wanunue kitabu changu, kwani kinapatikana katika maktaba kadhaa. Lakini napata picha kuwa watu hao hawajaelimika, kwani hawakuonyesha hiyo "intellectual curiosity" kuhusu suala hilo ambalo walikuwa wanalitolea kauli. Kwa mtazamo wangu, ishara muhimu ya kuelimika ni kuwa na hii "intellectual curiosity" maisha yote.

Utaratibu ni kuwa mtu unasoma kitabu na kisha unakijadili. Mimi kama mwandishi nimewahi kuelezea mazingira yaliyonifanya nikaandika kitabu hiki, na sababu za kuandika. Nilielezea malengo yangu. Katika video ambayo nimeiweka hapa, nimeongelea kwa kifupi sana, mazingira yaliyonifanya niandike kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na namna wasomaji wanavyokiona. Sikuelezea kila kitu, bali ni muhtasari tu. Tena, nilikuwa sijajiandaa, bali yalikuwa ni mazungumzo ya papo kwa papo.

Ni muhimu, tunapokiongelea kitabu, pamoja na mengine yote, kuangalia malengo ya mwandishi, ambayo huwa yametajwa katika kitabu chenyewe. Tathmini ya kitabu inapaswa kuangalia pia iwapo mwandishi amefanikiwa kutimiza malengo yake au la. Tunapokuwa tumekisoma kitabu, tunakuwa na uwezo na haki ya kuelezea chochote kilichomo, kiwe ni kizuri au dosari.

Kama una ufahamu wa kutosha, ukaelezea dosari za kitabu, unakuwa umemsaidia mwandishi. Mimi mwenyewe ni mhakiki, na nimechapisha tahakiki za vitabu kadhaa, nikielezea ubora na dosari zake. Na hilo ndilo nililotegemea, na ndilo ninalotegemea, kutoka kwa yeyote anayeongelea vitabu vyangu. Ni suala la kuelimishana.

1 comment:

Christian Bwaya said...

Kuna ka-utamaduni kabovu kameanza kuzoeleka kwenye jamii yatu. Na ni kama tumeanza kukakubali (siji labda shauri ya udogo wangu, huenda kalikuwepo enzi na enzi). Watu wanazungumza na kujadili mambo kwa kuyasikia sikia tu kwa waliyoyasikia mahali au basi hisia tu. Tumekuwa watu wa mijadala ya hisia.

Mfano hivi sasa ukipita kwenye vijiwe vingi unakuta watu 'wanajadili' rasimu ya Katiba. Ukiuliza aliyeisoma, hakuna, au basi ni wachache. Majadiliano yote yanafanyika kwa kutumia hisia zinazosikika kwenye vyombo vya habari! Kwa hiyo unakuta misimamo ya watu kuhusu Rasimu hiyo ya Katiba inategemea kinachozungumzwa na walioisikia rasimu ikijadiliwa kwenye vijiwe. Yaani aliyemsikia aliyeisoma, naye anaenda kusimulia alichosikia na kujigeuza bingwa wa kuwaaminisha watu kuwa anajua kilichozungumzwa kwenye rasimu. Wakati ukweli ni kwamba kasikia kwa aliyesikia. Hajasoma.

Kinachofedhehesha ni kwamba hali hii ya kuamini tetesi na hisia imejengeka hata kwenye masuala ya imani. Na hatustuki. Misimao yetu mingi kuhusu imani na dini zetu inatokana na mahubiri ya washeikh, Mapadre na Wachungaji. Sisi wenyewe hatujasoma hivyo vitabu vitakatifu. Tunasikia tu. Hatusomi biblia lakini tunajiita Wakristo. Hatusomi Quran na tunajiita Waislamu. Kichekesho. Utakuwaje muumini wa mafundisho usiyoyajua vyema?

Sasa sishangai mtu kutoka alikotoka anajipa kazi ya kufanya pitio la kitabu ambacho hata hajakisoma. Anajadili hisia. Na kama ilivyo kawaida, hisia hizi nyingi hujengwa kwenye misingi ya mategemeo potofu. Hisia za jumla jumla tu zinazotupa mahitimisho yasiyoendana na hali halisi.

Nina hakika kuwa bado tutahitaji miaka mingi zaidi kuuvunja utaratibu huu. Tusichoke kukumbushana hapa na pale.