Friday, September 15, 2017

SHAMBULIZI DHIDI YA TUNDU LISU LASIKITISHA WATANZANIA: Maaskofu waonya

MAASKOFU Katoliki Tanzania wamelaani vitendo vya vurugu, mauaji na uvunjifu wa amani vinavyoendelea nchini na kusema kuwa vitendo hivyo vinalifedhehesha Taifa kwa kuwa ni dhambi, uhalifu na siyo utamaduni wa Tanzania.

Wamesema hayo katika tamko walilolitoa Septemba 11, 2017 ambapo wametaka vitendo hivyo vikomeshwe mara moja. “Tunatamani kuona wale wote walio nyuma ya matukio haya ya vurugu, mauaji, utekaji na utesaji wanatafutwa na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” imeeleza sehemu ya tamko hilo.

Akiongelea tamko hilo la maaskofu, Makamu Mkuu Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania, Padri Dkt. Charles Kitima amesema kuwa Maaskofu wametoa tamko hilo kwa kuwa ni haki na wajibu wao wa msingi kama taasisi iliyo na wajibu ndani ya jamii ya kulea maadili ya watu na kulinda utu wa kila binadamu.

Amesema kuwa Kanisa kama taasisi lina jukumu la kuhakikisha malezi ya uadilifu kwa viongozi na kwa umma yanazingatiwa na yanapewa kipaumbele, na kuongeza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 19 ndiyo inayowapa uhalali maaskofu kuelekeza jamii juu ya kulinda utu, amani, haki na wajibu msingi ambazo ni stahili ya kila mtu kwa sababu ya ubinadamu wa kila mmoja.

Aidha Dkt. Kitima amesema kuwa Taifa la Tanzania halikuzoea matukio ya namna hii, jambo linaloashiria kupwaya kwa utawala wa sheria. “Kudhuru ama kupoteza maisha ya mtu yeyote si tendo linalokubalika mbele ya Jamii, Mungu na mbele ya Katiba yetu ya Muungano. Ni kinyume na utawala wa sheria. Hili sasa ni tatizo kubwa linalokiuka Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Matukio haya yamesikitisha watu wote wenye kuheshimu utu wa binadamu hata kama hakubaliani na wengine.

Mungu hakubaliani na uovu huu ndio maana maaskofu wanaonya wahusika na watekelezaji wa matendo haya kuacha tabia hiyo kwani inapingana na mpango wa Mungu wa kumuumba binadamu ili afurahie hadhi ya utu na uhai wake, zawadi pekee yenye kuonyesha sura na mfano wa Mungu aliye hai.

Nchi lazima ilinde uhai wa kila binadamu ndani ya Tanzania hata kama ni uhai wa mhalifu. Serikali iendeshe shughuli zake ikizingatia na kuongozwa na katiba ambayo inapaswa iheshimiwe kwani hakuna mtu wala kiongozi yeyote aliye juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Amesema.

Utu hauthaminiwi kwa sasa.

Pia Padri Kitima ameongeza kuwa kwa sasa utu (human dignity) wa mtu hauthaminiwi ambapo binadamu anaweza kupotezewa heshima na hata maisha yake, na kuonya kuwa wale wanaofanya hivyo wasipopewa onyo Taifa litaelekea pabaya.
“Taifa linalopuuza utu linajiangamiza. Utu tunaozungumza hapa ni wa kila mtu siyo wa mtu fulani tu. Hata muhalifu ana haki zake za msingi. Ibara ya 14 inatambua haki ya uhai wa kila mwanadamu, awe msafi au asiwe msafi, awe muhalifu au la, ana haki ya kulindwa. Unapojiamulia kuua mtu kwa sababu yoyote ile inaleta uvunjifu wa katiba.
Ni mahakama pekee ndicho chombo kinachoweza kutoa hukumu dhidi ya mhalifu.Taifa letu linaelekea kubaya kwa sababu utu haupewi tena kipaumbele, tunaweka kipaumbele vitu kuliko utu, tukumbuke kuwa Mungu hapendi uovu wetu wa kupuuza utu wa ndugu zetu, tutawajibika mbele ya Mungu,” Ameeleza.

