Ndoto yangu tangu ujana wangu ilikuwa ni kuwa mwalimu. Nilihitimu chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1976, nikateuliwa kuanza kufundisha pale, katika idara ya "Literature." Ndoto yangu ikawa imetimia. Ninaipenda kazi yangu na ninawapenda wanafunzi wangu.
Tangu mwaka 1991, ninafundisha katika idara ya kiIngereza hapa katika chuo cha St. Olaf, jimbo la Minnesota. Naleta picha kutoka miaka michache iliyopita nikiwa na wanafunzi wangu wa somo la kuandika kiIngereza. Hili ni moja kati ya masomo ninayofundisha.
Inapendeza kuwasaidia wanafunzi kujifunza matumizi ya lugha rasmi kwa nidhamu na usahihi kabisa. Lugha ina mitego na changamoto nyingi. Tuchukulie mfano wa mwanafunzi wa kubuniwa ambaye jina lake ni Mark. Tuchukulie kuwa Mark ameandika, "The reason why I spoke that way was because I was not feeling well."
Hapa Marekani, jamii ambayo kiIngereza ni lugha mama yao, watu wengi huandika kwa kiwango hicho, na wengi hawafikii kiwango hicho, kwani hutumia maneno, misemo, na miundo isiyo rasmi, ambayo wameizoea tangu utotoni, tofauti au kinyume na itakiwavyo katika lugha rasmi.
Kwa kuwa lengo langu ni kufundisha matumizi ya lugha rasmi iliyo bora kabisa, namshinikiza na kumwelekeza mwanafunzi Mark kurekebisha sentensi yake. Namwambia kuwa ametumia maneno mengi mno na asirudie neno au dhana katika sentensi. Anajikuna kichwa, anajitahidi, na hatimaye anaandika hivi: "The reason I spoke that way was that I was not feeling well"
Hiyo sentensi ni afadhali kuliko ilivyoandikwa mwanzo, kwa sababu angalau ameondoa neno "why" na neno "because," ambayo ni marudio ya "the reason." Lakini, ingawa rekebisho lake limeboresha sentensi, haijafikia kiwango cha juu kabisa cha ubora. Kwa hiyo ninaendelea kumshinikiza Mark atafakari zaidi. Labda, hatimaye anaandika hivi: "I spoke that way because I was not feeling well"
Hiyo ni bora zaidi, lakini si mwisho wa safari. Ninaendelea kumshinikiza Mark hadi aandike: "I spoke that way because I was unwell." Hapo niko tayari kumwachia, ingawa naweza kumshauri pia kuwa hilo neno "unwell" linaweza kutafutiwa neno tofauti na sentensi ikawa na ladha zaidi. Lakini hili badiliko si muhimu.
Ninajisikia raha sana kumfikisha mwanafunzi kwenye hatua hiyo, na ninajisikia raha kumwona mwanafunzi mwenyewe anavyofurahi kutokana na kutambua makosa na mitego aliyopitia. Hiyo furaha ninayopata haielezeki. Ndio siri ya mimi kuupenda ualimu namna hiyo. Sitaacha ualimu kamwe, labda nitakapokuwa sina tena uwezo wa kufundisha.