WaTanzania wenzangu, nimechapisha kijitabu, "Notes on 'Song of Lawino'" na sasa naleta hoja kuhusu bei yake.
Kijitabu hiki nimekiandika kutokana na jinsi ninavyoipenda fasihi. Nilipenda kuandika uchambuzi wa "Song of Lawino." Nimetumia miaka mingi kutafakari na kuandika. Ingekuwa ninalipwa kwa kila saa na siku niliyofanya hiyo kazi, ningekuwa tajiri.
Sasa kumbe matokeo ya shughuli yote hii ni kijitabu cha kurasa 70 tu. Watu watauliza bei yake ni shilingi ngapi. Ni dola 12, ambayo ni karibu shilingi 28,000. Najua kuwa wako watakaoshangaa bei hiyo kwa kijitabu cha kurasa chache.
Je, bei ya kitabu inawakilisha nini? Ndio thamani ya kitabu? Yaani tafakari yote na mawazo yote yaliyomo humu thamani yake ni hii shilingi 28,000? MTanzania akienda baa na hizi hela, atakunywa bia ngapi? Je kitabu hiki thamani yake ni sawa na hizi bia chache?
Binafsi, nakataa. Inatakiwa kitabu hiki kiuzwe angalau shilingi milioni moja. Angalau milioni moja, ukizingatia jasho nililotoa, na mikwamo niliyopitia. Niliyoandika humu nayaona kuwa ya thamani kubwa. Angalau kiuzwe milioni moja. Shilingi 28,000 ni dhuluma tupu, mchana kweupe.
Halafu, hiki ni kitabu ambacho hakitanunuliwa, labda na watu wachache sana. Huenda zisiuzwe nakala 10. Kingekuwa kitabu cha udaku, kingeuzika kwa kiasi fulani. Lakini hiki ni kitabu kikavu cha kitaaluma. Kitasota bila wateja. Hakitaniletea hela, labda visenti vichache. Ni kazi isiyo na ujira.
Mimi siandiki vitabu kwa ajili ya kupata hela. Nilitumia muda wangu wote huu kuandika hiki kitabu nikijua kuwa hakitauzika, labda nakala chache sana. Kinachonifanya niandike si pesa bali kuipenda kwangu fasihi. Nitaendelea kuandika.