Kadhalika amekumbusha kuwa ni wakati mwafaka sasa, wale wanaoshughulika na masuala ya umma warejee katika misingi ya Taifa ya mshikamano, umoja na amani kwa kila mtu.

“Hatuwezi kuwa tunang’oa mizizi ya matatizo yaliyopo kwa njia ovu; ni kweli Serikali inapambana na rushwa na wizi wa rasilimali za umma, lakini yote hayo lazima yafanyike kwa kuzingatia utu na utawala wa sheria. Hatuwezi kuondoa uovu kwa kutumia uovu kwa sababu sisi sote tutawajibika mbele ya jamii na mbele ya Mungu kwa kuulinda utu. Anayepuuza utu hata afanye kizuri namna gani, hakitakuwa na baraka za Mungu.

Tunaondoa uovu kwa kutumia sheria na njia nzuri iliyokubaliwa na watu wenye mamlaka ya nchi hii. Vyombo vya dola vimepewa mamlaka ya kuendesha nchi kwa utashi wa raia wa Tanzania hata kama wana uwezo wa kufanya lolote watakalo bado kutotii utashi wa watanzania ni usaliti dhidi ya utashi wa wananchi na katiba yetu ya watanzania.” Amesema.

Akielezea matukio ya kuvamiwa kwa ofisi za wanasheria, kupigwa risasi kwa Mbunge Tundu Lisu na kesi mbalimbali zinazoendelea nchini, Dkt. Kitima amesema kuwa matamko mengi yametoka kwa viongozi kadhaa dhidi ya Tundu Lisu, lakini yeye alikuwa anasimamia taaluma yake kama mwanasheria anayemtetea mwanadamu pia ambaye anafuata misingi ya haki za binadamu.

“Baba wa Taifa tarehe 25 oktoba 1961 alipokuwa akizindua Chuo Kikuu cha kwanza Tanzania (Dar es Salaam University College) alisema tunaaanza na kitivo cha sheria ili kujenga Taifa litakaloongozwa na sheria, na pia aliasa watanzania waheshimu haki za watu wote,, yeye Nyerere amekuwa kielelezo cha uongozi bora na kuweza kutatua matatizo makubwa na hata kung’oa ufisadi wa kila aina kwa kuongozwa na utaratibu wa kisheria. Alikuwa na uwezo wa kujenga mwafaka na wenye hoja tofauti na zake kwa njia ya masikilizano (consensus building) kwa kuongozwa na sheria ndio maana tumekuta rasilimali nyingi na amani na heshima kwa viongozi wetu.

Na hiyo ndio ilifanya aseme hatuwezi kuwa Taifa huru bila Chuo Kikuu chetu wenyewe akitaka tuongozwe na waelewa wa fani mbalimbali ili tuweze kujijengea Taifa huru letu wenyewe tuheshimu wataalamu wetu hata kama ushauri wao ni mgumu kuupokea., taifa hili ni letu wote na kila mmoja anahitaji kusikilizwa. Kuwapuuza wenye maoni tofauti si utanzania, tuwasilize na kuwaelimisha kama hawaelewi na hata watuelimishe nasi pia,” Amekumbusha.

Amesema kuwa hata mhalifu ana haki ya kutetewa mahakamani kwa sababu ya utu wake, lengo likiwa ni kumsaidia atendewe kwa haki kisheria na wala si kutetea uovu wake. Kila mtu ana haki ya kujitetea mahakamni kwa kupewa hudumu za kitaalamu ikiwepo huduma ya utaalamu wa kisheria.

Amesema sisi sote ni wadhambi na Kanisa lipo kwa ajili ya kuwabadilisha wadhambi waache uovu waongoke na ndicho hicho kilichomfanya Yesu awe kati yetu wanadamu. Wanasheria wanapowatetea wahalifu nia yao ni kuwasaidia pia wabadilike kwa kuheshimu sheria zetu hasa Katiba. “Lakini ikumbukwe kuwa wapo baadhi ya wahalifu wamesingiziwa. Sasa unapoona wanasheria wananyimwa majukumu yao ya kitaaluma kuwatetea watu kama hawa inakuwa siyo halali. Zaidi ya hayo Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kila mmoja ana haki ya kusimamia maoni yake ikiwa ni pamoja na maoni ya taaluma yake. Hawa watu wasinyimwe haki ya kuwatetea wahalifu mbele ya mahakama ili haki itendeke kisheria, kwa sababu wahalifu bado utu wao una thamani kuliko maslahi yetu yapitayo, uhai unadumu milele,” Ameeleza.

Kwa nini matukio hayo yanalaaniwa?

Aidha amebainisha kuwa maaskofu wanalaani matukio hayo na kuwataka wote waliohusika kuacha mwenendo huo kwani hakuna jamii iliyoweza kukomesha uhalifu ama uovu wowote kwa kuangamiza wengine. Ni jukumu la kueneza utawala wa sheria na uheshimu wa haki za kila mtu ndipo tutajenga Taifa lenye mafanikio kiuchumi na kisiasa.

Serikali ndiyo yenye jukumu la kulinda utu wa kila mtu na mali zake. Viongozi wa dini zote wana haki ya kuwahabarisha viongozi wa Serikali juu ya uadilifu, thamani ya utu, haki msingi za kila mtu na juu ya tunu za taifa ambazo ni WATU, ARDHI, SIASA SAFI, UONGOZI BORA. “Tumejenga nchi hii kwa sababu ya siasa safi, tulikwepa siasa chafu ndio maana Tanzania ilipata uhuru bila vita vya mtutu, na hivi Tanzania ilikuwa kimbilio la ukombozi wa Afrika. Tuliitwa USWISI ya Afrika. Tukipuuza utu wa mtu yeyote hata tujitetee vipi hatutaaminika wala kupata maendeleo yeyote. Kila nchi ina historia yake. Historia yetu ndio hiyo na wala haiwezi kuwa historia ya China wala ya Marekani. Hata watanganyika/watanzania wenye mawazo tofauti waliheshimiwa na kuondoka nchini walipoona hawako tayari kwendana na tunu zetu.

Tanzania tumekuwa Taifa lisilo na waasi bali Taifa lenye watu wenye mitazamo tofauti. Tulipokubali mfumo wa Vyama vya siasa lengo letu lilikuwa kujifunza kuachiana madaraka kwa njia ya uchaguzi wenye kuheshimu Katiba na sheria. Na hivi vyama vya kisiasa vilivyosajiliwa vyote vina hadhi sawa.

Wanaopata fursa ya kuongoza hupewa ushirikiano kwa mujibu wa sheria. Wapinzani wa kisiasa wa Tanzania ni watu wema na wanastahili kutendewa kiutu na siyo kuonewa na kunyanyaswa. Ni hatari kubwa kitaifa kuwanyanyasa wapinzani. Kazi ya viongozi wa dini ni kuipa Serikali taarifa ambayo ina ukweli kwa pande zote, kisayansi na kiutu. Maaskofu wanategemea nia njema ya walengwa wa ujumbe wao kuuheshimu na kuutendea kazi kadiri ya taratibu za kisheria,” Amehimiza.

Tanzania ni jamii yenye kupenda amani na umoja na haya ni matunda ya kuulinda na kuuheshimu utu wa kila mtu. Ujumbe wa Maaskofu unawakilisha kiu ya kila mtanzania kupinga ukiukaji wa misingi ya utu.

CHANZO: BLOGU YA TEC

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...